BAADA ya Jeshi la Polisi kuanza kupambana kwa nguvu na biashara ya dawa za kulevya, vigogo wa biashara hiyo wamelazimika kubuni mbinu mpya, ikiwa ni pamoja na kubadili maeneo ya kufanyia biashara hiyo, Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, tayari mmoja wa vigogo wa biashara hiyo aliyekuwa akiwatumia vijana wadogo kumsambazia bidhaa zake katika maeneo ya Kariakoo, Mwananyamala na Kinondoni, amehamishia biashara hiyo katika maeneo mengine nje ya mji.
Habari ambazo Tanzania Daima imezinasa kutoka miongoni mwa vijana walioajiriwa na kigogo huyo, zinayataja maeneo ambako hivi sasa wanaendesha shughuli zao kuwa ni, Vingunguti Bondeni, Coco Beach, Mwembe Yanga na katika maeneo mengine ya fukwe za bahari.
Kigogo huyo anayedaiwa kuwa ni kinara wa biashara hiyo, akiwatumia vijana zaidi ya 30, inasemekana amekuwa akiendesha takriban vijiwe mbalimbali maarufu kwa shughuli hiyo katika maeneo maalum jijini, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa vijana hao, uamuzi wa kigogo huyo kuhamisha makao yake umetokana na wasiwasi kuwa, maeneo ambayo awali yalikuwa yakionekana kuwa salama yamebadilika na kujulikana na vyombo vya usalama.
Waandishi wa Tanzania Daima waliotembelea Vingunguti Bondeni eneo la Makaburini na kukaa huko kwa takriban siku kadhaa, walifanikiwa kukutana na vijana hao wakiwa na mizigo ambayo ilikuwa na bidhaa hizo haramu.
Walipofika kwa mara ya kwanza, hawakuweza kuona dalili zozote za kuwapo kwa biashara hiyo hadi majira ya saa 12:00 jioni ambayo vijana kadhaa wakiwa katika makundi, walikuwa wakionekana wakifika wakiwa wamebeba mabegi mgongoni, mithili ya wasafiri.
“Mambo vipi kichaa wangu, umetuletea dozi au?” ni baadhi ya lugha za kawaida miongoni mwa vijana hao ambazo mmoja wa waandishi wa Tanzania Daima aliyejifanya mmoja kati yao alikuwa akizisikia kila mara alipokuwa nao.
Kwanza mwandishi huyo alipowaeleza vijana hao kuwa alikuwa akitaka kujiunga na kundi lao katika kufanya biashara hiyo, kijana aliyemkaribisha alimtaka kuchukua tahadhari kubwa wakati huu.
“Sisi wenyewe tunataka kuacha. Hii biashara sasa imekuwa ngumu sana, wakati wowote unaweza kukamatwa na polisi. Kabla serikali haijashtukia dili, biashara ilikuwa inalipa, mtu unaweza kuuza hadi ‘M’ (akimaanisha sh milioni moja), hapo ujue una laki moja. Sasa siku nzima unaambulia 50,000 na wakati mwingine unatoka kapa,” alisema kijana mwingine.
Vijana hao walisema, tangu serikali ilipoanza kushughulikia biashara hiyo, tajiri wao ambaye walimtaja kwa jina (jina tunalo), amekuwa mkatili dhidi yao, akifikia hatua ya kukataa kuwalipa ujira kwa ajili ya kazi hiyo kwa madai kwamba biashara hiyo ni mbaya.
Vijana hao wakionekana wachovu walisema kuwa, awali walikuwa wanafanyia biashara yao katika maeneo kadhaa ya Kariakoo, Mwananyamala na Kinondoni.
Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni kwa maelekezo ya tajiri wao huyo, wamelazimika kuhamia Vingunguti na wakati mwingine katika fukwe za bahari kwa sababu ya kuhofia kukamatwa na vyombo vya dola.
Kwa mjibu wa maelezo ya vijana hao, kutokana na ugumu wa mambo hivi sasa, bei ya dawa za kulevya imepanda kutoka sh 2,500 kwa kete hadi kufikia sh 5,000.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na Tanzania Daima, walionyesha wasiwasi wao kutokana na eneo lao kutumika kwa biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.
“Vijana wetu wanaweza kujiingiza katika makundi ya wanaofanya biashara hii, pia matukio ya uhalifu yanaweza kuongezeka,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo (jina tunalo).
Naye Mwandishi Wetu, Christopher Nyenyembe kutoka Mbeya, anaripoti kuwa, Ofisa Uhamiaji anayefanya kazi katika mpaka wa Tanzania na Zambia, katika mji mdogo wa Tunduma, Florian Rweikiza (30), anashikiliwa na Polisi, baada ya kugundulika kuwa alikiuka taratibu za utoaji wa kibali cha usafirishaji wa maiti ya Abdallah Siriri (32), aliyefia nchini Zambia na mwili wake kukutwa na dawa za kulevya.
Kukamatwa kwa ofisa huyo kunakuja siku moja tu baada ya mfanyabiashara wa mji mdogo wa Tunduma, Hamza Lema kunaswa akidaiwa kuwa mfadhili aliyejitolea kulipia gharama zote za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Zamba kuja Tanzania.
Ofisa huyo wa serikali wa daraja la kwanza, anadaiwa kutofuata taratibu za kiofisi, katika utoaji wa kibali kwa watuhumiwa wawili waliovuka mpaka kwenda nchini Zambia kuuchukua mwili wa marehemu Siriri.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Suleiman Kova alisema kuwa, mtuhumiwa huyo zaidi ya kutoa kibali hicho ambacho hakina kumbukumbu zozote, wala namba za ofisi, aliomba awepo wakati mwili wa Siriri ukifanyiwa upasuaji.
Kova alisema kuwa, Rweikiza hakutaka kuchukua vitambulisho vya watuhumiwa Hamis Mengashi (28) na mwenzake Edward Michael (28), ambao ndio walivuka mpaka kwenda nchini Zambia, ili kujua eneo wanalotoka na vitambulisho vyao vya kazi wanazofanya.