Kwenye fani ya mazingaombwe kuna vitu vikubwa vitatu. Cha kwanza kinaitwa wepesi wa mikono (sleight of hand), cha pili ni viinimacho (illusion) na cha tatu ni kupoteza lengo (distraction). Ili mazingaombwe yafanikiwe na kuwa na mvuto ni lazima vitu hivyo vitatu viende sambamba na kwa wakati muafaka. Sasa mwanamazingaombwe aliyebobea atahakikisha kuwa watu wanashuhudia mtu anaingizwa kwenye sanduku (sleight of hand), sanduku linakatwa nusu kwa upanga (illusion) huku mwanamazingaombwe anawaeleza na kuwachangamsha watu kwa maneno na porojo (distraction).
Pindi lile sanduku likiunganishwa tena na yule mtu aliyewekwa humo akatoka mzima (restoration) basi watu watapiga makofi na kumsifia mwanamazingaombwe wetu kwa onesho zuri na mwanamazingaombwe huyo atachukua pesa zake na kuandaa onesho jingine, na wale ambao hawataki kufikiri juu ya nini wameshuhudia wataendelea kupiga makofi na kuchekelea!
Utamu wa mazingaombwe huharibika pale ambapo watu wanagundua ujanja wa mwanamazingaombwe. Watu wa RDC wameleta mazingaombwe ya hali ya juu na nusura wafanikiwe kumrejesha mtu akiwa bado mzima toka kwenye sanduku. Watanzania walitaka kuridhishwa na onesho zuri la "Umeme". Ndipo wanamazingaombwe toka Houston walipotokea na vikolokolo vyao vya mazingaombwe. Wakawaambia watanzania kuwa wana uwezo wa kuleta nishati (kumkata mtu nusu bila kumuumiza) tena kwa bei rahisi. Watanzania wakaamini na wakawapa nafasi.
Kwa vile wanamazingaombwe wetu hawakuwa na lengo wala uwezo huo iliwabidi wafanye viinimacho. Ndipo wakaagiza "majenereta" ambayo hayakuweza kufika kwa muda muafaka. Wakaanza kuyatengeneza, na kuyaseti ili baadaye yazalishe umeme (ndio kumweka mtu kwenye sanduku kwa taratibu huku watu wakiangalia). Wakaleta na wapiga picha Airport kuona majenereta yanavyoletwa na ndege kubwa zaidi duniani ya mizigo! Watanzania wakapiga makofi na kushangilia!
Wakati watu wanajiuliza hivi kweli wataleta umeme hawa (je kweli mtu ataungika?) basi wanamazingaombwe wa RDC wakaanza kutuhamasisha pamoja na wasaidizi wao (Tanesco) wakilumbana na kukandiana hadharani (distraction). Lengo likiwa kununua muda. Wakati watazamaji (watanzania) wakiendelea kushangaa nini kinaendelea, tukatangaziwa kuwa jenereta liko tayari kuanza kazi wanasubiri Tanesco wakubali umeme wao. Wakati huo wote, RDC walikuwa wanasubiri mvua!!
Hatimaye, dua zao zikasikika na mazingaombwe ya mwaka yakafanyika. Mabwawa ya umeme yakajaa maji, umeme wa RDC haukutumika, Mkataba wa RDC na Tanesco ukauzwa kwa Waarabu, mwenye kutengeneza pesa akatengeneza pesa, na watanzania wakabakia kushangilia umeme wa kudumu (mgao umeisha)! na Rais Kikwete akashangilia na kuwapongeza viongozi wenzake majasiri, hodari na makini kwa jinsi walivyoshughulikia tatizo la umeme!
Onesho la mazingaombwe la RDC likafanyika kwa ufundi mkubwa. Kwa vile Watanzania hawajagundua kuwa wameshuhudia mazingaombwe, basi mwaka unaokuja watasubiri onesho jingine lenye kuhusu mkataba mwingine, na gurudumu la mazingaombwe na viinimacho linaendelea kubingirishwa!