MKAZI wa Buguruni Kisiwani, jijini Dar es Salaam, Teddy Alfred (43), amejiua kwa kunywa sumu inayodhaniwa kuwa ni ya panya, baada ya kushindwa kulipa madeni ya mchezo wa kubadilishana fedha, maarufu kwa jina la upatu.
Kabla ya kifo chake, Teddy ambaye alikuwa mkusanyaji wa fedha hizo, aliacha ujumbe kwamba ameamua kujiua kutokana na kuzidiwa deni la mchezo wa upatu, linalokaribia kufikia sh 200,000, na hakuwa na uwezo wa kuzilipa, wakati wanawake wenzake aliokuwa akicheza nao upatu, walikuwa wakimsonga kila kukicha kutaka fedha zao.
Katika ujumbe huo, Teddy aliandika kuwa: “Nimeamua kujiua kwa kushindwa kulipa deni la UPATU, na wanaosema wataleta MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA ni waongo, kwani maisha yangu ni ya shida sana na sina mume wa kunisaidia.”
Kifo cha mama huyo ambaye ameacha mtoto wa kike wa umri wa miaka 16, kimeibua simanzi kwa wakazi walio jirani naye, hata kwa waliokuwa wanamdai, kwani siku zote alisikika akizungumzia ugumu wa maisha, alikuwa akilalamikia madeni yaliyokuwa yakimsonga na alikuwa muumini mkubwa wa kupinga mkakati wa Rais Jakaya Kikwete wa kuleta ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’.
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu na mama huyo, kabla ya kifo hicho kutokea juzi, saa saba mchana, mama huyo alishinda akinywa pombe na kula, akisherehekea Sikukuu ya Krismasi, mara nyingi alikuwa akielezea azima yake ya kutaka kujiua, lakini aliokuwa nao ama walidharau au walimwona amelewa, hivyo hawakuwa makini kufuatilia nyendo zake.
“Teddy angejiua toka juzi, kwani majuzi usiku alifika kwenye duka moja (jirani na eneo analoishi) na kuulizia sumu ya panya, akaambiwa hakuna, hatimaye alikwenda kuitafuta sumu hiyo Buguruni sokoni, na ilipofika mchana, aliamua kunywa pombe aina ya gongo na sumu hiyo na hatimaye kufikwa na mauti,” alisema mmoja wa ndugu wa marehemu katika eneo la msiba huo.
Aliongeza kuwa: “Baada ya kunywa sumu hiyo, alikwenda kukaa katikati ya barabara za karibu na uchochoro wa nyumba yake, ghafla tulishuhudia amejilaza barabarani hapo, watu tulihisi amelewa, tulipomsogelea na kujaribu kuzungumza naye, hakuweza kusema, lakini ujumbe wake ndani na vifaa alivyotumia kuchanganya sumu hiyo, vilituonyesha kuwa Teddy alikuwa amekunywa sumu.”
Shuhuda huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema waliamua kumnywesha maziwa ili atapike, ikashindikana, kwa vile hakuweza kufungua mdomo na walikata shauri kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana, lakini alifia njiani kabla ya kufika hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Masindoki Masindoki alikiri kutokea kifo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Masindoki alisema kifo hicho kilitokea juzi saa saba mchana.
Alisema kuwa marehemu alikufa kwa kunywa dawa inayodhaniwa kuwa ni sumu na aliacha ujumbe kuwa “Nimeamua kujiua kwa sababu ya kuzidiwa na madeni ya michezo ya upatu.”
Alisema baada ya kunywa sumu hiyo, alikimbizwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kufariki muda mfupi baadaye. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika tukio jingine, Nasra Shabani (6) amefariki dunia baada ya kuunguzwa na moto sehemu za kichwani na kifuani.
Kamanda Masindoki alisema mtoto huyo alifariki dunia baada ya moto uliozuka ghafla juzi saa 1 jioni, Karakata kwa Gesa, katika nyumba ya Shaban Ramadhani.
Masindoki alisema nyumba hiyo ilikuwa na vyumba sita na moto ulianzia katika chumba cha mpangaji, Hassan Mohamed (36), ambapo uliunguza godoro na kochi.
Alisema baada ya moto huo kutokea, mama wa mtoto alipiga makelele kuomba msaada wa kuzima moto, ambapo mtoto huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kufariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Masindoki alisema chanzo cha moto huo ni taa ya chemli iliyokuwa ikiwaka na kulipuka baada ya muda mfupi. Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).