Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Bomoa Bomoa : Na nyie mbomolewe tupate watendaji safi.
http://www.habaritanzania.com/articles/2502/1/Bomoa-Bomoa-:-Na-nyie-mbomolewe-tupate-watendaji-safi.
By Elly Mgumba
Published on 01/5/2007
 
Wasiokumbwa na bomoa bomoa bado wanaamini kuwa zoezi hili lina lengo la kuweka majiji safi.Bila hofu wala mashaka wanaendelea kutoa hoja za kukejeli na kuwashangaa aidha wafanya biashara ama wenye nyumba walojenga sehemu zilizobomolewa.

Na HabariTanzania.com

Wasiokumbwa na bomoa bomoa bado wanaamini kuwa zoezi hili lina lengo la kuweka majiji safi.Bila hofu wala mashaka wanaendelea kutoa hoja za kukejeli na kuwashangaa aidha wafanya biashara ama wenye nyumba walojenga sehemu zilizobomolewa.Heri hata hawa ‘wasiokumbwa na bomoa bomoa’ kuliko hao mabwana bomoa bomoa wenyewe.

Wao ndo kabisa wakati sisi watanzania walalahoi tunaandika maumivu na mwaka wa mkosi wao ripoti zao zinapaa na kung’aa wakionekana viara na makamanda wa operesheni hii isiyo na macho.

Wengine watapandishwa vyeo licha ya elimu zao duni na fikra finyu katika upangaji na utekelezaji.Wengine wanajitokeza mbele ya vyombo vya habari na kujitapa kwamba ‘na bado’ zoezi litaendelea.

Nasema hivi hawa wote ni wale ambao hawajaionja joto ya bomoa bomoa na wala hawana utu wa kujaribu kufikiria adha wanayoipata wazalendo wenzao.

Binafsi naona neno lenyewe bomoa bomoahalina tofauti sana na butua butua ambayo kwa waliocheza ama wanaofahamu soka (kabumbu) watakubaliana nami kuwa ni mchezo usiovutia wala kuwa na
ufundi bali bora liende.

Je na watendaji wetu wanaoshabikia bomoa bomoa pasipo mipango sio wachezaji wanao butua butua??Binadamu anaweza kwenda likizo ya mambo yote lakini si likizo ya kufikiri,kwa kuwa asiyefikiri huyo hayuko hai.

Watekelezaji wa bomoa bomoa wameenda likizo ya kufikiri kwa kuamua kuutekeleza mpango huu kuanzia mwisho kuelekea mwanzo badala ya kinyume chake.

Watendaji wetu wameenda likizo ya kufikiri kwa kubutua butua bila kujali utu na uzalendo ama kujikumbusha kuwa wao haswa ndo chanzo cha huu wanaouita uchafu.

Usiniambie kuhusu mikakati endelevu,semina elekezi,mipango shirikishi na hadithi kedekede kwa kuwa zote nazifahamu na kwangu mimi na walalahoi waliowengi tunajionea kama ulimbukeni wa matumizi ya lugha.Wengi hatuvutiwi na uzuri wa kasha la kanda ya kaseti bali uzuri wa nyimbo zilizomo ndani yake.

Nakiri kuwa mazingira ya miji yetu kwa sasa ni safi ukilinganisha na kipindi cha nyuma.Ila nasikitishwa na ukweli kwamba ili kufikia hapa tulipo kuna wenzangu na mimi imetubidi kuwatoa kafara na hadi sasa aidha wanalala nje ama maisha yao ni ya kubahatisha mara baada ya nyumba ama biashara zao kubutuliwa.

Wakati tunayazungumza haya makomandoo hawa wanaingia mtaani leo hii tena kwenda kuendeleza butuaji huu kwa baraka za walio juu yao. Katika tafrija za kujipongeza wanaitwa majina mbali mbali ya kutukuka lakini hapa hapa tujiulize je walikuwepo wapi hawa watukuka wakati huu uchafu unajilundika??

Kwani sio wao waliotoa vibali na baraka za watu kujenga na kuwekeza katika maeneo ambayo wanajua dhahiri kuwa hayapaswi kujengwa?? Ni hulka ya kila mwanadamu kutaka kuona mabo yananyooka na yanakwenda kadiri yalivyopangwa.

Vivyo hivyo kila mtu anapokuwa na nia yake na anapoona ipo namna ya kuitimiza hana budi kufanya kila awezalo kuweza kutimiza kiu yake ya mafanikio.

Ninachojaribu kusema hapa nikwamba mimi Mtukwao ninapopata kiwanja ndoto yangu ni kujenga,mara baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria naanza zoezi la kujenga kibanda changu nijisitiri na wanangu.

Toka nachimba msingi hadi napaua serikali ipo na inaniona na siambiwi wala kuona alama kuwa eneo lile ni la wazi.Leo hii baada ya muda mrefu unanijia na ramani ya jiji eti nimejenga eneo la wazi nikueleweje??

Hii ramani ni mpya??kama si mpya nailikuwepo siku nyingi kwa nini isitumike mwanzoni kabla hata sijajenga kibanda changu??Lazima tukubaliane hapa jamani kuwa tatizo halipo kwa mjengaji bali kwa mtendaji ambaye huenda aidha hakutimiza wajibu wake ama alipendekeza njia mbadala na mambo yakanyooka na hatimaye Mtukwao kujenga kibanda chake eneo la wazi.

Adhabu ya mtoaji na mpokeaji rushwa ni moja sasa kama mjengaji alitoa rushwa ili ajenge eneo la wazi ama aweke biashara eneo la wazi matokeo yake ni bomoa bomoa basi zoezi hili lisisahau kuwabomoa waliopelekea kuwaingiza wenzao katika bomoabomoa.

Ndo maana nikasema Bomoa bomoa: Na nyie mbomolewe tupate watendaji safi.

Binafsi naamini mpango huu wa kusafihsa majiji mbali ya kuwa ni wa lazima lakini ulizingatia utu na kutambua makosa yalifanywa na serikali awali hadi kuruhusu watu kujenga ama kuwekeza biashara zao maeneo ambayo si sahihi.

Hili naling’amua pindi viongozi wa ngazi mabalimbali za manispaa wanapohojiwa nakulaumiwa kwa bomoa bomoa ambapo wanasisitiza kuwa upo mpango wa kuwasaidia wahanga.

Ninachoshindwa kuelewa mpango huu utanifaa nini hivi sasa wakati tayari nimeshalala nje na kudhalilika pasipo kifani??Kwa nini usingetangulia mpango huu kabla ya bomoa bomoa??

Nikifika hapa ndio maana nashawishika kuamini kuwa watendaji wako likizo ya kufikiri,wanatekeza mpango kisengere nyuma na wanastahili na wao kupata bomoa bomoa ili tupate watendaji safi.

Utajisikia vipi wewe leo hii ni siku y tatu toka kuvunjiwa nyuma au duka lako halafu afisa wa mtaa anapohojiwa anajibu kuwa hamkwenda kumlalamikia shida zenu?? Kumbe basi watendaji wote wamejiandaa kupokea matatizo ya wananchi na sio kuleta maendelea kwa kubuni na kutekeleza mikakati ya kimaendeleo.

Ina maana watendaji hawa wanachongojea wao ni kulalamikiwa ndipo wachukue hatua,lakini hata kuvunjwa kwa nyumba zaidi ya moja na kuwa na kaya kadhaa zinazolala nje unahitaji kengele ili uweze kuwasaidia??

Kama bomoa bomoa lengo lake kusafisha kile ambacho kipo sehemu ambako hakikupaswa kiwepo basi hata hawa watendaji ambao kimsingi hawawezi kazi nao wakumbwe na bomoa bomoa.Inakera zaidi unapokumbuka kuwa ni warasimu hawa hawa waliohusika katika suala zima la manunuzi ya eneo hili ulilovunjiwa na sasa wanakujia juu na kukubomolea.

Tunakumbushana tu jamani kwamba jamii mbali mabli zinazosemekana kuwa makatili duniani hazikuzaliwa bali zilitengenezwa.ni mkusanyiko wa machungu nakuonewa ndiyo yanayopelekea kuwepo kwa jamii hizi za ukatili na visasi visivyokuwa na mwisho.

Watawala msijisahau kwa upole wa Watanzania kwa kuwa kulowa kwa simba hakumgeuzi kuwa paka,simba ni simba na ataendela kuwa samba tu.

Tunapoendelea kubomoa kwa minajili ya kuweka miji katika hali ya usafi huku tukidai kuwa tunafuata ramani za majiji yetu tusisahau chochote,tubomoe kila kitu. Kama kweli miji yetu ina ramani basi tusiishie kuwabomolea akina Mtukwao peke yake bali tuwaendee na wenye viwanda walikoingilia maeneo ya makazi.

Usafi hautangamani na mazingira kwa kuwa hakutakuwa na maana ya kuwa ndani ya jiji safi kimandhari hali ya kuwa harufu ya ajabu ya kemikali,kelele za mashine nzito na adha lukuki zikiendela kuwakera walau wachache watakaobahatika kubakia katika maeneo ya makazi.

Zoezi hili lisiishie hapa bali liendelee kuchimba na kutafuta kulikoni na kwa jinsi gani muhusika alipata kibali kujenga kiwanda katika eneo la makazi ahali ya kuwa ramani ya jiji inasemekana ipo.

Bomoa bomoa imkumbe na kumbomoa yeyote aliyehusika kuidhinisha mauaji ya halaiki kwa kuruhusu kiwanda kujengwa eneo la makazi kwa kuwa siamini kama muhusika alijiamulia tu kujenga pasipo baraka za manispaa husika.

Hapa tena nilishangazwa kuona katika moja ya mahojiano mhusika wa manispaa akiwashangaa wakazi kwa kutokutoa taarifa ya ujenzi wa kitu fulani katika maeneo yao,anaendelea kuwalaumu watanzania kwa kutojijali.

Nikapata swali je ni mimi Mtukwao ninayepaswa kuhoji?? ramani ya jiji naijulia wapi mimi???Wengi wa wanaojenga ama kuwekeza biashara nzito katika maeneo ambayo si sahihi huwa na wao kwa namna moja wanakuwa wamelenga katika kutimiza ndoto zao hivyo wanatafuta namna yoyote ile kuweza kupata vibali,kwa mantiki hii ni lazm,a kuna mtu amabaye si msafi ndani ya watekelezaji wetu na kwa kuwa tunabomoa bomoa uchafu basi tusimsahau nay eye ambaye kwa uchafu wake ametusababishia sisi bomoa bomoa.

Haiwezekani leo hii ufurahie kuwekea nyumba yangu mimi Mtukwao alama ya X wakati nakisikia kiwanda Fulani jirani yangu ama baa Fulani mtaa wa pili ikiendelea kuporomosha muziki eti kwa kuwa wametishia kukupeka kortini.Kama kweli uko safi katika utekelezaji wako tokea mwanzo hadi mwisho unaogopa nini sasa??

Sishabikii ushindi wa baadhi ya wenye ‘nguvu’ dhidi ya bomoa bomoa bali nikiangalia kwa jicho la tatu naona ufa ambao huenda ukapelekea baada ya miaka michache ijayo tukawa na bomoa bomoa nyingine katika maeneo yaleyale kwa kuwa bila kuwabomoa watendaji waliopo basi maeneo haya yatajengwa tena wao wakiwa wawezeshaji wakuu.

Suala la uwajibishaji wa viongozi sio la msimu wala la mzaha mzaha inapaswa tuwe na utamaduni wa kufanya hivyo popote inapobidi. Kushindwa kufanya hivyo kunatutia mashaka sisi tuliobomolewa hali ya kuwa haikuwa makosa yetu ama kwa kuwa hatujui ramani ama kwa kuwa tulihakikishiwa na hao wahishmiwa.

Tunapata mashaka na uongozi mzima chini mpaka juu kuwa huenda na wenyewe umekwenda likizo ya kufikiri.Badala ya kushabikia ripoti zinazosema nimebomoa nyumba kadhaa tuwe na uwezo wa kusema tumezuia nyumba kadha zisijengwe katika maeneo ya wazi ama ya barabara.

Mikakati ya ubomoaji iendane na uwajibishwaji wa waliotia baraka za aidha ujenzi ama uwekezaji katika maeneno zilikopangwa kupita barabara ama ameneo ya wazi.

Serikali pia itambue kuwa uzuri wa mikakati sio urembo katika maandishi na makabrasha kede makabatini bali matokeo katika utekelezaji.Hata kama lengo la bomoa bomoa ni zuri kiasi gani mimi sitaweza kuliona tena iwapo nmeshaonja siku kadhaa kulala nje ama kushinda njaa hali ya kuwa ilikuwepo jinsi ya kufanya maandalizi kabla ya kutekeleza butua butua hii.

Kama tumeshindwa kuleta maisaha bora kwa kila mtanzania basi walu tulete usawa kwa kila mtanzania kwa kufanya bomboa bomoa yenye usawa kuanzia mjenzi hadi aliyesinzia na kuachia ujenzi ukatokea.Usawa pia ulenge kuanzia ‘asiye nacho’ hadi ‘mwenye nancho’ ili hatimaye tuweze kusema usawa kwa kila Mtanzania unawezekana.

Poleni ndugu zangu mlikumbwa na bomoa bomoa na haswa kukerwa na majibu ya nyodo yanayotolewa na waliopaswa kutoa msaada wakidai eti ianbidi tukairipoti hiyo ishu ofisini kwao.Waswahili husema “Uzuri ndio kipimo cha ubaya”.Bomoa bomoa inyooshe mikono kuwafikia watekelezaji waliohusika kuruhusu ujenzi holela.