RAIS Jakaya Kikwete, yuko katika hatua za mwisho za kukamilisha mabadiliko ya Baraza lake la Mawaziri, na wakati wowote kuanzia sasa anaweza kuyatangaza.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka vyanzo vya kuaminika serikalini, zinasema kwamba, Rais Kikwete ameshawasiliana na mawaziri wake wote watakaoguswa na uteuzi huo anaotarajia kuutangaza.
Kwa mujibu wa habari hizo, mabadiliko hayo yanaweza yakamhusisha pia mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale – Mwiru, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano ya Jamii).
Chanzo chetu cha habari kutoka serikalini kimelieleza gazeti hili kwamba, Kingunge ameamua kupumzika mwenyewe, baada ya kujiridhisha kuwa muda wa mwaka mmoja aliokaa na Rais Kikwete umeshamjengea kiongozi huyo uzoefu wa kutosha kuongoza serikali.
Habari zaidi zinasema kwamba, miongoni mwa mawaziri ambao wameguswa na mabadiliko hayo ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bernard Membe, ambaye huenda akapandishwa cheo na kuwa waziri kamili.
Membe, ofisa wa juu mstaafu serikalini akiwa amewahi kufanya kazi Idara ya Usalama wa Taifa, na katika balozi kadhaa nje ya nchi, anaweza akatangazwa kuwa ama Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Asha - Rose Migiro, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Kwa sababu hiyo basi, mabadiliko hayo yanaweza yakasababisha, Philip Marmo, ambaye sasa ndiye waziri mwenye dhamana ya utawala bora, akahamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu, kuchukua nafasi iliyoachwa waziri na marehemu, Juma Akukweti, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Inaelezwa kwamba, kutokana na kuanza kuwaelewa vizuri watendaji wake aliowafunda kwa semina elekezi kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Arumeru, nje kidogo ya Jiji la Arusha, matukio hayo yanayomlazimisha kufanya mabadiliko yamemuweka katika mazingira magumu.
Habari zinaeleza kwamba, kutokana na kuwa na nafasi tatu zinazopaswa kujazwa, Kikwete sasa atalazimika kuingiza sura mpya katika baraza lake la mawaziri.
Mbali ya kuziba nafasi, anakabiliwa pia na mtihani wa kujali uwiano wa kikanda au kimkoa, uzoefu wa nafasi hizo nyeti za Waziri wa Bunge, kadhalika anayefaa kwa masuala ya ushirikiano wa kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, Rais Kikwete, ama anatakiwa kumpandisha hadhi mmoja wa wabunge kutoka mikoa ya kusini hadi kwenye uwaziri, au anaweza kuteua mbunge na kisha kumpandisha hadhi.
Uzoefu wa Marmo katika masuala ya Bunge, akiwa amewahi kuwa Naibu Spika kwa muda mrefu na ule wa Membe, katika masuala ya kimataifa unawafanya wao kuwa na nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hizo, ingawa Rais ndiye mwamuzi wa mwisho.
Hata hivyo, kupanda kwa mawaziri hao kunafungua milango zaidi kwa mmoja wa wabunge wanawake kuwa na nafasi ya kuteuliwa kujaza moja ya nafasi zitakazobaki wazi, akichukua nafasi ya Migiro, japo kwa kuingia katika baraza hata kama si katika wizara ile ile.
Hadi sasa Rais Kikwete, kwa mamlaka aliyonayo ya kuteua wabunge kumi katika kila muhula wa uongozi, amebakiza nafasi tatu baada ya kuteua wabunge saba. Hata hivyo kuna uwezekano mdogo kwa Kikwete kuteua waziri kutoka nje ya wanasiasa ambao hivi sasa ni wabunge tayari.