Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Vigogo wapigana vita
Vigogo wapigana vita
By Habari Tanzania | Published  01/11/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Irene Mark

NI dhahiri kwamba, sasa taifa limeingizwa katika mzozo mkubwa wa kimaadili unaoweza kubadili mwelekeo wa mahusiano ya kisiasa na kikazi miongoni mwa watu kadhaa maarufu serikalini, bungeni na katika sekta ya biashara.

Jambo ambalo lilianzia nje ya Bunge kabla ya kuingia katika taasisi hiyo nyeti ya kutunga sheria, sasa limebadili mwelekeo na kulifanya lichukue sura inayoweza kuwapaka matope wabunge kadhaa, wanasiasa wa kawaida, wafanyabiashara na kiongozi mmoja wa juu kabisa serikalini.

Kikubwa katika suala hili, ni kuingizwa kwa madai ya rushwa yanayowahusisha watu maarufu katika mwenendo wa mambo ya kisiasa, kijamii na kibiashara.

Suala hili ambalo kimsingi kiini chake bado hakijawekwa bayana, liliwekwa hadharani jana na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.

Ndesamburo, mbunge matata, ambaye wakati fulani kwenye Bunge lililopita aliadhibiwa kwa kutoa kauli ambazo alidaiwa kushindwa kuzithibitisha, jana alitoa matamshi mazito akiihusisha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, na tuhuma za rushwa.

Mbunge huyo pekee wa upinzani aliyerejea tena bungeni kwa mara ya pili mfululizo kwa upande wa Tanzania Bara, jana hiyo hiyo alitangaza uamuzi wake wa kujiuzulu ujumbe wa kamati hiyo, akikataa kuhusika na vitendo hivyo.

Ndesamburo, katika barua ya kujivua wadhifa huo aliyomwandikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, ametoa sababu mbili zilizomfanya afikie uamuzi huo.

Anaitaja sababu ya kwanza ya kujiuzulu ujumbe huo kuwa ni kutoridhishwa kwake na namna kamati hiyo ilivyoyashughulikia madai yanayoihusisha kamati kupokea rushwa katika kesi inayowahusisha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mbunge Malima.

Mengi alifungua kesi hiyo akilalamikia kauli iliyotolewa na Malima bungeni akivituhumu vyombo vya habari vinavyomilikiwa na mfanyabiashara huyo (Mengi), kutoa muda mfupi kwa masuala yanayohusu taifa wakati vikitumia muda mwingi kuelezea mambo yanayomhusu yeye mwenyewe.

Katika barua yake, Ndesamburo, mbaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini (CHADEMA), amemweleza Spika kuwa kumekuwapo na madai kwamba wabunge (akimaanisha wajumbe wa kamati hiyo) wamepewa rushwa na mfanyabiashara mwingine maarufu wa jijini Dar es Salaam (jina tunalihifadhi) ili kuacha kulifuatilia suala linalohusu kesi ya Mengi na Mbunge Malima.

Pili, katika barua hiyo ya Januari 10, mwaka huu, Ndesamburo anadai kuwepo kwa mazingira ya mhimili wa utawala kuingilia Bunge kitu ambacho ni kinyume cha utawala bora na mgawanyo wa madaraka.

“Dhamira yangu inanisukuma kuamini kwamba, mambo haya ni kikwazo cha ukweli na haki, hivyo sitawatendea haki Watanzania walionichagua kuwawakilisha bungeni kama nitaendelea kushiriki katika kamati husika,” alisema Ndesamburo.

Alipoulizwa na Tanzania Daima, Spika Sitta alikiri kupokea barua hiyo na kusema kwamba, uamuzi wa mwanasiasa huyo ni wa jazba.

“Why should I comment! (Kuna haja ya mimi kutoa maoni yangu!) Ana haki ya kufanya hivyo, lakini nilimshauri nikamwambia asichukue uamuzi wa haraka…unajua mwanasiasa haendi hivyo, huo ni uamuzi wa jazba,” alisema Spika Sitta.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Ndesamburo alibainisha kuwa, uamuzi wake wa kujiuzulu unatokana na kauli zenye utata zinazotolewa na kiongozi mmoja wa juu serikalini, akidai kuwa zina lengo la kumharibia maisha yake.

Alisema kuwa, wakati kesi ikiendelea, Mengi aliwahi kumwita na akamweleza kuwa aliitwa na kiongozi huyo wa juu serikalini na kutakiwa kuondoa kesi hiyo, kwani atashindwa, kwa kuwa mfanyabiashara mwingine ameihonga kamati hiyo ili yeye ashindwe.

“Halikuwa jambo dogo, nililifikisha kwenye kamati na wenzangu walishtushwa na hili, tukakubaliana tumwite … (Mengi), atuthibitishie hayo…tukahitimisha kikao cha kamati ile, tukaenda kwenye Krismasi,’’ alisema Ndesamburo.

Alisema, baada ya kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka mfanyabiashara huyo alimpigia simu na kumwambia kuwa ameelezwa na kigogo huyo wa serikali kuwa iwapo ataitwa na kamati hiyo kuhusiana na tuhuma hizo, ayakane maneno hayo.

“…(akimtaja Mengi) alinipigia akaniambia … (akimtaja kiongozi wa serikali) amemwambia ayaruke maneno yale…nilishangaa sana kwa kiongozi mkubwa wa nchi kutaka … (Mengi) aniruke! Inasikitisha…nikayapeleka maneno hayo kwenye kamati.

“Niliwaambia wenzangu nikaona si sahihi kuendelea na kesi hii ambayo rushwa ipo ndani yake na mimi nitashindwa kwa sababu dhamira itanisuta… nikaandika barua ya kujiuzulu,” alisema Ndesamburo.

“Nilishauriwa kulishughulikia jambo hili kwa mujibu wa taratibu za Bunge na ningefanya hivyo lingekuwa siri kali, hivyo wananchi wasingeweza kufahamu haya…kila siku tunasema tunataka utawala bora ni upi sasa? Lazima wananchi wafahamu mambo haya,” alisema.

Alisema kanuni na katiba zinampa haki ya kuzungumza, hivyo kuendelea kuwapo kwenye kamati hiyo na kushindwa kulizungumza jambo hilo ni sawa na kukiuka maadili.

Aidha, Ndesamburo alihoji uwepo wa uongozi bora kwenye utawala na kutaka kujua kinachofichwa na viongozi hao ni kitu gani na kwa nini kiongozi huyo na mfanyabiashara wasiwajibike kwa wananchi ili haki itendeke na wanaodaiwa kupewa rushwa wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Ndesamburo, alihoji kinachofichwa na kutaka wananchi wajulishwe mwenendo wa kesi hiyo, kwa vile hiyo ni sehemu ya utawala bora na kwamba yupo tayari kuhojiwa kwa chochote kuhusu kauli hizo.

Alihitimisha mazungumzo yake kwa kusema: “Leo (jana) asubuhi nimemkabidhi Spika wa Bunge barua ya kujiuzulu kwenye kamati ingawa ameniomba kutofanya hivyo…ni jambo zito linalozungumzwa na kiongozi mkubwa serikalini… ‘am over seventy’ nimevuka umri wa Biblia, siogopi kufa, ili mradi niseme kweli.”

Habari zaidi ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka vyanzo kadhaa vya habari zinaeleza kwamba, dhamira kubwa ya moja ya kundi linaloshiriki katika vita hiyo iliyoanza kufichuliwa na Ndesamburo ni kuona kwamba, kile kinachoonekana kuwa ni madhambi ya kiongozi mmoja wa juu serikalini yanaanikwa.

Jitihada za Tanzania Daima za kumpata Mengi na kiongozi huyo wa juu serikalini jana ziligonga mwamba katika kile kilichoonekana kuwa kila upande kutokuwa tayari kuweka bayana ukweli halisi wa jambo hili, japo kwa wakati huu.

Hata hivyo taarifa za uhakika ambazo gazeti hili lilikuwa limezipata, zilikuwa zikieleza kwamba, kila upande katika vita hii ulikuwa umejiandaa kukabiliana na upande mwingine.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.