Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Baada ya moto wa Magufuli kuwawakia...Mbeya wakiri uzembe
Baada ya moto wa Magufuli kuwawakia...Mbeya wakiri uzembe
By Habari Tanzania | Published  12/21/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
.Ni kuhusu sh. milioni 600 za viwanja
.RC aomba muda wajipange vizuri
 
Na Solomon Mwansele, Mbeya
 
MKOA wa Mbeya umekiri uzembe ndani ya Halmashauri ya jiji hilo, uliosababisha sh. milioni 600 za mradi wa kupima viwanja kutotumiwa ilivyokusudiwa.
 
Fedha hizo zilizotolewa na Serikali Kuu, zilikusudiwa kupima viwanja vya ujenzi wa nyumba 600 ambavyo vingeuzwa kwa wananchi.
 
Mkuu wa mkoa huo, John Mwakipesile, alikiri uzembe huo jana, ambapo alisema anakubaliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, kuwa uzembe huo umesababishwa na uongozi wa jiji, hali iliyomfanya waziri huyo kuamuru fedha hizo zirejeshwe Serikali Kuu.
 
Mwakipesile aliyasema hayo jana ofisini kwake, alipotakiwa kutoa kauli ya serikali ya mkoa kuhusu agizo la Waziri Magufuli kutaka fedha hizo zirejeshwe kwa kuwa mkoa huo umeshindwa kuzitumia.
 
Fedha hizo zilitolewa mwaka mmoja uliopita ili zitumike kuwaondolea tatizo la kupata viwanja vya ujenzi wa nyumba za kuishi wananchi, ambalo katika mikoa kadhaa ukiwemo wa Mbeya, husababisha ujenzi holela kwa watu kuvamia na kujenga maeneo yasiyoruhusiwa.
 
"Tangu asubuhi nimekuwa najaribu kumtafuta Waziri Magufuli kwa simu kuhusu suala hili, sijafanikiwa kumpata. Lakini ikishindikana, basi nitamtumia fax ili anipe muda nijue sababu zilizochangia uzembe huu kufanyika," alisema Mwakipesile.
 
Alisema pia, alizungumza na Katibu Tawala mkoani hapa, Assumpta Ndimbo na kumtaka amuandikie barua ya kumuomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Salome Sijaona, avute subira ili uongozi wa mkoa ufuatilie na
 
kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa.
 
Mbali ya hatua hizo ambazo zimechukuliwa kufuatia agizo la Magufuli, juzi, Mwakipesile alisema vile vile uongozi wa mkoa umemtuma Meya wa jiji la Mbeya, Atanas Kapunga, kwenda Dar es Salaam, kuwaelewesha watendaji wa wizara kuhusu hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa na mkoa juu ya fedha hizo ili kuwashawishi kusimamisha uamuzi wa kuzirejesha Serikali Kuu.
 
"Nimeshtushwa sana na taarifa iliyotolewa na Waziri Magufuli, kututaka turejeshe fedha hizo zote ili zipelekwe katika halmashauri nyingine" alisema Mwakipesile.
 
Alibainisha kuwa wanamuomba asichukue hizo fedha, nao watahakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa na Serikali kuu na kuongeza kuwa anamheshimu Magufuli kutokana na uchapakazi wake, na ana imani kuwa atawaelewa, na yeye (Mwakipesile) atahakikisha anaondoa uzembe uliosababisha tatizo hilo.
 
Mkuu huyo wa mkoa alisema leo atakuwa na kikao na viongozi wa jiji la Mbeya, wamueleze matatizo waliyonayo na yaliyosababisha mkoa kupata fedheha hiyo kubwa.
 
"Nawaomba wananchi wa Mbeya watulie na nitawaeleza kipi kinaendelea. Nina hakika serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, itaniamini na kuziacha fedha hizi, na mimi nitazisimamia kikamilifu kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa," alisema Mwakipesile.
 
Kuhusu wazembe watakaobanika kuwa chanzo cha tatizo hilo, alisema wataona ni nani amezembea katika utendaji au kama ni mfumo ndio uliosababisha watajua yarekebishwe vipi katika mkutano huo wa leo.
 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji, Elizabeth Munuo, alipofuatwa, alisema taarifa inayohusiana na tatizo hilo inaandaliwa na ikikamilika wataiwasilisha leo (jana) saa 6 mchana kwa mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya.
 
"Tutaijadili kwa pamoja na matokeo ya majadiliano hayo tutawajulisha nyie ikiwa ni pamoja na wananchi wote. Tafadhali tuvute subira, jambo hili ni nyeti hivyo maelezo ya kina yanahitajika," alisema Elizabeth.
 
Meya wa jiji, Kapunga alipotafutwa hakuweza kupatikana na ilidaiwa na Katibu Muhtasi wake (hakutaja jina) kuwa amesafiri nje ya mkoa kikazi na atakuwepo hapa kuanzia wiki ijayo.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.