Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete jana ametimiza mwaka mmoja wa uongozi wake madarakani na leo atazungumza na makundi mbalimbali ya jamii katika kuelezea mafanikio na changamoto za serikali yake ya awamu ya nne.
Kwa mujibu wa Mwandishi Msaidizi wa Rais, Maura Mwingira, Rais Kikwete ambaye yuko Dodoma kikazi ataadhimisha kutumiza mwaka mmoja wa uongozi wake kwa kuzungumza na vikundi vya jamii mjini Dodoma.
Alisema hotuba ya Rais Kikwete itatangazwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa na Radio Tanzania Dar es Salaam.
Rais Kikwete alichaguliwa kwa kura za kishindo kwenye uchaguzi uliofanyika Desemba 14, 2005, na aliapishwa Desemba 21, 2005 katika sherehe zilizofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Serikali ya Rais Kikwete ina baraza la mawaziri 29 na naibu mawaziri 31 ambao aliwateua Januari 4, mwaka huu na aliwapishwa Januari 5, mwaka huu.
Waziri Mkuu Edward Lowassa aliteuliwa Desemba 29, 2005 na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano siku hiyo hiyo na aliapishwa rasmi Desemba 30, 2005 katika sherehe zilizofanyika Ikulu ya Chimwaga, Dodoma.
Rais Kikwete mara baada ya kuliapisha baraza lake la mawaziri alifanya ziara katika kila wizara kwa lengo la kujifunza na kueleza matarajio yake ya kiutendaji katika wizara hizo.
Kipindi cha mwaka mmoja Rais Kikwete amekwisha fanya mabadiliko ya baraza la mawaziri Oktoba , mwaka huu kwa kuwabadilisha wizara baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri.