WAKATI waamini wote wa dini ya Kikristu duniani wakijiandaa kusherehekea Sikukuu ya Krismasi kesho, miti ya mikrismasi imeonekana kuwa adimu katika Jiji la Dar es Salaam.
Miti hiyo maarufu, imekuwa ikitumika sana katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismasi kwa kupamba kanisa, nyumba na sehemu mbalimbali zikiwamo za burudani, ikiwa ni ishara ya kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristu, takribani miaka 2000 iliyopita.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa siku mbili, umebaini kuwa, miti hiyo imetoweka na kusababisha kuwa ghali mno pindi inapoonekana.
Imebainika sababu kubwa ya kupotea kwa miti hiyo, ni hatua ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuzuia kukatwa miti hovyo.
Maeneo maarufu ambayo miti hiyo imekuwa ikipatikana kwa miaka yote ni Tazara, Ubungo, Mwenge na njia panda ya Tabata.
Tanzania Daima imeshuhudia baadhi ya wakazi wa maeneo ya Tabata, Ubungo, Msasani na katika maeneo mengine ya jiji, wakihaha huku na kule kutafuta miti hiyo bila mafanikio.
Lilian Ibrahim mkazi wa Msasani, alisema kuwa kwa siku mbili sasa amekuwa akitafuta miti hiyo ilhali amekuwa akifika katika maeneo inakouzwa na kushindwa kuipata.
“Jana niliambiwa kuwa miti hiyo inapatikana maeneo ya Tazara, lakini nimefika katika eneo hilo na sikuipata.
“Inasemekana kuwa watu wa Idara ya Misitu wamekuwa wakikamata magari yote yanayopakiza miti hiyo kutokana na sheria inayozuia ukataji miti hovyo,” alisema Lilian.
Katika maeneo ya Kariakoo, Tanzania Daima ilimshuhudia mkazi aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Kigamboni, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, akiwa na tawi la mti huo.
Mkazi huyo alisema amepata tawi la mti huo katika maeneo ya Tabata baada ya kuelekezwa na jirani yake.
“Tawi hili unaloliona nimelinunua kwa sh 7,000. Mwaka huu miti hii haipatikani kirahisi kama miaka mingine iliyotangulia,” alisema mkazi huyo huku akipanda basi na kuondoka.
Juhudi za kuwapata maofisa waandamizi wa wizara, akiwamo Ofisa Habari Mkuu, Sheiba Lal Bul, jana zilikwama.