Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Je, sifa za Awamu ya Nne ni majungu ya wanahabari?
Je, sifa za Awamu ya Nne ni majungu ya wanahabari?
By Habari Tanzania | Published  12/24/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

WANATAALUMA wa mambo ya habari wanasema kuwa na habari ni kuwa na nguvu au mamlaka makubwa.

Msemo huu unaenda sambamba na ule unaosema kwamba, umashuhuri wa viongozi wa siasa ni matokeo ya kazi ya wanahabari. Watanzania tumeshuhudia ukweli wa misemo hiyo yote miwili katika pilikapilika za kisiasa za Awamu ya Nne.

Viongozi wa Awamu ya Nne waliibuka na kuwa mashuhuri kwenye kampeni mwaka 2005, kwakuwa walisimama karibu sana na kuwakumbatia wanahabari kwa hali na mali.

Yapata miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, tayari wanahabari wengi walikuwa na rais wao na walimpigia debe hadi kweli akafika Ikulu. Lakini suala la kujiuliza ni kama sifa zote walizomwagiwa viongozi wa Awamu ya Nne kama ni kweli wanazo?

Kama ambavyo kampeni za Awamu ya Nne zilivyosema Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na maisha bora kwa kila Mtanzania, Watanzania walijawa na matumaini makubwa kwamba sifa za viongozi hao kweli zitalikomboa taifa.

Tunachokiona hivi sasa ni kinyume cha matarajio hayo. Ari Mpya imekwisha, Watanzania wamevunjika moyo, hawaoni kama kuna matumaini mbele yao kwa kuwa maisha yamekuwa magumu zaidi kuliko yalivyokuwa miezi 12 iliyopita.

Kipato chao kimepungua zaidi ya maradufu wakati bei za mahitaji ya lazima kama mchele, maharage, gharama za usafiri, kodi ya pango na vifaa vya ujenzi vimepanda zaidi ya mara mbili.

Kwa maana hii, nguvu ya kusonga mbele kujipatia maendeleo haipo kwa vile hakuna umeme, maji n.k.

Mvua imenyesha ikaisha na imeanza tena, hakuna kiongozi anayewaeleza wakulima mvua hiyo ni ya kulimia au kupandia.

Hakuna kiongozi anayeeleza kama wakulima wamepewa mbegu au pembejeo kwa hiyo kwa eneo hili la wakulima hakuna uongozi kabisa kwa sababu kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia.

Yule kiongozi aliyekuwa anaishi na wakulima akiwaelekeza jinsi ya kulima mashamba, kupanda mazao na kulima, mwasisi wa taifa hili, hayati Mwalimu Julius Nyerere, hatunaye tena na hivyo tumebaki na manyapara wanaotoa amri na wanaopasua anga za juu na kupenda sifa.

Katika maeneo ya mijini, binadamu sasa wamekuwa sehemu za uchafu, wale wale waliokuwa wanashangilia ari mpya, sasa wanakusanywa na kuswagwa kama wakimbizi na kupelekwa kwenye maeneo yaliyo mithili ya dampo, huko wakajitafutie riziki zao, tunawaita ‘Wamachinga’.

Ajira waliyoahidiwa kwao zimekuwa ndoto za Alfulela ulela. Kwa ujumla, kasi tuliyoahidiwa ya uchumi kwamba tutakuwa na kasi ya kwenda mbele, imekuwa kinyume chake. Ila kweli Kasi ipo, lakini ni ya kurudi nyuma.

Panapokuwa hakuna ari ya wananchi na hakuna nguvu ya wananchi, lakini kuna kasi ya viongozi kubomoabomoa kile walichonacho wananchi, kuna kasi ya viongozi kuweka saini mikataba ya kifisadi ya uchimbaji madini, kuuza rasilimali za umma na kuuza nyumba za serikali kiholela.

Wajibu wa waandishi wa habari wenzangu katika haya yote ni kuieleza jamii, hawa tuliowapigia debe kuingia madarakani ni watu wa aina gani. Na tukae tukijua tayari wananchi huko mitaani wameishaanza kusema waandishi wa habari tumewasaliti, kwakuwa tumekuwa tukiandika habari za kusifia kuliko habari zenye masilahi ya wananchi.

Mbona waandishi wa habari miongoni mwetu tuliwaambia wananchi kupitia vyombo vya habari kuwa wamepata viongozi wazuri.

Sisi waandishi ndio tuliwaambia wananchi kuwa Rais Kikwete amefunika awamu zilizomtangulia, sasa ukweli uko wapi?

Ebu sisi waandishi wa habari tuwaeleze raia ubora wa Rais Kikwete unaomzidi mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na rais wa Awamu ya Tatu Rais Benjamin Mkapa.

Tukishindwa kueleza hilo kwamba ni ya kweli, basi sisi waandishi wa habari ni wapika majungu na ni lazima tuwajibike kitaaluma, kwakuwa tutakuwa tumesaliti taaluma yetu kwa kuwaambia wananchi uongo.

Uandishi wa habari ni taaluma inayoshughulika na utoaji wa habari, lakini habari hizo ziwe za kweli, na lazima habari hizo zielekeze taifa jinsi ya kujipatia maendeleo.
Pale ambapo uandishi wa habari unapokuwa ni wa kisanii, kwa maana halisi ya kujikomba kwa wenye madaraka na kuwaambia wananchi mambo yasiyo ya ukweli ni usaliti wa taaluma ya habari.

Sasa tumeshuhudia katika Awamu ya Nne kwamba baadhi ya vyombo vya habari na wanahabari walisaliti taaluma kwa matarajio ya kupewa vyeo na hadi leo hali hiyo ipo kwa kuwa vyeo bado vipo, wapo waliopata na waliokosa.

Sasa tuwekane sawa, tuanze kufanya kazi kwa misingi ya taaluma na maadili kwakuwa aibu tuliyoipata inatosha. Na tukumbuke kuwa kitakachokomboa taifa letu ni ukweli usiopakwa rangi ya dini, vyama, vyeo n.k.

Kwa kuwa tunapowaeleza ukweli wananchi tunawapa ari, nguvu, kasi na uwezo wa kuamua na kutawala maendeleo yao na kuchochea kasi ya kwenda mbele kwa taifa letu.

Mungu ibariki Tanzania.

0755312859; katabazihappy@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.