Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  AU yabariki Ethiopia kuivamia Somalia
AU yabariki Ethiopia kuivamia Somalia
By Habari Tanzania | Published  12/27/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
ADDIS ABABA, Ethiopia

UMOJA wa Afrika (AU), umesema kwamba Ethiopia ina haki ya kuivamia Somalia kijeshi kwa kuwa inahisi usalama wake unahatarishwa na wapiganaji wa Kiislamu wa nchi hiyo.

AU pia ilikiri kwamba imeshindwa kushughulikia kikamilifu tatizo linaloikabili Somalia.
Ndege za kivita za Ethiopia juzi zilipiga mabomu viwanja vya ndege vya Somalia katika harakati zake za kuisaidia serikali ya muda ya Somalia dhidi ya Umoja wa Mahakama za Kiislamu (UIC).

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, alikwisha kusema kwamba nchi yake iko katika vita na Waislamu hao.

Wakati AU ikisema hivyo, wapiganaji wa Kiislamu jana walirudisha nyuma majeshi yao baada ya wiki moja ya mashambulizi ya mabomu na makombora kati yao na serikali ya muda inayosaidiwa na askari wa Ethiopia.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, askari watiifu wa UIC walijiondoa kilometa zaidi ya 50 kutoka kusini mashariki mwa Daynuney, mji ulio kusini mwa Baidoa, yaliko makao makuu ya serikali.

Kurudisha majeshi huko kunafuatia mashambulizi ya ndege za Ethiopia dhidi ya viwanja viwili vikuu vya kimataifa Somalia, ambavyo Ethiopia ilisema kwamba vinatumika kuingiza silaha.

Wakazi wa vijiji vilivyo kando ya barabara walisema kwamba wapiganaji wa Kiislamu waliondoka katika ngome yao kuu huko Bur Haqaba na walikuwa wakijikusanya pamoja kueleka mji mkuu Mogadishu.

Wapiganaji hao pia walishuhudiwa wakiondoka katika mji wa Bulo Barde, ambako wiki mbili zilizopita walidai kuuteka na kuwatishia wakazi kwamba mtu yeyote asiyeswali mara tano kwa siku atachinjwa.

Mmoja wa viongozi wa UIC, Sheikh Mohamoud Ibrahim Suley, alikiri kuondoka katika sehemu hizo akisema kwamba ni moja ya mbinu zao za kivita.

UN imekadiria kwamba kuna askari 8,000 wa Ethiopia wanaoisaidia serikali ya muda.
Patrick Mazimhaka, naibu mwenyekiti wa Kamisheni ya AU aliliambia Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kwamba AU haitaikosoa Ethiopia kwa kuwa tayari ilishawaeleza kwamba itaingia vitani pale itakapobidi dhidi ya UIC.

Aliongeza: “Ni juu ya kila nchi inapotishiwa kuamua hatua ya kuchukua kulinda uhuru wake.”

Mazimhaka alisema kwamba jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuiunga mkono serikali ya muda.

Pia alisema kwamba AU itakutana kipindi cha siku mbili zijazo kutatua suala hilo pamoja na kuangalia uwezekano wa kutuma haraka jeshi la kulinda amani.

BBC/AP


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.