JANA, karibu vyombo vyote vya habari nchini vilipamba habari zao kutokana na tamko la Rais Jakaya Kikwete, la kukataa sifa za uongo anazodai kupewa na watu mbalimbali kuhusu uongozi wake, tangu alipochaguliwa kuongoza taifa mwaka jana.
Kauli hiyo nzito ya kwanza na ya aina yake toka kwa Kikwete, aliitoa juzi mjini Dodoma, alikokwenda kufungua mafunzo ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni mwenyekiti wake.
Kikwete alidiriki kusema kwamba, anakerwa na sifa za uongo, na kwamba angependa kuona watu wakimkosoa badala ya kumbebesha mzigo wa sifa zisizo na ukweli wowote.
Kimsingi, rais ameiboresha kauli yake aliyoitoa hivi karibuni alipofanya mahojiano na vyombo kadhaa vya habari na akasema, pale Ikulu hakuna mazungumzo bali kilichopo ni ‘ndiyo mzee.’
Kwa hakika, kati ya kauli za Rais Kikwete zinazopaswa kuungwa mkono na Watanzania, basi ni pamoja na hii ya kuwakataa ‘wapambe nuksi’.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, mara kadhaa watu wanaomzunguka Rais Kikwete, wamekuwa wakifanya hicho alichokishitukia kwa ajili ya kujikomba.
Si kujikomba kwa manufaa ya wengi, bali kwa manufaa binafsi, wakitaka waonekane walio bora mbele ya rais.
Kwa mtazamo wetu, watu wa aina hii ni maadui, kwani wanamjaza ujinga rais badala ya kumsaidia katika kazi ngumu aliyonayo katika kupambana na ahadi lukuki alizotoa, alipokuwa anajinadi mwishoni mwa mwaka jana, alipokuwa anataka apewe ridhaa ya kuingia Ikulu.
Tunaamini kwa kulitamka hilo, Rais Kikwete sasa ataanza kuiongoza nchi kwa kufuata misingi na taratibu halisi za majukumu yake.
Hii ina maana kwamba, hatawapa mwanya wanafiki waliokuwa wanapelekea umbeya badala ya ushauri, hali ambayo tunadhani itachangia kwa kiasi kikubwa ufanisi wa utendaji wake na viongozi wake wakuu.
Kama rais ameliona hilo, ni vyema hata wasaidizi wake, kuanzia Waziri Mkuu, mawaziri, makatibu wa wizara, wakuu wa mikoa hadi kule wilayani, wakafuata nyayo za Kikwete anayeonyesha ameanza kujua wajibu wake kwa watu anaowaongoza.
Ameshadanganywa vya kutosha na watendaji wa sekta kadhaa nyeti nchini, lakini pengine alikuwa hajabaini, na sasa ameanza kutoa makucha yake.
Tuseme ameamua kwamba, muda wa kufanya kazi kwa majungu sasa basi, ni kazi tu ili kujaribu kutimiza ndoto za mamilioni ya Watanzania ambao bila shaka wameupitisha kwa madhila makubwa mwaka mmoja wa uongozi wake.
Tunaamini kwa staili mpya ya Rais Kikwete, angalau kiwango cha uwajibikaji kitapanda na kuanza kurudisha hadhi ya mkuu huyo wa nchi aliyekuwa anaanza kupoteza umaarufu, kama ripoti ya utafiti ya Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) ilivyoonyesha kwamba, idadi ya watu wanaopendezwa na utendaji wake imeshuka.
Tunadhani njia pekee ya kurudisha imani ni kuchapa kazi, kama alivyobaini na kukataa sifa anazobebeshwa kila kukicha, ilhali nchi ikizidi kumomonyoka.
Ndiyo maana tunasema, heri Rais Kikwete amegundua unafiki anaofanyiwa. Tunaamini wanafiki waliokuwa wakitaka kutumia nafasi yake kumharibia kwa kumpa sifa za kijinga watakuwa wameumbuka na badala yake watabadili mwelekeo na kuanza kumpa ushauri