Yanga ya Dar es Salaam ambayo ni moja ya timu tatu za Bara na yenye jukumu la kwanza kubakisha nyumbani Kombe la Kagame la klabu bingwa ya soka ya Afrika Mashariki na Kati kutokana na kuwa mshindi wa ligi kuu ya Bara mwaka jana, jana ilianza kwa kwa wasiwasi michuano hiyo na kuambulia sare ya 0-0 mbele ya St. George ya Ethiopia.
Na kikwazo kikubwa kilikuwa mlinda mlango Dennis Onyango aliyekuwa asajiliwe na Yanga mwaka jana akitokea SC Villa ya Uganda ambaye alizuia mashuti mengi ya washabuliaji wa mabingwa wa Bara kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Yanga, hatahivyo, itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutumia vizuri angalau nafasi moja kwani washambuliaji Thomas Maurice, Gaudence Mwaikimba, Said Maulid, John Barasa na Gulla Joshua aliyeingia kipindi cha pili walishindwa kufunga pamoja na kubaki na Onyango tu katika lango la St. George.
Kitu pekee ambacho Yanga inaweza kujivunia, kama ushindi kwenye soka ungekuwa unapatikana na kujikusanyia pointi kama ngumi, ni ukweli kuwa mashuti mawili ya washambuliaji wake yalimmuumiza Onyango aliyelazimika kukaa chini na kutibiwa, yaliyopigwa na Gulla aliyepata pasi ya Amri Kiemba katika dakika ya 67 na Maurice dakika moja baadaye.
St.George ambayo ilitolewa kimizengwe katika raundi ya pili ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuichapa Asante Kotoko ya Ghana mabao 4-0 katika mechi ya kwanza Addis Ababa, ingeweza kupata bao la kuongoza kama mshambuliaji wake Fikru Tefera angetumia vizuri nafasi nzuri aliyopata katika dakika ya nne.
Mchezaji huyo alinasa mpira aliokuwa nao beki Ramadhani Wasso lakini jitihada zake zikaokolewa kiufundi na Lulanga Mapunda.
Kocha wa Yanga, Mmalawi Jack Chamangwana alisema timu ilicheza vizuri na kupata nafasi nyingi za wazi lakini walishindwa kuzitumia kwa kufunga magoli.
alisema wakishinda mechi mbili katika kundi lao la ’A’ watakuwa wametinga hatua ya robo fainali hivyo hana wasiwasi wa kutoka mapema bado. Kundi hilo linaongozwa na Ulinzi yenye pointi tatu.
Kocha wa St. George Micho Sredojevic alisema wameridhika na matokeo ya sare kwani alitegemea mchezo huo kuwa mgumu, lakini pia hali ya hewa imewaathiri kwani Ethiopia kwasasa kuna baridi wakati Tanzania kuna joto.
Aliisifu Yanga hatahivyo, kuwa ni timu nzuri ingawa ilikosa nafasi mbili za wazi za kufunga magoli.
Timu zilikuwa:
Yanga: Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Ramadhani Wasso, Edwin Mukenya, Lulanga Mapunda, Mohamed Banka (Amri Kiemba dk. 71), John Barasa, Said Maulid, Thomas Maurice na Gaudence Mwaikimba (Gulla Joshua dk. 62).
St. George: Dennis Onyango, Deyas Degfo, Samson Muwgeta, Abebaw Butako, Degu Debebe, Zablon Amanaka, Assaul Basope, Abraham Kudemor (Mungeta Mehret dk. 72), Mulazor Regassa, Fikru Tefera naJames Omondi (BenjamAssefa dk.68).
Wakati huohuo, timu ya Ulinzi ya Kenya jana Jumamosi iliichapa Polisi ya Zanzibar magoli 2-1 katika mchezo wa kwanza wa Kundi A uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Magoli ya Ulinzi yalifungwa katika dakika za 75 na 85 na Joseph Akinga na Sammy Simiyu, wakati bao la Polisi lilifungwa na Mohamed Seif dakika ya 67 baada ya kupata pasi ya Khamis Supian.
Michuano hiyo inaendelealeo kwa mechi ngumu kati ya Simba ya Bara na APR ya Rwanda, Polisi Uganda kukutana na vibonde SID ya Djibout ambao walilala 6-0 katika mechi ya kwanza Ijumaa Dar es salaam, na katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wenyeji Moro United watawakaribisha mabingwa watetezi wa michuano hiyo SC Villa ya Uganda.
SOURCE: Lete Raha