Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kibondo tusidhani Rais Kikwete ni Kipofu
Kibondo tusidhani Rais Kikwete ni Kipofu
By Prosper Kwigize | Published  01/10/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Miongoni mwa mambo ambayo ninayaogopa sana hapa nchini ni pamoja na kumdharau au kumuona kiongozi wa nchi hususani Rais kama mtu asiye na maana au asiyeona mbali au asiye na utaratibu wowote katika kuratibu masula ya uongozi na maendeleo, kabisa hili naliogopa.
 
Na miongoni mwa viongozi wa nchi ambao mara zote wako makini kila siku kuhakikisha nchi haiharibiki hata kama kuna mapungufu kwa mtazamo wa watu ni pamoja na Rais, yeye huwa makini kufuatilia kuwa mambo yote yanafuata utaratibu, nah ii ndo sababu mheshimiwa Kikwete aliwahi kusema katika nafasi yake ya Urais hana ubia na mtu.
 
Kila kiongozi aliyeko kokote nchini hufuatiliwa hatua kwa hatua kwa kujua ama bila kujua na katika taarifa mbalimbali mheshimiwa Rais atapata kujua yanayoendelea kote nchini kutokana na vyanzo mbalimbali vya habari. Kwa maana hii si rahisi mtu atoe hoja yoyote ya kumshawishi.
 
Hivi karibuni watu au mtu aliyejipachika jina na dhamana ya wananchi wote wa Kibondo (sina hakika kama kweli mawazo yake ni wananchi wa Kibondo, hata mimi sikujua hoja hii) na kama si utashi na mawazo ya wananchi basi mwandishi anapaswa kuomba radhi pia. Katika gazeti liitwalo MwanaHalisi la desemba 6 ukurasa wa 14, mtu aliyejiita Juma Maftaha aliandika Barua ya wazi kwa Rais akielezea kile kinachoonekana kama dharau kubwa kwa Rais au kumuona kana kwamba yeye ni kipofu na Kiziwi.
 
Katika barua hiyo ya wazi kwa mheshimiwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, ambayo imejizolea umaarufu sana kaba wilayani Kibondo ambayo wengi wa wanaoisoma huitaja kama unafiki na chuki binafsi baina ya mwandishi na mkuu wa wilaya ya Kibondo, jumla ya aya 20 ziliandikwa na mheshimiwa Maftaha aliyeamua kuwasemea wananchi bila kuwa na takwimu sahihi za wilaya.
 
Kana kwamba haitoshi gazeti la Kulikoni la tarehe 15-21 Desemba mwaka huu, watu wengine kama pia si mtu mmoja aliyeamua kupokonya utashi wa wengi kwa kuyaita mawazo yake kama mawazo ya wananchi aliandika barua kwa mhariri wa gazeti hilo akielezea yaleyale yalioandikwa na gazeti la Mwanahalisi kwa kichwa kisemacho ‘Rais Kikwete DC huyu hatufai’ingawa alipunguza idadi ya aya na kuacha aya 17 badala ya 20.
 
Kinachonifanya niseme au niamini kuwa hayakuwa mawazo ya wananchi wa kibondo ni kile kitendo cha baraua ya wazi kwa Rais mwandishi kujitambulisha na kishe katika barua ya maoni kwa mhariri ikatajwa kuwa ni wananchi wa wilaya ya Kibondo na wakati huo huo kil akitu kikifanana na barua ya awali, hakika hii ni dharau kwa Rais wetu kwamba yeye hajui yanayoendelea Kibondo.
 
Kwa msomaji makini na mjuzi wa kutafakari kile akisomacho utakubaliana nami kuwa kilichoandikwa katika barua ya wazi kwa Rais katika gazeti la MwnaHalisi na barua kwa mhariri iliyomlazimisha Rais aone kuwa DC hafai ni kilekile na mwandishi ni yuleyule na wala si mawazo ya wananchi wa Kibondo kama alivyodai mwandishi huyo, bali kwa haraka utabaini kuwa watu hao wawili wana visa binafsi na hivyo kutaka kuvuruga mawazo ya wananchi.
 
Ninaposema kuwa fikra za mwandishi wa barua hizo ni potofu sina maana ya kuanzisha malumbano naye wala kubeza mawazo yake hata kidogo, wala simaanishi kuanzisha malumbano katika haya bali msingi mkubwa katika hili ni kuhakikishi kuwa kwa dhana zetu binafsi tusipotoshe ukweli.
 
Ni haki ya kikatiba kila mtu kutoa maoni lakini katiba hiyohiyo inasema mtu ana haki ya kutoa fikra zake ili mradi asivunje sheria (kimsingi kupotosha jamii/umma ni kuvunja sheria), alichokifanya mwandishi Maftaha ni kuidhihirishia jamii kuwa ana chuki binafsi na mkuu wake wa wilaya na hivyo kuandika barua zisizowakirisha mawzo ya wanakibondo wote.
 
Kudhihirisha kuwa mwandishi wa kile ambacho kilipewa jina la makala na gazeti la mwanahalisi (kimsingi ile si makala maana hakuna takwimu zozote zilizoandikwa kudhirisha ukweli wa kilichosemwa na mwandishi Juma maftaha. Hebu sasa tupitie hatua kwa hatua barua hizi mbili zilizomo kwenye kulikoni na Mwanahalisi.
 
Kwanza nikumbushe kuwa zote hizo zinafanana, kutofautiana kwa aya tatu ni kutokana na uchapaji au jinsi ambavyo mhariri wa habari na makala alizipanga. Katika barua ya wazi kwa mheshimiwa Rais mwandishi Maftaha katika aya ya kwanza anataja kuwa ‘sisi wananchi wa wilaya ya Kibondo lakini mwisho anaweka jina lake kuthibitisha kuwa yale ni mawazi yake binafsi. Ukifananisha na aya hiyo katika gazeti la Kulikoni kilichopungua ni jina la mkuu wa wilaya tu mengine ni yale yale.
 
Ukisoma aya ya pili na ya tatu hakuna kilichobadilishwa ingawa aya ya nneya mwanahalisi alikwenda tofauti na kulikoni kwa kuweka kipengele cha chuki za DC kwa wanaokwenda kinyume naye, hata hivyo hakuweza kutaja ni nani alizidishiwa chuki na DC baada ya kupinga maongozi yake, sehemu nyingine zote ni sawa isipokuwa mpangilio tu.
 
Katika aya ya sita ya gazeti la mwanahalisi ambayo ni ya tano katika kulikoni mwandishi Juma anasema mkuu wa wilaya alipiga marufuku mafundi seremala ili yeye ajinufaishe, huu ni uongo kwani kilichozuiliwa na serikali wakati huo ilikuwa ni uvunaji horela wa misitu na wizara husika ilisitisha shughuli za uvunaji wa misitu hadi ilipotangazwa kinyume chake baadaye, ni kutokana  na hilo mafundi wengi Kibondo walikosa vitendewa kazi hususani mbao hasa kwa waliokuwa na mbao zisizo harali kwa mujibu wa sheria ya uvunaji wa maliasili.
 
Aidha katika aya hiyohiyo mwandishi anayataja magari ya shirika linalohudumia wakimbizi na masuala ya maendeleo wilayani la Tanganyika Christian Refugee service (TCRS) kuwa linatoa magari yake kusafirisha mbao za mkuu wa wilaya, lakini hakuna mahala alipotaja namba za gari husika, siku ya kusafirisha mbao wala wapi mbao hizo hupelekwa.
 
Katika aya ya saba ya mwanahalisi ambayo ni aya ya sita ya Kulikoni mwandishi anataja kuwa DC wake ameihujumu miradi ya TASAF kwa manufaa yake na kusababisha gharama za miradi hiyo kuwa kubwa, huu pia ni uzushi na uchochezi kwa wananchi na dharau kubwa kwa wananchi waliohusika katika kufanikisha miradi ya TASAF.
 
Wilaya ya Kibondo ni miongoni mwa wilaya chache sana kati ya zilizokuwa na ufadhili wa TASAF awamu ya kwanza zilizofanya vizuri, kama mwandishi Juma Maftaha ni raia makini atakumbuka kuwa serikali ya awamu ya tatu kupitia kwa Rais mstaafu Benjamin William Mkapa ilitoa cheti cha ubora wa miradi na utendaji mzuri wa wilaya ya Kibondo katika mpango wa mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF, cheti hicho alikabidhiwa mkuu wa wilaya ya Kibondo Luteni Kanal John Mzurikwao katika sherehe kubwa za TASAF Kitaifa zilizofanyika wilayani Magu mkoani Mwanza mwaka juzi , mbele ya Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa.
 
Mwandishi Juma maftaha katika gazeti la Mwanahalisi desemba 6, desemba 2006 ndani ya aya ya 10 aliandika maneno ambayo pia yamo katika gazeti la Kulikoni toleo la tarehe 15-12 desemba 2006 yanapatikana katika aya ya 9 yakisema kuwa wakati wa minada DC hulazimisha mambo ili ajinufaishe! Hapa pia hapakutajwa takwimu zozote kuthibitisha ni lini na wapi na katika mnada gani ambapo DC alishinikiza kupendelewa.
 
Katika aya ya kumi ya Kulikoni na aya ya kumi na moja ya mwanahalisi mwandishi Juma maftaha anazungumzia Uwanja wa Mpira wa miguu wa mji mdogo wa Mabamba wilayani Kibondo kwamba DC aliagiza uwanja huo upandwe miti kitu ambacho pia ni uzushi, uwanja huo nimeutembelea hivi karibuni na haujapandwa miti kama anavyosema na wapenzi wa soka wanautumia kwa ajili ya mazoezi ya viungo na soka.
 
Uwanja wa Mabamba uliopo jirani kabisa na Msikiti, ulikarabatiwa na mmoja wa wapenzi wakubwa wa soka ambaye amekuwa akisaidia sana chama cha mpira wa mgiguu wilaya ya Kibondo KDFA kifedha ili kuendeleza soka ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu wilayani Kibondo Bw. Jamal Abdallah Tamim. Bw. Jamal alifanya hivyo ili vijana wapate mahala pa kuchezea soka na kukuza vipaji vyao, itakumbukwa kuwa Mji wa Mabamba umewahi kuwa na moja ya timu kubwa na machachari ya AMAVUBHI FC ilikuwa tishio kwa timu nyingine wilayani humo.
 
Katika ulimwengu wa uwazi na ukweli kama alivyotaja katika aya ya mwisho ya barua yake kwa Rais katika gazeti la manahalisi desemba 6, kuna mahali mwandishi alipaswa atoe takwimu au hali halisi juu ya kile anachokitoa kwa Rais Kikwete ili aepuke lawama ya kumdharau au kumuona kuwa ni Kipofu na haoni yanayoendelea Kibondo wakati yeye ndiye Rais wa jamhuri ta muungano wa Tanzania.
 
Katika aya ya 15 -16 ya gazeti la Kulikoni, ambazo ni aya za 18 na 19 za Mwanahalisi, mwandishi Juma Maftaha anaelezea kuwa wakuu wa wilaya waliotangulia wilayani Kibondo ambao aliwataja kuwa ni Shashu Rugeye na John Masaga, kwamba walifanya mambo makubwa sana kuiendeleza wilaya ya Kibondo kuliko anavyofanya mkuu wa wilaya wa sasa John Mzurikwao.
 
Akitaja moja ya vigezo Maftaha anasema kuwa « nanukuu ‘kwa mfano alikuwepo Shashu Rugeye alifanya kazi vizuri kabisa na baadae akafuatia John Masiaga (alikosea jina ni MASAGA) nae alifanya kazi vizuri na akajenga madarasa mengi na kwa keli maendeleo yalikuwa yanaonekana’ mwisho wa kuinukuu aya hiyo.
 
Ukweli ni huu ; tukizungumzia kipengele ambacho anakitaja yaani ujenzi wa madarasa, wilaya ya Kibondo tangu uhuru hadi mwaka 2002 ilikuwa imefanikiwa kuwa na shule za sekondari tano tu (kwa miaka 41 shule 5) huku shule za msingi zikikadiriwa kufikia 70 ambazo hata hivyo zilikuwa kero sana kwa kutokidhi mahitaji ya wana Kibondo.
 
Tangu mwaka 2002 baada ya kufika kwa Mzurikwao kupokea kijiti cha Masaga (si DC tena, alitemwa na serikali ya awamu ya nne) anayetajwa kufanya mambo makubwa ya ujenzi wa madarasa na kuifanya wilaya kuwa na shule tano tu huku kati ya hizo za serikali zikiwa 4, sasa wilaya ya Kibondo chini ya huyo DC anayegombezwa na Juma Maftaha ina jumla ya shule 24 katika kipindi cha miaka minne ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 200%.
 
Katika kipindi hicho cha serikali za awamu ya kwanza ya marehemu Baba wa Taifa wilaya ya Kibondo hadi kustaafu kwa Mwalimu JK Nyerere haikuwa na shule ya sekondari hata moja, hadi pale ilipojengwa shule ya sekondari ya wasichana Kibondo chini ya serikali ya awamu ya pili miaka ya 1985-1988, shule ya sekondari ya wasichana Kibondo inaongoza katika matokeo ya kidato cha sita kila mwaka kwa shule za kanda ya Mangharibi.
 
Kati ya mwaka 1990 na mwaka 2000 wilaya ilikuwa na mikakati mikubwa sana ya kuinua kiwango cha elimu sambamba na ujenzi wa shule za sekondari ambapo shule ya sekondari ya Maragalasi iliyoko Kibondo mjini,shule ya sekondari Kumgogo iliyoko tarafa ya Mabamba pamoja na shule ya sekondari ya Kakondo iliyoko tarafa ya mabamba zilianza kujengwa chini ya mpango wa maendeleo ya elimu wilayani uliopewa jina la Kiha la MWANSEKUKI lenye tafsiri ya KWANINI UNAKATAA huu ulikuwa ni mpango wa kukusanya michango kutoka kwa wananchina watumishi ili kufanikisha ujenzi huo, mpango huo haukupata mafanikio.
 
Baadaya ya kukwama kwa MWANSEKUKI bodi ya elimu ya wilaya iliunda mkakati wa kushirikisha wadau wengi zaidi na kutafuta zaidi wafadhili na hivyo kuamua kubadilisha jina la MWANSEKUKI na kuuita mkakati huo kwa jina la kizungu ambalo lililenga zaidi utegemezi kuliko kuchangisha raia waliokuwa tayari wamechoka bila mafanikio.
 
Ilianzishwa asasi ya kiserikali iliyoitwa Kibondo District Education Trust (KIBODET) ambao licha ya kuwa na lengo mbadala wananchi nao waliendelea kutobolewa mifuko yao kwa ajili ya sekondari. Hata hivyo KIBODET nayo iliishia midomoni mwa wachache na sekondari hizo za KUMGOGO, KAKONKO na MARAGALASI hazikujengwa, hadi kipindi alichokuwepo mkuu huyo anayedaiwa kutofaa ambaye alitumia nguvu na ushawishi mkubwa kukamilisha ujenzi huo bila kukusanya michango mingi toka kwa wananchi kama awali.
 
Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mika arobaini ya mitano ya uhuru wa Tanganyika mkuu wa mkoa wa Kigoma Kanal Joseph Simbakalia akiambatana na viongozi mbalimbali wa ngazi ya mkoa, mwakilishi wa shirika la Mpango wa maendeleo duniani UNDP Bibi Rudovica Tarimo pamoja na viongozi wengine  wa wilaya alifanya kile ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya Uhuru wilayani Kibondo, achilia mbali wakati wa Nyerere.
 
Kwanza kanali Simbakalia aliweka mawe ya msingi katika jumla ya shule mpya za kata 9 pamoja na kushiriki ujenzi wa baadhi ya shule hizo zinazotarajiwa kufunguliwa mwakani, vyombo vingi vya habari vililipoti kuwa mkuu huyo wa mkoa aliitaja wilaya ya Kibondo kuwa wilaya ya kwnza kwa ujenzi wa shule za sekondari katika mkoa wa Kigoma, iweje leo mtu unabeza mafanikio haya?
 
Kwa upande wa shule za msingi toka kati ya shule 70 mwaka 2002 sasa wilaya ya Kibondo ina takribani shule za msingi 110 na katika aadhi ya vijiji kuna shule zaidi ya moja, ingawa bado lipo hitaji la kujengwa kwa shule nyingine zaidi kutokana na ongezeko la watu ambalo lilithibitishwa na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 iliyobaini mkoa wa kigoma kuwa na ongezeko kubwa la watu.
 
Unaweza ukapingana nami kuwa labda namtetea mkuu wa wilaya anayepingwa na watu kupitia kwa Juma Maftaha, ukweli ni kwamba kama mwandishi wa habari ninawajibu wa kuhakikisha naihabarisha jamii kwa mambo ya ukweli bila kuathiri taaluma yangu na kamwe sitakuwa tayari kuona na kuchekelea wananchi wanapopotoshwa na wachache kwa maslahi binafsi.
 
Katika hili ninaweza kusema kwa uchambuzi huu wa kina kutoka katika aya za mwandishi Juma Maftaha na katika kutoa takwimu za wapi Kibondo ilikuwa na sasa iko wapi naamini utakubaliana nami kuwa kweli mkazi huyu wa Kibondo anataka kumwona mheshimiwa Kikwete, Rais wetu kuwa ni Kipofu na haoni vema yanayoendelea nchini.
 
Kamwe nasisitiza kuwa sikusudii kusuluhisha chochote kama DC ana Mgogoro wowote na Bw. Juma Maftaha, kama wana ugomvi baina yao ni vema wamrudie muumba wao atawasamehe kuliko kuwaingiza raia wote wa wilaya ya Kibondo katika balaa hili la kutoona mazuri ya serikali, Nia yangu ni kuhakikisha pale palipo na ukweli basi jamii ijivunie na asiwepo hata mmoja anayebeza shughuli za wananchi.
 
Kuandika barua kwa Rais bila kuzingatia ukweli na hali halisi ni kumuona Rais wetu kama Kipofu na kwamba kwa njia ya maandishi yetu tutaweza kushawishi tutakavyo kutoka kwa Rais wetu ambaye wakati akiapa kuongoza taifa hili aliahidi kuongoza kwa misingi ya katiba, sheria na utawala bora, aidha aliwahi kusema katika moja ya hotuba zake kuwa katika nafasi yake ya urais hana ubia na mtu. Labda juma Maftaha wewe uliahidiwa kuwa na ubia na Rais hadi umethubutu kumshirikisha upuuzi kwa madai kuwa ni ya wananchi wa Kibondo?
 
Si uungwana kabisa kugeuza masuala ya maendeleo kuwa sehemu za midahalo ya kipuuzi wala kutafutia ubwana, umwinyi na utwana huku ulisababisha wilaya ya Kibondo ionekane ya majungu na haikaliki au haitawaliki. Wakati wa uchaguzi mkuu kwenye baadhi ya mikutano kuna watu wengi walisikika wakisema ‘twavyutse’ wakiwa na maana kuwa wananchi wa Kibondo si wale wa zamani wakulazimishwa kuchukua dhabau na kukimbilia goroli, wameamka sasa wako macho, hivyo hawkotayari kutumiwa kama vyambo kwa migogoro ya watu tu.
 
Tabia na misemo ya watani wa waha eti Waha hawna shukurani zimepitwa na wakati sasa ni wajibu wa watu wote kushukuru kwa chema kinachokuwa kimefanyika kuliko kuona kila kitu ni upuuzi.
 
Namalizia hapa kwa kusema wananchi wa Kibondo tusidhani Rais wetu ni Kipofu anaona na anajua kila jambo, lakini pia hana ubia na mtu katika nafasi ya urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania .
 
 
TEL. 0754 077478, 0784 676888

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.