Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amemteua Dunstan Tido Mhando, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT).
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Channel Ten cha Dar es Salaam, kiliikariri Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kuwa Tido anachukua nafasi ya Samwilu Mwaffisi.
Taarifa hiyo ilisema uteuzi huo umeanza Desemba 16, mwaka huu. Kabla ya uteuzi huo Tido alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Akizungumza katika kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC jana jioni, Tido alithibitisha kwamba ameteuliwa kuongoza Taasisi ya Utangazaji Tanzania.
Tido aliwashukuru wafanyakazi wa BBC kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake wa miaka saba, akiwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC na miaka mingine kadhaa akiwa mtumishi wa kawaida wa shirika hilo.
Alisema ana matumaini kwamba atapata ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa TUT kwa kuwa wengi wao alishafanya nao kazi alipokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambapo alianzia kazi miaka ya mwisho ya 1960.
Baada ya kuondoka RTD Tido alijiunga na Sauti ya Amerika (VOA), kituo cha Nairobi nchini Kenya na baadaye alijiunga na BBC.