Na. Prosper Kwigize (0754 077478)
Tabora
Timu ya mpira wa wavu ya mkoa wa Tabora ilishindwa kabisa kuonesha makucha yake kwa timu ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma baada ya kufungwa jumla ya seti tatu kwa sifuri katika mpambano wa kirafiki kati ya mkoa wa Kigoma na Tabora.
Kipute hicho cha aina yake na cha nguvu kilichezwa jumamosi iliyopita katika uwanja wa muungano mesi unaomilikiwa na jeshi la ulinzi wa Tanzania JWTZ mjini Tabora baada ya timu ya Tabora kutoa mwaliko kwa timu ya kibondo.
Ikiwa chini ya nahodha wake mahili Bw. Isaya Nzuguru Kibondo Volleyball Club- KVC inayoundwa na vichana wadogo chini ya miaka 23 ambao pia hucheza soka katika moja ya vilabu vya wilaya ya Kibondo, waliongoza mwanzo hadi mwisho wa mpambano huo dhidi ya Tabora.
Wakicheza mbele ya kaimu mkuu wa mkoa wa Tabora Bw. Moshi Mussa Chang’a ambaye ni mkuu wa wilaya ya Tabora, vijana wa timu ya Tabora walijikuta wakiambulia nusu ya point katika kila mchezo kwa kushindwa na wababe wao waliopata point 25 kila mzunguko.
Katika mzunguko wa kwanza (round) timu ya Kibondo ilishinda kwa jumla ya point 25 dhidi ya 19 za Tabora na mzunguko wa pili tabora ilizidiwa zaidi kwa kufungwa jumala ya point 25 kwa 16.
Mzunguko wa mwisho ambao ndio uliowapa ushindi Kibondo uliwaacha hoi zaidi wenyeji wao baada ya kujikuta wakiambulia point 11 kwa 25 na hivyo mwamzi wa mpambano huo Bw. Herbert Ntibakazi kuitangaza Kibondo kama mshindi wa mpambano huo kwa seti 3-0.
Aibu hiyo kwa wenyeji Tabora ilishuhudiwa pia na meya wa Manispaa ya Tabora mheshimiwa Peter Lembeli na mkuu wa brigedi ya jeshi kanda ya Tabora Luteni kanali Methew Sukambi ambao walionesha wazi kufurahishwa na vijana wa Kibondo kichezo.
Akitoa mawaidha baada ya mchezo huo kaimu mkuu wa mkoa wa Tabora Bw. Chang’a amewapongeza sana Kibondo kwa kuonesha kwamba walikuwa na maandalizi pamoja na mshikamao miongoni mwao na katika mchezo pia.
Aidha ametoa wito kwa mkoa wa Tabora kuanza mara moja mazoezi ya michezo mbali mbali ili kuondoa aibu ambayo imekuwa ikiukuta mkoa kimichezo hasa wanapopambana na mkoa wa Kigoma .
Mkoa wa Kigoma umekuwa ukiwashinda majirani zao wa Tabora katika michezo mbalimbali na katika kombe la Taifa Kigoma iliuondoa mkoa wa Tabora katika mechi zote mbili kwa ushindi wa 2-1 na 2-0