Midraji Ibrahim na Muhibu Said
RAIS Jakaya Kikwete leo mchana ataongoza waombolezaji kuupokea mwili wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Juma Akukweti, aliyefariki dunia akiwa nchini Afrika Kusini.
Akukweti (59) aliyekuwa amepelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi Desemba 21, mwaka jana, alifariki saa 8.30 usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Mill Park mjini Johannesburg.
Akitangaza taarifa ya kifo hicho jana kwa niaba ya Rais Kikwete, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Rose Lugembe, alisema serikali ilikuwa inakodisha ndege kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kurejesha mwili wa marehemu nchini.
Mwili wa marehemu Akukweti unatarajiwa kuwasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kati ya saa 6:00 na saa 7:00 mchana.
Waziri Akukweti alikuwa ni miongoni mwa majeruhi wa ajali ya ndege aina ya Cessna namba 5HTZ, mali ya Kampuni ya Tanzanair iliyotokea Desemba 16 mwaka jana, mjini Mbeya.
Katika ajali hiyo, Mwandishi na Mpiga Picha Mwandamizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Theresia Nyantori, alifariki papo hapo na wengine kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, lakini jioni yake walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Majeruhi wawili kati ya watano waliohamishiwa Muhimbili, Mratibu wa Mpango wa Uendelezaji Masoko ya Mazao ya Kilimo (AMSDP), Nathaniel Katinila na Afisa Habari Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, George Bendera, walifariki wakati wakiendelea kupata matibabu Muhimbili.
Rubani wa ndege hiyo, Martin Sumari, amekwisha kutibiwa na kuruhusiwa kutoka Muhimbili huku Msaidizi wa Waziri, Aniceth Kanje, akiendelea kupata matibabu.
Lugembe ambaye wakati wa kutangaza taarifa hiyo alikuwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vincent Mrisho, alisema serikali ilikuwa inawasiliana na familia ya marehemu kwa ajili ya kupanga taratibu na mahali atakapozikwa.
Waziri huyo na ujumbe wake, walikwenda Mbeya kukagua na kutoa pole kutokana na kuungua kwa soko la Mwanjelwa Desemba 15 mwaka jana.
Akukweti alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi kutokana na ushauri uliotolewa na madaktari wake waliokuwa wakimtibu Muhimbili kuwa anahitaji utalaam ambao haupatikani nchini.
Akukweti alizaliwa Septemba 20, 1947 katika Kijiji cha Ligoma, Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma. Mwaka 1958 hadi 1961 alisoma Shule ya Msingi Ligoma na alijiunga Shule ya Kati ya Mattaka kati ya Mwaka 1962 na 1965.
Alisoma Sekondari ya Songea kati ya mwaka 1966 na 1969, baadaye alijiunga Shule ya Sekondari Tabora kwa ajili ya kumaliza masomo yake mwaka 1970-1971.
Mwaka 1972-1975, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Sayansi na Ualimu, mwaka 1978-1979 alijiunga Chuo cha Uongozi Esami na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Uongozi.
Aliajiriwa Chuo cha Usafirishaji kama Mkufunzi mwaka 1975-1979 na 1979-1982, alikuwa mshauri wa wanafunzi katika chuo hicho.
Akukweti, mwaka 1982-1989 aliajiriwa kama Meneja Utawala Taasisi ya Utafiti wa Samaki (Tafiri), baadaye alihamishiwa Kampuni ya Kusindika Mafuta ya Moproco, kushika wadhifa huo hadi mwaka 1990.
Alianza siasa mwaka 1990 hadi kifo chake akiwa amechaguliwa kuwa Mbunge wa Tunduru mfululizo. Mwaka 2000-2005 alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge na Januari 4, 2006 aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Waziri wa Nchi Ofisi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge).
Katika hatua nyingine, Mamia ya waombolezaji, wakiwamo ndugu, jamaa, marafiki na majirani, walianza kumiminika nyumbani kwa marehemu, Masaki Chole, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 asubuhi, huku baadhi wakilia kwa uchungu.
Waombelezaji hao, wakiongozwa na mjane wa marehemu, Awetu Akukweti pamoja na watoto wake wawili, Aziza na Shamsa, walisema taarifa za kifo hicho zimewashtua sana kwani habari walizokuwa wanazipata kutoka Afrika Kusini zilikuwa zikieleza kuwa hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Kauli hiyo iiliongeza majonzi na simanzi na kusababisha eneo lote la nyumba mpya za serikali ambapo Waziri Akukweti alikuwa akiishi na familia yake, kutawalia na vilio kutoka kwa waombolezaji, hususan wanawake.
Kutokana na kuzidiwa na uchungu, mtoto wa mwisho wa marehemu, Shamsa, alizirai na kusaidiwa na baadhi ya waombolezaji ambao walimshikilia na kumtuliza kwa kumlaza chini.
Kwa mujibu wa mtoto wa saba wa marehemu, Aziza, taarifa za maendeleo ya afya ya baba yao, walikuwa wakipelekewa na mama yao mdogo, Esther Akukweti, aliyekuwa akimuuguza marehemu Afrika Kusini.
Alisema taarifa za kifo cha baba yao, walizipata saa 9:00 usiku wa kuamkia jana kutoka kwa mdogo wake, Salma aliyepigiwa simu na kaka yao, Jamaldin Akukweti.
"Kwa kweli nimepokea msiba wa baba kwa masikitiko makubwa, si unajua ni kitu ambacho hatukukiwazia, pia si unajua aliondoka hapa akiwa mzima? Na kila ulipokuwa ukiuliza unaambiwa kuwa ni mzima na anaendelea vizuri hadi alipoingizwa theatre (chumba cha upasuaji) tulikuwa tukiambiwa hivyo," alisema Aziza na kuongeza:
Aziza alisema kuwa baba yao atazikwa kijiji kwake, Ligoma, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
"Of course (ndivyo hivyo) atazikwa Tunduru kwa sababu ndiyo kwake," alisema Aziza.
Mtoto wa kaka ya marehemu, Mariamu Akukweti (26) alisema: "Tumepigiwa tu simu na Ofisi ya Waziri Mkuu, wakaomba watu watakaoshirikiana nao kwenda kupokea mwili."
Aziza alisema anakumbuka alichozungumza na baba yake kwa mara ya mwisho kwamba ilikuwa wakati anapelekwa Afrika Kusini kutibiwa. "Alisema 'Nitarudi, naenda kutibiwa, kaeni salama'".
Aziza alisema kitu kikubwa ambacho kwa kifo hicho, anaamini kuwa amekipoteza, ni upendo wa baba yake ambao alisema alikuwa akiuonyesha kwa watu wote.
"Alimpenda kila mtoto wake na hakumtenga yeyote," alisema Aziza.
Watoto wengine wa marehemu Waziri Akukweti, aliwataja kuwa ni Zainabu, Kassim, Latifa, Khadija, Hamida, Aziza, Rehema, Ashura na Shamsa.
Kwa mujibu wa Mariamu, mtoto wa kwanza kabisa wa Waziri Akukweti, Khamis, alikwisha kufariki tangu akiwa mdogo.
Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amin