Mabasi yanayosafirisha abiria Jijini almaarufu kama daladala yamekisusa kituo cha mabasi cha Makumbusho na kukiacha cheupee na tope lake utadhani kimetifuliwa na tinga tinga.
Kufuatia hali hiyo, daladala zililazimika kupita mitaani kusanya abiria.
Mwandishi wa habari hizi aliyefika kituoni hapo mapema leo amekuta kituo kikiwa kitupu bila abiria wala daladala.
Baadhi ya abiria waliozungumza na Alasiri wamesema kituo hicho kwa sasa hakifiki kutokana na kutapakaa matope kila sehemu na kufanya abiria ’walioulamba’ kula tope hadi magotini.
Mwandishi ameshuhudia baadhi ya daladala zikipita mitaani kukusanya abiria katika makazi ya watu na zingine zikilazimika kurejea katika kituo cha zamani cha Mwenge kusaka abiria.
John Martin mkazi wa Makumbusho amesema maamuzi ya uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kukihamishia kituo cha Mwenge katika eneo hilo kabla hakijakamilika ni ubabaishaji.
’’Kituo hiki ni cha kisasa na kimejengwa kwa gharama kubwa, lakini cha kushangaza kimefurika matope na hakifai tena’’ amesema Martini.
Baadhi ya abiria waliodamkia kituoni hapo walionekana wakihaha baada ya kukuta kituo ’kimeyeyuka’.
Hali hiyo ilizua tafrani baada ya abiria hao kukosa mwelekeo na wasijue wapate wapi usafiri wa kuwahi makazini mwao.
’’Jamani nimejitahidi kutembea kwa miguu mpaka huku halafu nakuta hakuna usafiri, sasa tukapandie wapi magari au tutembee mpaka Moroko’’, mama mmoja ambaye hakutaja jina lake alisikika akilalamika.
Kero hiyo ya tope hata hivyo imekuwa neema kwa wajanja wachache ambao wameibuka na mradi mpya wa kusafisha miguu ya watu iliyojaa tope kwa gharama ya shilingi 100 kwa kila anayehudumiwa