WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wametahadharishwa juu ya uwezekano wa kutokea kwa kimbunga kitakachoambatana na mvua na upepo mkali.
Tahadhari hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana.
Kamishna Tibaigana alisema taarifa iliyotolewa na Idara ya Hali ya Hewa nchini imetahadharisha kutokea kwa kimbuga hicho.
Tibaigana alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na taarifa za uwezekano wa kutokea kwa kimbunga hicho kwa kuepuka kuogelea baharini hasa kutika kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
Alisema Polisi wataweka ulinzi katika maeneo ya ufukwe wa bahari ambapo askari wa doria watakuwapo katika maeneo hayo ili kuhakikisha hali ya usalama inakuwapo.
Aidha Tibaigana alisema kutokana na hali ya wasiwasi ya ubora wa kivuko kinachosafirisha abiria kutoka Magogoni kwenda Kigamboni, watumiaji wa kivuko hicho, wametakiwa kipindi hiki cha sikukuu, kutojazana katika kivuko ili kuepuka uwezekano wa kivuko kuzidiwa na kusababisha ajali
Aliwataka watumishi wa kivuko hicho kuwa makini na kutoa taarifa kila mara kinapokwama au kupata tatizo jingine lolote.
Alisema watumishi wa kivuko hicho wanapaswa kuhakikisha kuwa hakijazi abiria kupita kiasi na madereva wanaopenda kwenda Kigamboni kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi watumie njia ya Kongowe badala ya kulazimisha magari kupitia katika kivuko hicho.
Tibaigana alisema amewaelekeza makamanda wa Polisi wa mikoa, wilaya na vituo kufanya tathmini ya makanisa ambayo yatakuwa na ibada za usiku ili yapewe ulinzi.
Alisema familia zitakazokwenda kushiriki ibada usiku, zihakikishe kuna ulinzi katika nyumba zao na polisi watafanya doria za jumla mtaani.
Kwa wenye magari ambao watayatumia kwenda nayo kanisani, alisema hawataruhusiwa kuyaondoa mpaka ibada itakapomalizika na kwamba atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema ufyatuaji wa fataki hautaruhusiwa katika kipindi chote cha sikukuu za Krismasi na mwaka mpya kutokana na kujitokeza kwa vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha.
Alisema yeyote atakaye kuwa na mtoto na kumwacha kupotea atachukuliwa hatua za kisheria, alisema askari hasa wa kike watakuwa katika maeneo watakayokuwa wakisherehekea watoto.