Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mwekezaji Mzungu ageuka sumu Hifadhi ya Serengeti
Mwekezaji Mzungu ageuka sumu Hifadhi ya Serengeti
By Habari Tanzania | Published  12/24/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mobini Sarya

UAMUZI wa serikali kukaa kimya muda mrefu kushughulikia kilio cha wananchi wanaoishi karibu na eneo la Hifadhi ya Serengeti wilayani Bunda na Serengeti, limechukua sura mpya kutokana na vitendo vya kikatili vinavyodaiwa kufanywa na mzungu mmoja bilionea aliyenunua eneo ndani ya hifadhi hiyo.

Kwa muda mrefu, wananchi wa wilaya hizo wanaoishi kwenye vijiji vinavyoizunguka mbuga ya Hifadhi ya Serengeti, wamekuwa wakiishi kama watumwa waliouzwa kwa mwekezaji huyo kutoka Marekani, anayemiliki hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano hifadhini humo.

Mbunge wa Serengeti, Dk. James Wanyancha, alikuwa kiongozi wa kwanza kuvunja ukimya huo hivi karibuni, alipotembelea jimbo hilo na kupokea malalalmiko ya wananchi kuhusu vitendo wanavyotendewa na kampuni hiyo, huku viongozi wa serikali wakiwa kimya.

Wananchi hao walimweleza kwa nyakati tofauti alipopita kwenye kata zao kuwa, toka kampuni hiyo iwekeze, wamekuwa hawana amani kabisa kutokana na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa na askari wa kampuni hiyo, waliogawanyika makundi mawili; VGS na Grumeti.

VGS ni askari wa kampuni hiyo waliopewa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kulinda vijiji vinavyoizunguka hifadhi hiyo, ili kuhakikisha hakuna mwanakijiji yeyote anayepika kitoweo cha nyama ya porini, wakati Grumeti ni askari wanaolinda hifadhini na kutembeza watalii.

Askari hao kila mmoja kwa nafasi yake, wamekuwa wakitumia udhaifu uliopo miongoni mwa viongozi wa serikali mkoani Mara, kuwapiga wananchi kuwadhalilisha na kuwafungulia kesi za uongo na kukiuka hata utaratibu wa sheria za nchi.

Baada ya kupokea malamiko, Dk. Wanyancha alisema kuwa, vitendo vinavyofanywa na askari wa kampuni hiyo kwa kuwachapa wananchi bakora, hasa watu wazima mbele ya watoto wao, ni vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Inadaiwa na wananchi hao kuwa, askari wa kampuni hiyo, wamekuwa na tabia ya kuwachapa bakora kila wanapowakuta wamepika nyama za wanyama pori.

Pia wananchi hao walisema kuwa, wamekuwa wakibughudhiwa majumbani kwao na askari wa kampuni hiyo, wanaofungua vyungu wakitaka kuona ni mboga gani zimepikwa siku hiyo, wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na kampuni hiyo kuanzisha utaratibu wa kuwakamata watu na kuwazushia kesi za kutunga.

Dk. Wanyancha aliiomba serikali kuingilia kati, kwani jeshi hilo limeanzishwa kinyume cha sheria za nchi bila kufuata utaratibu na linapaswa kuvunjwa.

Inadaiwa kuwa, jeshi hilo linapewa mafunzo ya kijeshi yanayotolewa na maofisa wa jeshi wastaafu kutoka Afrika Kusini na Australia.

“Ndio, ni wanajeshi hao kama si wastaafu, wanaonekana hata miili yao. Waliwapa vijana mafunzo ya kijeshi makali ambayo wengi walishindwa kuvumilia na kuyakimbia,” anasema askari mmoja wa Game Reserve kutoka pori la akiba la Ikorongo akielezea jinsi wakufunzi hao walivyo.

Hata hivyo, pamoja na mbunge huyo kutaka jeshi hilo livunjwe na kuitaka kampuni hiyo kuacha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, Tanzania Daima ilifika kwenye kampuni hiyo na kukutana na ofisa utumishi, Nelson Mafie.

Ofisa huyo aliwaambiwa waandishi wa habari kuwa watu wanaoishutumu kampuni hiyo hawapendi kuiona ikiendelea na kwamba jeshi analodai mbunge livunjwe, liliundwa kisheria, ndio maana DC, RPC na maofisa wengine wa usalama wamekaa kimya.

Lakini mkuu wa wilaya hiyo, Edward ole Lenga alipohojiwa alisema kwamba, kwa sababu ya kuwa mgeni katika wilaya hiyo, bado alikuwa akiendelea kujifunza mwenendo wa mambo mbalimbali.

Hata hivyo, alipopigiwa simu tena baada ya siku chache, alisema kulikuwa hakuna jeshi lolote, wala watu wa namna hiyo

“Huo ni uongo, mbona magazeti yameandika wee jeshi, jeshi lakini mimi nawaambia ni uongo, hakuna,” alisema Lenga.

Maelezo ya viongozi hao yanatofautiana na yale ya wananchi wa Kijiji cha Nyichoka, ambao kutokana na kile wanachokielezea kuwa ni ugumu wa mambo, walifikia hatua ya kuwaita waandishi wa habari kutembelea kijiji chao, ili kujionea jinsi mwekezaji huyo anavyofanya uharibifu kijijini hapo, ikiwa ni pamoja na watu wake kuchoma moto milima katika kile kinachoonekana kuwa ni kusaka utajiri wa madini.

Wananchi wa wilaya hiyo wanaituhumu kampuni hiyo kuwa imekuwa ikitumiwa na wakubwa wasio waaminifu kutorosha mali kwenda nje bila kuhojiwa na kutolea mfano mayai ya mbuni zaidi ya 200 yaliyokutwa na wabunge waliotembelea kampuni hiyo yakiwa tayari kusafirishwa kwenda nje.

Ilidaiwa kuwa, baada ya wabunge hao kuyakamata na bila kutolewa maelezo, sasa yanahifadhiwa katika pori la akiba la Ikolongo.

Askari wa Game Reserve kutoka pori la akiba la Ikolongo, waliwaambia waandishi wa habari kwa siri kuwa, kuna taarifa zinazoonyesha kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikiwatega wanyama wadogo kama chui na kuwasafirisha kwa kutumia viwanja vya ndege vilivyoko hifadhini humo, kikiwamo kile cha Solonera.

“Humu hakuna ulinzi usiku na mchana. Ndege zinaruka kwenye mbuga hii na kutua bila kuhojiwa. Ukiuliza unaambiwa ni ya mwekezaji. Tumekwisha gundua kuwa, wanasafirisha madini aina ya Green Thomarin,” alisema askari mmoja aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina.

Diwani mmoja aliyezungumza katika kikao cha Baraza la Halmashauri alisema, anasikitishwa na vitendo ambavyo wananchi wake wanafanyiwa na kampuni hiyo ya Grumet Reserve Fund na sasa wananchi hao wamechoka.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Diwani wa Kata ya Mcharo, Julius Marigeri ambaye alisema kuwa, kwa sasa ni vigumu wananchi kuvumilia vitendo vinavyofanywa na kampuni hiyo, kwani vinakiuka misingi ya haki za kibinadamu.

Marigeri alivitaja kuwa ni pamoja na wananchi kuchapwa bakora na askari wa kampuni hiyo wanapokwenda kuoga au kuchota maji na kunywesha mifugo kwenye Mto Rubana, unaotenganisha vijiji na hifadhi hiyo, ambao wamekuwa wakiutumia kwa miaka mingi.

Marigeri alisema kuwa, kutokana na kipigo wanachokipata wananchi hao kutoka kwa kampuni hiyo ya mwekezaji, tayari watu kadhaa wamepoteza maisha, na akamtaja mtu mmoja aliyepoteza maisha kuwa ni, Ntonga Manongo (65) aliyekutwa anaoga mtoni na askari wa kampuni hiyo kabla ya kuanza kumchapa bakora hadi alipopoteza maisha.

Pia askari wa kampuni hiyo wanadaiwa kusababisha uhasama mkubwa kati yao na jamii inayozunguka mbuga kwani baadhi ya wafanyakazi wake wanadaiwa kujihusisha katika mahusiano yasiyofaa na wake za watu, ambao huwachukua na kukaa nao porini kwa siku kadhaa.

Diwani wa Kata ya Unyari, Sumera Kiarata akieleza kero inayoletwa na kampuni hiyo alisema kuwa, mwekezaji huyo alipora maeneo ya wazi ambayo wananchi wanatakiwa kuwinda ili kujipatia kitoweo kwa ahadi kwamba, atakuwa anawalipa kila kijiji sh mil. 1.8, ingawa tangu alipopewa mwaka 2004 alifanya hivyo kwa mwaka mmoja tu.

Diwani mwingine wa Kata ya Kuzungu, Ndovu Chacha, alisema wanafunzi wawili tayari wamekamatwa na askari wa kampuni hiyo na kufikishwa mahakamani huku wakiendelea kukaa mahabusu kwa siku kadhaa bila sababu baada ya kukutwa wanaoga na kufua nguo za shule katika Mto Rubana.

Ili kuonyesha kuwa kampuni hiyo imeleta maafa wilayani hapo, diwani mmoja alikiambia kikao hicho cha Baraza la Halmashauri kuwa, jambo hilo wamelazimika kulifikisha katika Halmashauri ya CCM ya wilaya na wana matumaini limekwishafika ngazi ya taifa.

Wakazi wa Serengeti, nao wanalalamikia halmashauri hiyo kuwasaliti kwa kuchukua eneo linalotambulika kisheria na serikali kuwa la wawindaji wadogo kwa ajili ya kitoweo na kumuuzia mwekezaji huyo kinyume cha sheria za nchi, ambazo ilipaswa itangazwe tenda gazetini.

Baada ya kumuuzia eneo hilo kwa mkataba wa kulipwa sh mil. 80 kwa mwaka, ndipo mwekezaji akaanzisha utarabu wa kuhakikisha hakuna mwananchi anapika nyama kutoka porini.

Wakazi na baadhi ya madiwani wanadai kuwa, baadhi ya madiwani na watendaji wengine wa wilaya wamekuwa wakifanya kazi kwa masilahi ya mwekezaji, wakimtaja mwenyekiti wa Baraza la halmashauri hiyo, John Ng’oina.

Mwenyekiti huyo alihojiwa katika kikao cha baraza hilo hivi karibuni, kwanini amekuwa mjumbe wa bodi inayounda kampuni hiyo na atawezaje kuijadili kampuni hiyo ikileta matatizo jambo ambalo aliwajibu madiwani kuwa si kosa kujiunga.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Waziri wa Usalama wa Raia kuelezea mateso wanayopata wananchi, pamoja na kuunda jeshi, hakuweza kupatikana kwa maelezo kwamba alikuwa kwenye kikao mkoani Dodoma na naibu wake.

Pia gazeti hili lilifanya mahojiano na viongozi wa usalama mkoani Mara, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Edward Ole Lenga, aliyesema kuwa hana taarifa na kuwepo jeshi kwenye eneo lake, huo ni uongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi mkoani Mara (RPC), David ole Saibul, alisema kuwa wale ni walinzi tu kama walivyo walinzi wengine wa kampuni binafsi na kwa hiyo hawezi kuwafuatilia, maana hawamuhusu.

Wakati wakisema hayo, kuna habari kwamba hivi karibuni, viongozi wa Kata ya Kunzugu na Mcharo, waliitisha mkutano na wananchi wakaeleza kero zao, wanawake wakawa wanaelezea hadi wanalia kutokana na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa na askari hao, ikiwamo kubakwa na kuiomba serikali ifanye uchunguzi.

Hivi karibuni, Tume ya Haki za Binadamu ilifanya ziara yake Mkoa wa Mara. Katika Wilaya ya Serengeti, ilipokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kampuni hiyo jinsi inavyowanyanyasa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Rubabi)
    Rating
    Hivi ndivyo viongozi wetu wanavyofanya,wanauza nchi yetu na kujigamba kwamba wawekezaji wameleta maendeleo,maendeleo yako wapi hapo?Wakati wananchi wananyanyaswa hivi na hakuna anayewashughulikia?
     
  • Comment #2 (Posted by Mtanzania mwenzenu)
    Rating
    Kama huyo bwana ni mzungu wa Kimarekani yawekana kabisa malalamiko hayo ni ya kweli kwani siku zote Weupe huwadharau sana weusi huko Marekani. jambo la busara ni serikali za ngazi ya Kijiji wakishirikiana na Wilaya hadi Mkoa kufanya uchunguzi kuangalia makosa yako wapi.
    Haiwezekani vijiji vyote hivyo vikawa vinalalamika bure.
    Halafu kitu kingine. Mkuu wa Wilaya ya Serengeti hakupaswa kutoa kauli ya haraka kuita malalamiko ya wananci uongo wakati hajafanya utafiti. Huu ni ujeri tu usio na maana. RPC kujilinganisha na walinzi wa makampuni binafsi ni fedheha katika jeshi.
    Hivyo basi, Mwandishi wasiliana tena na waziri husika au naibu wake halafu uandike majibu yao safu hii tena. Kama hawatatoa majibu ya maana nitalishughulikia mwenyewe.Naomba wasisubiri niliingilie kati. Aksante kwa kazi nzuri
     
  • Comment #3 (Posted by Ritte)
    Rating
    Najiuliza,hivi Tanzania tuna viongozi toka kuzimu au ni laana?Kila uchafu unaofanywa na mgeni hasa Mzungu ni Tanzania tu,na viongozi wanaona. Mgeni anaishi kama malaika mwananchi ni mumwa,hebu nenda kwao uishi hivyo.Mbona viongozi wetu kila leo wanatumia fedha yetu wanakwenda nje lakini bado hawajifunzi au wana vichwa vya mawe?Tutachekwa na kuonewa hadilini? Mimi niko Urusi kuna matezo kwa wageni na huwezi toka peke yako sehemu zingine,wanakuua na hakuna wa kuhoji. Mheshimiwa rahisis sikiza watu wako na ufuatilie kilio chao vinginevyo kwa viongozi uliowapelekea watakufa nawe utakwenda kujibu siku ya mwisho ulikopeleka wale uliopewa.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.