Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Polisi aswekwa ndani kwa 'kuwaua' mbuzi wa jirani
Polisi aswekwa ndani kwa 'kuwaua' mbuzi wa jirani
By Habari Tanzania | Published  12/21/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Adai walikula mazao yake
 
RPC asema hakuna aliye juu ya sheria
 
Na Suzy Butondo, Shinyanga
 
POLISI mkoani Shinyanga inamshikilia askari wake, KonsteboAbasi, kwa tuhuma za kuwachinja mbuzi wawili na kuwajeruhi ng'ombe aliowatuhumu kula mazao shambani kwake.
 
Askari huyo aliwachinja mbuzi hao na kuwajeruhi miguu kwa panga ng'ombe wawili.
 
Tukio hilo lilitokea juzi mchana katika kijiji cha Lubaga, Kata ya Kambarage. Mifugo hiyo ni mali ya ndugu wawili Peter Ngelela na Monica Ngelela.
 
Mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo ambalo nusura lizue tafrani baada ya majirani kutaka 'kumsulubu' polisi huyo, Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Kamishna Msaidizi Simon Nyakoro, alifika eneo la tukio na kuzungumza na mmiliki wa mifugo hiyo, Monica (58) na kumuahidi kuwa sheria itachukua mkondo wake.
 
"Hakuna mtu aliye juu ya sheria, kama kweli amefanya hivyo, ni kitendo cha aibu na hakiwezi kuvumilika. Naomba radhi kwa niaba ya jeshi la polisi...hatukumtuma kufanya hili, tupe muda tunachunguza na tutachukua hatua zinazofaa," alisema Kamanda Nyakoro.
 
Alisema polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwa kuanzia imemuweka chini ya ulinzi askari huyo na itamfikisha kwenye mahakama ya kijeshi ili kujua ukweli wa jambo hilo, na akipatikana na hatia atachukuliwa hatua.
 
Aliongeza kuwa kimsingi Watanzania wote wana wajibu wa kufuata taratibu za kisheria wanapohisi kuonewa ama kunyan'ganywa haki zao, badala ya kutumia mabavu na ukatili kwa kivuli cha dola.
 
Aliwataka wakazi wa kijiji hicho kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kazi inayoendelea hivi sasa mkoani humo na Tanzania kwa ujumla, ya kupambana na uhalifu chini ya mpango shirikishi wa ulinzi baina ya jeshi hilo na raia.
 
Mapema, akitoa maelezo mbele ya Kamanda huyo, Monica alisema na wajukuu zake wawili walipokwenda kumuuliza Konstebo Abasi kwa nini amewachinja mbuzi wake, alijibu kuwa atawaua kama alivyowaua mbuzi.
 
"We bibi ni kichawi nitakuua na vifaranga vyako, na laiti ningekuwa na bunduki ninge washoot sasa hivi, hebu tawanyikeni nisije nikawamaliza," alidai bibi huyo akikariri maneno hayo mbele ya Kamanda Nyakoro.
 
Taarifa kutoka kijijini hapo, zilieleza kuwa kucha nzima wanakijiji, hususan vijana, walikesha kulinda mizoga ya mbuzi hao ili isitoweke kwa kuibiwa ama kuliwa na wanyama wa porini na kuvuruga ushahidi.
 
"Tulishampigia mwano(yowe la vita) askari huyo, bahati nzuri akakimbia na panga lake kwa kutumia baiskeli, vinginevyo ingekuwa mwisho wake," alidai kijana mmoja ambaye alionekana kuingiwa na hofu alipotakiwa na waandishi kutaja jina lake.
 
Wakizungumza, wakazi wa kijiji cha Lubuga, waliwashukuru waandishi waliofika kijijini hapo asubuhi ya siku ya pili ya tukio baada ya kuarifiwa na wanakijiji hao kwa simu ya mkononi.
 
Wakizungumzia juu ya ziara ya ghafla ya Kamanda Nyakoro kijijini hapo, walisema imewafariji kwani vinginevyo walikuwa wakilielewa vibaya jeshi hilo kuwa ndilo linalowaonyesha ubabe.
 
Wakati huohuo, polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu saba waliokamatwa katika maeneo tofauti wilayani Bukombe, wakiwa na bunduki saba aina ya magobole, zinazosadikiwa kumilikiwa na watu hao kinyume cha sheria.
 
Kamanda Nyakoro alisema silaha hizo zimepatikana kufuatia operesheni maalum inayoendelea wilayani humo, ambapo watu watatu waliofahamika baadaye kwa majina ya Ryuba Kara (45), Joseph Elias (32) na Claud Emmanuel (40), walikutwa katika pori la Mtembela kwenye maficho maalum ya majambazi, na kukamatwa.
 
Alisema polisi walifika katika pori hilo linaloungana na pori la Biharamulo, na kuwakuta ndani ya kibanda kidogo cha nyasi wakiwa na magobore matatu na guduria dogo lilokuwa na lita tatu za pombe haramu ya gongo.
 
Katika operesheni hiyo, pia watu wanne wakazi wa kijiji cha Masumbwe wilayani Bukombe, walikamatwa kufuatia kukutwa na magobore manne ambayo yanaaminika yanatumika katika vitendo vya ujambazi.
 
Waliokamatwa wametambuliwa kuwa ni Charles Ngindu (41), Omari Mabula (60), Paul Mwiguru (45) na Shija Bisengwa (30). Mwingine Kamore Nchika (45) alikutwa na baruti gramu 40.
 
Kamanda Nyakoro amewataka wananchi wenye taarifa zozote zitakazosaidia kukamatwa kwa wahalifu, hususan watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kuzifikisha taarifa hizo vituo vya polisi ili hatua za haraka zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kuwatia mbaroni watuhumiwa.
 
 

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.