Takwimu zinabainisha kuwa,karibu mwanamke au msichana mmoja nchini Tanzania hufa kila saa kutokana na matatizo ya ujauzito na uzazi (kabla na baada ya kujifungua).
Katika kujaribu kukabili tatizo hilo linalotishia maisha ya akina mama wengi, serikali imeweka mikakati mbadala kuhusu kuzuia vifo au magonjwa yatokanayo na uzazi, lakini hali ni kama bado haijabadika au kuleta unafuu katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari(UTPC) ulifikia makubaliano na shirika lisilo la kiserikali liitwalo Women Dignity Project (WDP) kufanya uchunguzi ili kubaini kwa nini wanawake wanakufa wakati wa kujifungua na nini kifanyike kukabili hali hiyo.
Uchunguzi huo ulielekezwa katika mikoa mitano ya Shinyanga,Singida,Manyara,Lindi na Rukwa.
Waandishi wa habari katika mikoa hiyo kupitia klabu zao za waandishi, walipewa jukumu la kuifanya kazi hiyo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyoainishwa na WDP.
Kwa upande wa eneo la kusini, hasa katika wilaya za Lindi mjini na Lindi vijijini,waandishi waliopewa dhamana hiyo ni Felix Mwakyembe ( gazeti la Mtanzania),Utengile Ibrahim(Radio Tanzania) na Raphael Waryana(ITV/Radio One).
Waandishi hao wakitumia mbinu za utafutaji habari, walihoji watu na kufanya uchunguzi ili kupata taarifa mbalimbali muhimu.
Miongoni mwa yaliyojitokeza katika uchunguzi huo ni wanawake wajawazito hawahudhurii kliniki na wale wanaobahatika kufika kliniki ni kwamba maelekezo ya wauguzi na madaktari hawayazingatii.
Wanawake wajawazito wanaopata matatizo,hupelekwa kwa waganga wa kienyeji ambao huwatibu kwa dawa zao, ambazo hudai kuwa zitawawezesha kujifungua salama.Lakini ukweli uko bayana kuwa, wajawazito wengi wanaotumia tiba hiyo hawaponi.
Kama hiyo haitoishi, kwa mujibu wa uchunguzi huo ni kwamba,wanawake wanaojifungulia majumbani kwao wanakufa kwa sababu hawapati matunzo wanayostahili.
Wakunga na waganga wa kienyeji ni kwamba hawawezi kumudu kutibu matatizo yanayojitokeza baada ya kujifungua kama vile kutokwa na damu nyingi.
Uchunguzi katika eneo hilo, pia umebaini kuwa wanawake wengi hasa wenye kipato cha chini,wanakabiliwa na utapiamlo mkali kutokana na kula lishe duni.
Sababu nyingine zinazochangia vifo hivyo ni upungufu au ukosefu wa madaktari na wauguzi wenye sifa na utaalamu wa fani hiyo, hasa maeneo ya vijijini, uchache wao katika hospitali na zahanati ni tatizo ambalo linatakiwa kushughulikiwa kwa uzito unaostahili kama lengo ni kutaka kuyanusuru maisha ya akinamama na watoto wao.
Mkoa wa Lindi hauna madaktari bingwa wa kuhudumia akina mama hao.
Kwa upande wa vijana ambao hawazingatii ushauri wa wazazi au wakubwa wao kuhusu masuala ya kujamiiana hunywa pombe kwa wingi, kujitosa kufanya tendo la ndoa holela, na kupata mimba ambapo huishia kuitoa.
Matatizo ni mengi yanayochangia vifo hivyo,mengine ni baadhi ya wanawake hawataki kutumia vidonge vya uzazi wa majira kwa imani kuwa vinasababisha vifo kwa wanawake. Matokeo yake ni kujikuta wakifa kutokana na kubeba ujauzito muda mfupi tu baada ya kujifungua na kuhatarisha maisha yao.
Uchunguzi pia umebaini kuwa, wanawake wengi wanatumia njia za uzazi za kienyeji kama vile kufunga kamba mkononi na nyinginezo.
Wanafanya hivyo kutokana na imani waliyonayo kuwa njia hizo ni salama na zitawasaidia kuepuka kupata mimba wasizozitarajia. Hata hivyo, njia hizo zimeonekana kwa ujumla kuwa hazifai kwani zimepitwa na wakati.
Wanawake wajawazito wenye matatizo hawapelekwi haraka katika hospitali za wilaya na mikoa.
Hii inasababishwa na ukosefu wa usafiri wa kuaminika kutoka vijijini na hata wanapofika katika hospitali hizo hali huwa ni mbaya na hata kusababisha kifo cha mama mjamzito.
Halikadhalika imani za kale kwa watu wanaokawia kujifungua kwa wakati muafaka zinachangia na misimamo ya waume zao au wao wenyewe na kwamba badala ya kwenda hospitali kimbilio na tegemeo lao linakuwa tiba za kienyeji.
Sababu zipo nyingi zikiwemo rushwa, ukosefu wa elimu na miundo mbinu ya kuaminika ambayo huchangia kuwakawiza akina mama kupata huduma na kusababisha vifo vyao
Kufuatia uchunguzi huo,ilipendekezwa kuwa kunahitajika kampeni maalum ya kuielimisha jamii kuachana na mila potofu ambazo zinazuia akina mama kwenda kujifungulia kliniki na kupata uangalizi makini na wa kitaalamu.
Serikali inatakiwa kuongoza kampeni hii na wadau wote washiriki katika kuhakikisha kuwa ufanisi unapatikana.
Kama hiyo haitoshi,wakunga wa jadi na waganga wanatakiwa kupewa mafunzo maalum ya kitabibu ili kuinua uwezo wao katika kuwahudumia akina mama wajawazito kwa njia bora zaidi.
Akina mama wajawazito, wanatakiwa kushauriwa kuhudhuria kliniki kama njia mojawapo ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Pia serikali inashauriwa kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini yanakuwa na zahanati zenye vifaa muhimu na vya lazima kwa ajili ya kujifungulia akina mama.
Afisa Mradi Mwandamizi wa taasisi ya Women Dignity Project(WDP),Subila Mwambingu akizungumzia kuhusu vifo vya uzazi na magonjwa yatokanayo na uzazi kwa waandishi wa habari hivi karibuni, alisema kuwa tatizo hili, kwa namna yoyote latakiwa kuchukuliwa hatua muhimu na za makusudi katika kulidhibiti kwa sababu linaweza kuzuilika na kuokoa maisha ya akina mama na wasichana hao.
Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa kuchukuliwa katika kujaribu kukabili tatizo hili ni, kuongeza bajeti katika sekta ya afya, ili kuhakikisha kuwa huduma muhimu na za lazima zinapatikana.
Kwa mujibu wa Azimio la Abuja lililoridhiwa na nchi nyingi ni kwamba linatoa wito wa kutenga asilimia 15 ya bajeti ya taifa kwenye huduma za afya.
Katika miaka ya karibuni,Tanzania imeongeza bajeti katika sekta ya afya hadi kufikia asilimia 10.1.Pamoja na ongezeko hilo, bado kuna upungufu kufikia kiwango cha azimio la Abuja kwa asilimia 15.
Hali hii inaashiria kuwa, fedha zaidi zinahitajika kwa ajili ya kuhudumia sekta ya afya na kiasi kikubwa kiweze kuelekezwa kwenye huduma za kuzuia vifo na magonjwa yanayotokana na uzazi badala ya mkazo mkubwa kuwekwa katika kutibu tu.
Kwa namna yoyote ile,fedha zaidi zinahitajika kwa ajili ya sekta ya afya na kiasi kikubwa kiweze kuelekezwa kwenye huduma za kuzuia vifo na magonjwa yanayotokana na uzazi.
Hata hivyo, katika kutilia mkazo uimarishaji wa huduma hiyo ni kwamba, umuhimu mkubwa uelekezwe kwenye ngazi ya chini ya huduma ya afya na kwenye jamii ambayo haina huduma.
Hatua nyingine muhimu zinazotakiwa kuchukuliwa ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa akina mama wote wajawazito, bila ya kujali kama wana uwezo wa kulipia au la.
Huduma hizo, ni pamoja na zile zinazotolewa kabla ya kujifungua,wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Kulingana na utafiti wa kitaifa kuhusu masuala ya afya mwaka 2004/2005 (Tanzania Demographic and Health Survey) asilimia 40 ya wanawake walitoa taarifa kuwa,upatikanaji wa fedha kwa ajili ya matibabu ndiyo tatizo kubwa katika kupata huduma za afya.
Sera ya kitaifa inazungumzia kuhusu huduma bure kwa akina mama wajawazito. Hivyo,wanawake wasiambiwe kupeleka chochote wakati wanapokwenda kujifungua na wasitoe hongo ili waweze kupata huduma nzuri au bora.
Huduma bora zinatakiwa ziwepo au zipatikane kwa wanawake wote, hata wale wanaoishi vijijini.
Hatua nyingine muhimu zinazotakiwa kuchukuliwa ni pamoja na kupanua huduma za dharura na upasuaji kwenye kiwango cha vituo vya afya(emergency Obstetic Centre).
Huduma hizo za dharura zihakikishwe kuwa zinapatikana kwa mwanamke kati ya mmoja hadi saba kwa wanaohitaji.
Nyingine ni kupanua huduma za dharura na upasuaji kufikia kwenye ngazi ya vituo vya afya, ili wanawake wengi zaidi waweze kuzifikia wakati wa uzazi wa dharura.
Pia inatakiwa uboreshwaji mkubwa katika swala zima la kutoa rufaa kwa akina mama, ikiwa pamoja na kuboresha barabara na usafiri wa maeneo ya vijijini, ili hata wakati wa dharura wanawake waweze kuzifikia hospitali zenye huduma inayotakiwa.
Ni muhimu ikahakikishwa kuwa, wanawake wote wanasaidiwa au kuhudumiwa na wahudumu wenye ujuzi wakati wa kujifungua na si vingnevyo.
SOURCE: Nipashe