Wafanyabiashara watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kuingiza Visiwani Zanzibar shehena ya kuku wanaosadikiwa kutoka nchini Brazil.
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maliasili Zanzibar, imesema wafanyabiashara hao wamefanya hivyo kinyume na amri ya Serikali ya kupiga marufuku uingizwaji wa nyama na aina zote za ndege visiwani humu.
Kuku hao walikutwa wakiwa wamehifadhiwa katika maduka yao na wengine kwenye makontena.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, Dk. Kassim Gharib Juma, alithibitisha kukamatwa kwa wafanyabiashara hao wote wakiwa ni wenyeji wa Zanzibar.
Alisema kuku hao kwa sasa wako chini ya uangalizi wa polisi katika maduka ya wafanyabiashara hao na wengine wameamriwa kurudishwa katika nchi walikotoka.
Dk. Gharib alisema mfanyabiashara Salim Said Bakhresa, aliingiza kuku hao kupitia Dar es Salaam na ameamriwa kuwarejesha walikotoka.
’’Idara imelazimika kuchukua hatua hii ili kulinda afya za Wazanzibari kutokana na hofu ya mafua ya ndege,’’ alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha, alisema kuku wengine walikamatwa katika maduka maarufu ikiwemo Qualitu Super Market pamoja na Mombasa Mini Super Market yanayomilikiwa na wafanyabiashara wakubwa visiwani humu.
Mkurugenzi huyo alisema kuku waliokamatwa katika duka la Quality Super Market, walikuwa wamehifadhiwa katika jokofu ambapo wataalamu wa afya walishauri wafungiwe na funguo zikabidhiwe kwa polisi.
Alisema kuanzia sasa, Idara yake itafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka mbalimbali kwa vile imegundulika kwamba, kuku hao wanaingizwa kwa njia za magendo kutoka mikoa ya Tanzania bara kwa kutumia usafiri wa majahazi.
Mkurugenzi huyo alisema kuku hao wamekuwa wakiingizwa kupitia bandari ya Malindi na Pemba na kuwataka maofisa afya kuchukua hatua zaidi kudhibiti uingiaji wa kuku hao na wanyama wengine aina ya ndege.
Soko la kuku Zanzibar, linatengemea zaidi kutoka Brazil, Afrika Kusini na mikoa ya Tanzania bara kutokana na mahitaji makubwa yaliyojitokeza katika soko la sekta ya utalii Zanzibar.
Hatua hiyo imesababisha kuku kupanda bei kutoka Sh. 3,000 hadi 5,000 kutokana na soko la utalii.
Kukamatwa kwa kuku hao kumekuja siku chache baada ya Idara hiyo kuwateketeza kwa moto kuku wengine walioingiazwa Zanzibar wakitokea mkoani Tanga.