RAIS Jakaya Kikwete, amesema anakerwa na sifa za uongo ambazo amekuwa akipewa na watu mbalimbali kuhusu uongozi wake, tangu alipochaguliwa kuongoza taifa mwaka jana.
Alisema akiwa kiongozi anayetambua wajibu wake kwa watu anaowaongoza, angependa kuona watu wakimkosoa badala ya kumbebesha mzigo wa sifa zisizo na ukweli wowote.
Kikwete aliyatoa maneno hayo mazito ya kwanza yenye mtazamo unaoweza kubadili mitazamo ya watu wengi wakati akifungua mafunzo ya makada wa Chama Cha Mapinduzi mjini hapa jana.
Alisema hafanyi kazi kutokana na sifa za uongo kwa kuwa haziwezi kumsaidia katika uongozi wake na serikali yake.
Kikwete alisema kiongozi yeyote anayependa sifa katika uongozi wake, ni lazima atapata matatizo katika kuongoza kwa kuwa kinachotakiwa si sifa na badala yake ni kufanya kazi kwa uhakika.
“Sipendi sifa za uongo kwa sababu hazitanisaidia chochote na katika uongozi na pia serikali yangu. Mtu anakwambia unapendwa sana na wananchi. Je, ni kweli?” alihoji Kikwete.
Rais Kikwete alisema ili CCM iendelee kustawi na kuimarika, inapaswa kuongozwa katika misingi na taratibu zilizowekwa badala ya kujikita katika majungu.
“Nina marafiki ndani ya chama, na sijarithi maadui wa watu. Kuna kisa gani hadi nirithi maadui wa mtu? Adui yako si wangu. Tusiongoze chama kwa majungu,” alisema Rais Kikwete pasipo kueleza ni nani hasa alikuwa akimwelekezea maneno hayo.
Aliwaonya wanachama wa CCM kuacha kuongoza chama hicho kwa majungu kwa kuwa hawatafika mbali.