Na Mwasu Sware
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeongeza adhabu kwa wafanyabiashara ndogondogo watakaoendelea kufanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi, kutoka kati ya Sh2,000 na Sh5,000 na kuwa Sh15,000 na kifungo si chini ya miezi 3.
Akizungumza jana na Mwananchi ofisini kwake jana, Afisa Habari wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, alisema hatua imetokana na wafanyabiashara hao kuendelea kukaidi agizo la Waziri Mkuu, la kuwataka wahamie kwenye maeneo husika yaliyotengwa kwa ajili ya biashara.
Tabu alisema, adhabu zilizokuwa zikitolewa mwanzoni zimeonekana kuwa ndogo. Alisema wafanyabiashara walikuwa wakijifanya mabubu au viziwi pindi wanapokamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka, ili waweze kuachiwa.
"Mwanzoni ilikuwa wanatozwa Sh2,000 hadi Sh5,000, lakini wafanyabiashra wengi wameonekana kumudu adhabu hiyo na hivyo kuendelea kufanya biashara, hivyo hivi sasa mahakama imeongeza faini hadi kufikia Sh15,000, atakayeshindwa atatumikia kifungo kisichopungua miezi mitatu," alisema Tabu.
Alisema kuwa mahakama vilevile inaendelea kuandaa adhabu kwa wafanyabiashra watakao kiuka na kwenda kufanya biashara sehemu isiyostahili.
Tabu alisema kuna kanuni na taratibu za uendeshaji wa Miji hivyo ni lazima zizingatiwe na ziheshimiwe, kuwa Miji inapangwa kutokana na matumzi husika.
Tabu aliyataja maeneo ambayo bado wafanyabiahsra wameendelea kuwa kero ikiwa ni pamoja na Posta mpya, Buguruni, na Kariakoo.