Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Ujenzi wa barabara kuu wakwama
Ujenzi wa barabara kuu wakwama
By Habari Tanzania | Published  12/25/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mwandishi Wetu

MGONGANO mkubwa wa kiutendaji umetokea baina ya makampuni ya ujenzi wa barabara kuu na serikali juu ya mkakati uliopitishwa na serikali ya awamu ya tatu wa kujenga barabara.

Kutokana na mgongano huo, kuna kila dalili kwamba miradi kadhaa ya barabara kuu nchini haitakamilika kwa muda uliopangwa kwa sababu ya ongezeko la fedha za ujenzi ambazo hazikuidhinishwa.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari ambavyo vimezungumza na Mwananchi, mfumo wa kusanifu na kujenga unalalamikiwa kwamba ni mgumu kuutekeleza na umesababisha kupanda kwa gharama za ujenzi na sasa makampuni mengi yanataka serikali iongeze fedha za ujenzi kwa kati ya asilimia 10 na 20.

Kutokana na hali hii, matumaini ya Watanzania kuondokana na adha ya usafiri kwa kukamilika kwa barabara hizo yameanza kufifia.

Barabara hizo ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi ni sehemu ya barabara kuu nchini zilizotatarajiwa kuunganisha mtandao wa nchi nzima.

Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk Makongoro Mahanga, amethibitisha kwamba mgogoro umeibuka baada ya wakandarasi kudai kuwa miradi ya ujenzi waliyopewa wameshindwa kuikamilisha kutokana na utaratibu unaotumika katika kutoa zabuni za ujenzi wake kuonekana ni mzigo kwao.

Tayari serikali imeunda timu ya wataalamu kuchunguza sababu za kukwama kwa ujenzi wa barabara hizo ambazo ulionekana kupambamoto katika serikali iliyopita.

Dk Mahanga alisema kwamba ipo timu ya wataalamu inayotafuta sababu za kusuasua kwa ujenzi wa barabara kuu kadhaa.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwa baadhi ya kampuni za wakandarasi zinataka kuongezewa fedha ili kukamilisha kazi hiyo kutokana na gharama za ujenzi kuongezeka kabla kumaliza kazi waliyopewa.

Wakandarasi hao wanasema kwamba mfumo mpya wa ujenzi ambao kitaalam unajulikana kama kusanifu na kujenga (design and construction) ndiyo chanzo kikuu cha kuongezeka kwa gharama za ujenzi.

Habari zaidi zinaeleza kuwa mfumo huu wa ujenzi ambao asili yake ni nchini Marekani, ulianza kufanya kazi na iliyokuwa Wizara ya Ujenzi (sasa Miundombinu) wakati wa serikali awamu ya tatu.

Baadhi ya wakandarasi waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao walieleza kuwa baada ya kampuni kushinda zabuni hutakiwa kuwasilisha mchoro wa uliosanifiwa na ukipitishwa kampuni hiyo utakiwa kuanza ujenzi.

Walisema chini ya mfumo huo, kampuni iliyoshinda zabuni inapokamilisha kila kitu serikali huteua kampuni ya wahandisi washauri ambayo kazi yake kubwa huwa ni kukagua na kusimamia ujenzi wa barabara.

Habari zinasema, kampuni zilizoteuliwa kusimamia ujenzi wa barabara zilifanya marekebisho katika michoro iliyowasilishwa na wakandarasi husika na hivyo kusababisha ongezeko la gharama.

"Unakuwa umeshasaini mkataba wa kujenga barabara na mhandisi mshauri anafanya marekebisho yake bila ya kujali gharama zinazoongezeka hivyo unapoanza ujenzi lazima ukwame," alisema mhandisi mmoja miongoni mwa kampuni zinazojenga barabara.

Inaelezwa kuwa mfumo huo wa kusanifu na kujenga ni mgeni hapa nchini na kwamba uliozoeleka ni kuwapo mchoro wa barabara baada ya usanifu na kisha kutafuta kampuni ya kujenga kwa kufuata kazi iliyofanywa na kampuni za usanifu.

Miradi ya ujenzi wa barabara inayosuasua kwa sasa ni pamoja na wa Dodoma hadi Manyoni uliochini ya mkandarasi Konoike (Japan) ambayo hadi sasa ni kilometa 69 tu ndio zimekwisha kuwekwa lami na nyingine kama hizo zimekwama.

Barabara nyingine zilizokwama ni kati ya Shinyanga hadi Tinde mkandarasi akiwa ni Grenkey wa China, Lindi hadi Mnazi Mmoja inayojengwa na kampuni ya Karafi & Sons, barabara kati ya Singida hadi Shelui yenye urefu wa kilometa 110 inayojengwa na kampuni ya CIETCO ya China na Nangurukuru-Mbwemkulu -Mingoyo yenye urefu wa kilometa 95.

Dk. Mahanga alithibitisha kukwama kwa ujenzi wa barabara hizo na kwamba serikali inatarajia kupata ripoti ya timu ya wataalamu iliyoiteua kuchunguza hali hiyo.

Alisema timu hiyo itachunguza kwa undani matatizo yanayodaiwa na wakandarasi kuchelewa kumaliza ujenzi wa barabara walizopewa ili wajadiliane nao kabla ya kuchukua hatua nyingine za kwenda kwenye mahakama za usuluhishi.

Dk Mahanga alisema wakandarasi waliochelewa kumaliza kazi zao kila mmoja ana sababu zake. Wapo wanaodai kuwa wamekwama kutokana na mvua zinazonyesha na wengine wanaeleza wamekwama kutokana na kupanda kwa gharama za ujenzi.Aliutetea mfumo unaodaiwa na makandarasi kuwa unaongeza gharama kuwa ni bora ambao unatumika hivi sasa duniani kote.

Naibu waziri huyo alisema miradi ya ujenzi ambayo inatumia mfumo huo wa kusanifu na kujenga kuwa ni pamoja na daraja la Umoja lililopo mkoani Mtwara, ambao unaendelea vizuri na akataja mradi ambao unatumia mfumo tofauti na huo ni barabara ya Rombo ambao umekwama kukamilika.

Alisema mfumo huu huenda haujazoeleka kwa wakandarasi ndio maana wanafikiri matatizo waliyonayo yamesababishwa na mfumo huo.Hata hivyo, Dk Mahanga alihoji ni kwa nini makandarasi walikubali kutumia mfumo huo wa kusanifu na kujenga wakati wakijua kuwa ni wa gharama.

Alisema serikali itahakikisha inaweka mazingira ambayo yatatoa haki kwa pande zote zinazohusika katika suala hilo na kuhakikisha ujenzi wa barabara hizo unaendelea kama ilivyopangwa.

"Tunajua ujenzi hauendi kama tunavyotaka. Umechelewa na tayari kuna mazungumzo baina ya timu ya wataalam na makandarasi na nia ni barabara zijengwe," alisema Dk. Mahanga.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.