OFISA Habari wa Kitengo cha Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, George Bendera, ambaye aliumia vibaya katika ajali ya ndege aina ya Tanzanair, iliyokuwa imebeba msafara wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) Juma Akukweti, amefariki dunia.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana, zilieleza kuwa marehemu Bendera alifariki dunia jana usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) alikokuwa akitibiwa.
Taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa jana, ilieleza kuwa mwili wa marehemu Bendera utasafirishwa kesho kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Bigwa, Morogoro, baada ya kutoa heshima za mwisho katika Kanisa Katoliki Muhimbili.
Marehemu Bendera ni miongoni mwa majeruhi watano waliopata ajali katika ndege pamoja na Waziri Akukweti Desemba 16 wakiwa njiani kurejea Dar es Salaam wakitokea Mbeya kukagua athari za moto uliounguza Soko la Mwanjelwa.
Katika ajali hiyo, mwandishi wa habari mwandamizi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Theresia ‘Teddy’ Nyantori alifariki dunia papo hapo na aliyekuwa Mratibu Mkuu wa Mpango wa Uendelezaji wa Mazao Ofisi ya Waziri Mkuu, Nathaniel Kitinila, alifariki siku mbili baadaye katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Wakati huo huo, Waziri Akukweti juzi usiku alipelekwa katika Hospitali ya Mill Park, Johannesburg, Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.