Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Makontena ya Zanzibar yakwama Mombasa
Makontena ya Zanzibar yakwama Mombasa
By Habari Tanzania | Published  06/13/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Makontena 350 yenye vyakula na vifaa mbali-mbali vya majumbani yaliyokuwa yakisafirishwa kuja visiwani humu, yamekwama katika Bandari ya Mombasa, nchini Kenya.

Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Bw. Mustafa Aboud Jumbe, alithibitisha jana kukwama kwa makontena hayo.

Bw. Mustapha, alisema makontena hayo yamekwama kutokana na meli kubwa za mizigo kukosa sehemu ya kutosha kufunga gati na kushusha mizigo katika muda muafaka.

Alifafanua kuwa, mbali na makontena hayo, pia makontena mengine 150 ambayo yalikuwa yasafiri-shwe nje ya nchi, yame-kwama Zanzibar kutokana na kukosekana kwa meli ya kuja kuyachukua.

Bw. Mustapha alisema bandari hiyo ina eneo la asilimia 60 inayoweza kutumika kwa ajili ya meli za mizigo na abiria na asilimia 40 inatumiwa kwa ujenzi wa bandari mpya.

Mkurugenzi huyo alisema bandari hiyo ina urefu wa mita 240 wakati mita 90 zinatumiwa na kampuni ya ujenzi ya Phil HIL kutoka nchini Uholanzi na mita 130 zimebakia kwa ajili ya meli na matumizi ya bandari.

’’Ni kweli tumepokea taarifa kutoka Mombasa, Kenya kuwa makontena 350 ya Zanzibar yamekwama katika bandari yao kutokana na kukosekana usafiri wa kuyaleta Zanzibar,’’ alisema Bw. Jumbe.

Alisema hivi sasa meli zinazoruhusiwa kuingia katika Bandari ya Zanzibar ni zenye urefu wa chini ya mita 130, jambo ambalo linasababisha kampuni ya uwakala wa mizigo ya Masker Container kushindwa kuleta meli kubwa za mizigo.

Mkurugenzi huyo alisema meli zinazotumiwa na kampuni hiyo zina urefu wa mita 150 hali inayosababisha viongozi wa kampuni hiyo kutafuta meli ndogo zitakazoweza kusafirisha mizigo hiyo kutoka Mombasa.

Hata hivyo, alisema kampuni nyingi za meli zimekuwa zikilalamika kutumia muda mwingi zinapoleta mizigo Zanzibar na kulazimika kulipa kodi zaidi kwa vile eneo lililobakia hutumiwa kwa zamu kati ya meli za abiria na mizigo.

Bw. Mustapha alisema bandari hiyo hivi sasa inakabiliwa na hali mbaya ya uchakavu na ndio maana uongozi wa shirika hilo umeamua makontena yote yahifadhiwe nje ya bandari eneo la hoteli ya Bwawani.

Alieleza kwamba, lengo la shirika hilo katika mwaka ujao wa fedha ni kukusanya zaidi ya bilioni 4.8 ambapo katika kipindi cha miezi mitano, limekusanya shilingi bilioni 2.5.

’’Tunaomba wafanyabiashara na wananchi Zanzibar wawe wavumilivu wakati huu ambapo ujenzi wa bandari hiyo unaendelea kwa vile tatizo lililopo lipo nje ya uwezo wa shirika,’’ alisema Bw. Mustapha.

Alisema kutokana na uchakavu wa bandari hiyo, wameamua kulifunga eneo la kaskazini la Bandari hiyo.

Baadhi ya wafanyabiashara Zanzibar, wamesema kutokana na tatizo hilo, wanalazimika kushusha mizigo yao katika Bandari ya Tanga au kusafirisha kwa majahazi kuleta Zanzibar.

’’Tatizo hilo limesababishia gharama kubwa za usafirishaji, lakini vile vile ni hatari kwa sababu majahazi tunayoyatumia hayana bima,’’ alisema mfanyabiashara Bw Seif Makame.

Alisema kutokana na hali hiyo, mfumuko wa bei za vyakula umekuwa mkubwa kwa kuwa gharama za usafirishaji zimeongezeka mara mbili.

Ujenzi wa bandari ya Zanzibar ulitarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu, lakini hadi sasa umekuwa ukiendelea kwa kuchechemea kutokana na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza katika mradi huo.

Ujenzi huo unafadhiliwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) ambao wametoa zaidi ya Sh. bilioni 31, unaendeshwa na kampuni ya Phil kutoka Uholanzi.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.