SAKATA la dawa za kulevya zilizofumuliwa kwenye tumbo la mwili wa marehemu, Abdallah Siriri (32), limeibua siri ya mtandao wa biashara hiyo baada ya polisi kumnasa mfanyabiashara wa Tunduma, Hamza Lema (34), kuwa ndiye aliyefadhili kuusafirisha mwili huo.
Vyanzo vya habari vya uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, vimeeleza kuwa Lema ambaye anashikiliwa na polisi, alitoa sh milioni mbili kwa ajili ya kuusafirisha mwili wa marehemu Siriri kutoka nchini Zambia hadi Tanga.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, kunatokana na taarifa zilizolifikia Jeshi la Polisi kwamba ndiye aliyeomba kibali cha kusafirisha maiti hiyo kutoka Idara ya Uhamiaji katika mpaka wa Tunduma.
Zinaeleza kuwa Lema alisimamia zoezi la upatikanaji wa kibali hicho mpaka kilipopatikana, ambapo maiti hiyo iliruhusiwa kuingia nchini kabla ya kugunduliwa kuwa tumboni ilikuwa imejazwa dawa za kulevya aina ya cocaine.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Suleiman Kova, jana aliwathibitishia waandishi wa habari kukamatwa kwa Lema.
Katika mkutano na waandishi uliofanyika ofisini kwake, muda mfupi baada ya kukutana na maofisa upelelezi kutoka makao makuu Dar es Salaam na wataalamu kutoka kitengo cha dawa za kulevya, Kova alikiri kumshikilia mfanyabiashara huyo.
Alisema mfanyabiashara huyo anaishi eneo la Maporomoko katika mji mdogo wa Tunduma na anafanya biashara ya kuuza vifaa vya umeme.
Alisema mfanyabiashara huyo alitiliwa shaka na kunaswa na Polisi baada ya kujidai kwa maofisa Uhamiaji kuwa maiti hiyo inamhusu.
“Mfanyabiashara huyo, alitumia muda mrefu kuwashawishi wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji ili wairuhusu maiti hiyo kupita, walipokubali na kutoa kibali cha kuusafirisha mwili huo, yeye alilipa gharama ya kuupitisha, sh milioni mbili na gharama nyingine zilizohitajika,” alisema Kova.
“Tumemkamata mfanyabiashara huyo, tunamhoji ili kujua alijihusisha vipi na kwa kiwango gani kwenye suala hili, na alikuwa na uhusiano gani na marehemu yule hadi akatoa sh milioni mbili mpakani.
“Tunataka kujua alitaka kunufaika na nini katika utoaji wa msaada huo, hayo ni maswali machache tunayojiuliza,” alisema Kova.
Kamanda huyo alisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo na wengine saba waliokuwa wakiusafirisha mwili huo, kutasaidia kuweza kuufahamu mtandao mzima wa dawa za kulevya, na kuongeza kuwa hali hiyo itakuwa imefungua ukurasa mpya.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi, lakini uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ndiyo inayojihusisha na kundi lililonaswa na marehemu huyo, na kinachotakiwa ni kujua dawa hizo zinatoka wapi.
Akizungumzia taarifa za awali za ndugu waliouchukua mwili wa marehemu Siriri kwenda kuuzika nyumbani kwao Tanga, Kamanda Kova alisema marehemu alikuwa mfanyabiashara wa mitumba katika Barabara ya 15, na ndugu zake hawafahamu kama alikuwa na biashara nyingine zaidi ya kuuza mitumba.
Uchunguzi wa awali uliofanywa na Tanzania Daima kutoka kwa baadhi ya wakazi wa mji wa Tunduma, unaonyesha kuwa dawa hizo zinatoka Afrika Kusini na ziliingizwa nchini humo kutokea Amerika ya Kusini.
Kutokana na taarifa hizo, Kamanda Kova alisema jeshi hilo halina taarifa zozote za dawa hizo zinakotokea, na kwamba wanafanya mawasiliano na nchi jirani ili kujua chanzo cha dawa hizo ili kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni.
Aliwataka raia wema kutumia namba za simu yake ya mkononi 0754-034224 na 0787-034224, kutoa taarifa ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo, na kwa kupitia tukio hilo, iwe ndiyo nafasi ya kuwataja wengine