MWILI wa Mtanzania aliyefia nchini Zambia, Abdallah Siriri (32), ambao ulirudishwa nchini katika mazingira ya kutatanisha, umekutwa ukiwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 1,003, zinazokadiriwa kuwa na thamani ya sh milioni 26.7 ndani ya tumbo lake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova alisema, Siriri ambaye ni mkazi wa Tanga, alikutwa na mauti nchini Zambia, Jumatano ya wiki iliyopita baada ya pipi moja kupasukia tumboni.
Kamanda Kova alisema kuwa, kundi la watu waliojifanya kuwa ni ndugu wa marehemu waliotajwa kwa majina ya Hamis Mengashi (28) na Edward Mapunda (28), walikwenda Zambia kuuchukua mwili wake baada ya kupata taarifa za msiba huo.
Kova alisema, Jeshi la Polisi lilifuatilia nyendo za watu hao baada ya kuwatilia shaka, na wakabaini kuwapo kwa pilika pilika za kuusafirisha mwili wa ndugu yao kutoka katika Kitongoji cha Isoka nchini Zambia kuja Tanzania.
Alisema wakiwa njiani na mwili huo katika Kitongoji cha Vwawa, kilometa 30 mpakani mwa Tanzania na Zambia, polisi waliwakamata watu saba wakiwa ndani ya gari yenye namba za usajili T 697 AEH aina ya Toyota Coaster.
Aliwataja watu waliokuwamo ndani ya gari hilo ambao nao wanashikiliwa na polisi kuwa, ni dereva wa gari, Amour Salum (30), mkazi wa jijini Dar es Salaam, Hemed Juma (34), Joshua Charles mkazi wa Uyole jijini Mbeya, Husein Omar (29) mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam na Andrew Mwakikato ambaye ni mpiga debe wa Tunduma.
Alisema pamoja na watu hao, polisi iliwanasa pia, Mapunda na Mangashi ambao walipita mpakani hapo wakiwa na kibali cha kwenda kuuchukua mwili wa marehemu nchini Zambia.
Watu hao wawili walikutwa wakiwa na hati zilizokuwa zikionyesha kwamba, walivuka mpaka na kuingia Zambia kwenda kuchukua maiti ingawa hazikuonyesha siku ambayo walivuka kurejea nyumbani.
Kamanda Kova alisema, hali hiyo iliwapa shaka polisi wa kituo cha Vwawa ambao walilazimika kuomba hati ya kuupasua mwili wa marehemu na ndipo walipozikuta kete hizo za mihadarati kwenye utumbo wake mwembamba.
Alisema, mmoja wa watuhumiwa hao, Hemed, aliyekuwa kwenye gari lililobeba mwili wa marehemu, alikutwa na tiketi za ndege za kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia, zilizokatwa Dar es Salaam, ambazo zilitumiwa Desemba 22, siku mbili baada ya kifo cha marehemu.
Kova alisema, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, ukisubiri ndugu halisi wajitokeze. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.