Na Maimuna Kubegeya
JESHI la Polisi nchini limeandaa utaratibu wa kukagua shehena zote za vyuma chakavu katika maeneo ya mipakani vitakavyoingizwa kutoka nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa mabomu hayo yanatoka nchi jirani ambazo hakuzitaja na kuwa jeshi lake limejipanga kukabiliana nayo.
Alisema kupatikana kwa mabomu hayo jijini Dar es Salaam kumelipa fundisho jeshi lake na hivyo kuamua kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo mbalimbali hasa ya mipakani ambapo yanayoshukiwa kuwa ndio chanzo cha uingizwaji wa mabomu hayo.
Januari 2, mwaka huu gazeti hili lilichapisha taarifa yake ya uchunguzi iliyokariri vyanzo mbalimbali vikieleza kuwa mabomu hayo yanatokana nchi jirani zenye hali tete kiusalama, zikiwemo Burundi na Rwanda na yanaingizwa nchini yakiwa ni sehemu ya vyuma chakavu, ambavyo havina uthibiti wa kutosha.
IGP Mwema alisema jeshi lake likishirikiana na tume maalum ya muda itatumia vifaa maalumu vya kukagulia mabomu ambavyo vitapelekwa katika maeneo ya mipakani ili kuweka ulinzi na kuhakikisha mabomu zaidi hayaingii nchini na kuhatarisha maisha ya raia
Alisema kutakuwako na ukaguzi kwa wapokeaji wote wa vyuma hivyo wakiwamo mawakala waliopewa vibali vya biashara ya vyuma chakavu kwa mujibu wa sheria.
Alisema jeshi lake kupitia kikosi chake cha silaha pia linaandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa raia kuhusiana na namna ya kutambua silaha na kuchukua tahadhari kwa silaha mbalimbali yakiwamo mabomu.
Elimu hiyo itatolewa kuanzia mashuleni, vijiweni na maeneo mbalimbali na kwa kuanzia jeshi hilo limeandaa vipeperushi. Pia litaandaa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusiana na suala hilo, alisema Mwema.
Katika hatua nyingine IGP amesema takwimu na taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya jeshi hilo zinaonyesha kuwa hali ya uhalifu nchini imepungua pamoja na kuwa na matukio ya hapa na pale.
IGP aliahidi kuwa jeshi lake litajitahidi kuboresha huduma zake kwa raia na vilevile kuweza kufikia katika maeneo yote nchini ili kuonyesha uwajibikaji wake.
Alisema jeshi hilo pia limeanzisha utaratibu wa kutoa matukio ya wiki kila Ijumaa, ili kuboresha uhusiano wake kati yake na raia kwa lengo la kujenga mahusiano mema.
Akizungumzia suala la dawa za kulevya, IGP Mwema alikiri kuwa bado ni tatizo na kutoa wito kwa jamii kushirikiana na jeshi lake kwa kupeleka taarifa sahihi zitakazosaidia kuwakamata wahusika na kuwatia katika mkono wa sheria
"Taarifa tumepata nyingi, lakini kwa mujibu wa sheria za nchi ni lazima uwe na ushahidi utakaothibitisha tuhuma hizo kwa mtuhumiwa ili kurahisisha ukamataji wake," alisema Mwema.
Alisema polisi wanaongeza nguvu na utaalamu katika kupambana na dawa za kulevya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kama vile Tume ya madawa ya kulevya na Taasisi ya Kuzuia Rushwa.
Akizungumzia tatizo la uzagaaji wa silaha, Mwema alisema oparesheni bado inaendelea na kuwataka wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha katika vituo vya polisi na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokaidi agizo hilo.
Aliwataka wote wanaomiliki sare za jeshi au nguo zinazofanana na za jeshi hilo kuzisalimisha au kuziteketeza kwani wakikamatwa nazo watachukuliwa hatua za kisheria.