Na Joyce Joliga, Tunduru
SAFARI ya mwisho ya marehemu Juma Jamaldini Akukweti ilihitimishwa jana baada ya mwili wake kuzikwa jana mchana nyumbani kwao Tunduru mkoani Ruvuma.
Marehemu Akukweti (59) ambaye hadi mauti inamkuta akiwa kitandani nchini Afrika Kusini, akipata matibabu katika Hospitali ya MillPark, alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), alizikwa na mamia ya watu kutoka nje na ndani ya Mkoa wa Ruvuma, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Marehemu alizikwa jana saa 6.00 mchana nyumbani kwake katika Kijiji cha Makoteni kilichopo katika Kata ya Ligoma, wilayani Tunduru.
Mazishi hayo ambayo yalihudhuriwa na mamia ya watu, wakiwamo karibu viongozi wote wa juu wa serikali, yaligubikwa na vilio na nyuso za simanzi kutoka kwa waombolezaji.
Baadhi ya viongozi wengine wa juu wa serikali waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Spika wa Bunge, Samwel Sitta, mawaziri, naibu mawaziri, viongozi dini na wabunge wote wa Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya shughuli za mazishi, Rais Kikwete alisema serikali itasaidia kutekeleza miradi yote iliyoahidiwa na marehemu wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2005.
Alisema miradi ambayo itatekelezwa kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tunduru ni pamoja na ujenzi wa barabara, shule na kuwatafuatia soko la uhakika wakulima wa korosho.
Alimwelezea marehemu Akukweti kuwa alikuwa mchapakazi, muungwana, mpole, mwenye upendo na muadilifu na kwamba atakumbwa daima.
"Tutamkumbuka marehemu kwa upendo, uadilifu, upole , uchapakazi enzi za uhai wake," alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia aliahidi kuisaidia familia ya marehemu kwa kadri ya uwezo wake pale ambapo watakuwa na matatizo.
Naye mwakilishi wa familia ya marehemu, Abbas Ngajini, alishukuru serikali kwa msaada wake mkubwa iliouonyesha wakati wa kumuuguza marehemu lakini akasema Mungu alimpenda zaidi na kuamua kumchukua. Marehemu ameacha wake wawili na watoto tisa.
Katika mazishi hayo, Wizara ya tawala za Mikoa na Serikali za mitaa ilitoa ubani wa Sh milioni moja kwa familia ya marehemu. Wengine waliotoa mchango wa rambi rambi kwa familia ni Mkoa wa Ruvuma ulitoa Sh milioni moja, wabunge wa Mkoa wa Ruvuma Sh700,000, Mkoa wa Mbeya Sh milioni moja, wabunge wa Mkoa wa Mtwara Sh500,000 na wananchi waliofika walichangia Sh2,330,000.
Baadhi ya wananchi waloihudhuria mazishi hayo waliiambia Mwananchi kuwa Wilaya Tunduru imepoteza kiongozi shupavu ambaye alikuwa amejitolea kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Akukweti alifariki Alhamisi saa 8.30 usiku katika Hospitali ya Mill Park mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu zaidi Desemba 21, mwaka jana.
Waziri Akukweti alikuwa ni miongoni mwa majeruhi wa ajali ya ndege aina ya Cessna namba 5HTZ, mali ya Kampuni ya Tanzanair iliyotokea Desemba 16 mwaka jana, mjini Mbeya.
Katika ajali hiyo, Mwandishi na Mpiga Picha Mwandamizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Theresia Nyantori, alifariki papo hapo na wengine kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, lakini jioni yake walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Majeruhi wawili kati ya watano waliohamishiwa Muhimbili, Mratibu wa Mpango wa Uendelezaji Masoko ya Mazao ya Kilimo (AMSDP), Nathaniel Katinila na Afisa Habari Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, George Bendera, walifariki wakati wakiendelea kupata matibabu Muhimbili.
Rubani wa ndege hiyo, Martin Sumari, amekwisha kutibiwa na kuruhusiwa kutoka Muhimbili, lakini amelazwa katika Hospitali Kuu ya jeshi ya Lugalo, huku Msaidizi wa Waziri, Aniceth Kanje, akiendelea kupata matibabu.