MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Rais Jakaya Kikwete, amesema malalamiko ya rushwa katika uchaguzi ndani ya chama hicho, yamesababisha kidharaulike.
Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti huyo aliwataka wanachama wa chama hicho tawala, kuwakataa na kuwatia aibu watakaogombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chama kwa kutumia rushwa.
Alisema uchaguzi wa CCM, umekuwa ukivunjia heshima chama chao kutokana wagombea wengi kutuhumiwa kutoa rushwa kwa wajumbe ili wapate nafasi kwa kuwanunua wajumbe.
“Mara nyingi uchaguzi wa chama chetu, umekuwa ukikivunjia heshima chama kutokana na tuhuma za rushwa, wengi wamekuwa wakinunua uongozi, jamani nawaombeni uchaguzi wa mwakani uwe tofauti,” alisema.
Aliwataka wale wote wenye jitihada za kupata uongozi kwa njia ya rushwa wakataliwe na kuhakikisha wanafikishwa mahali ambako wataona aibu, ili kukiimarisha chama.
Pamoja na hayo, Kikwete alikiri kuwapo kwa udhaifu katika maeneo kadhaa ya chama chake, jambo ambalo linaweza kusababisha kiwe ombaomba.
“Kuna udhaifu katika maeneo kadhaa ya chama. Jambo hili linaweza kutusababisha siku tukiishiwa tukaomba msaada kutoka kwa mtu ambaye hana heshima katika jamii na kukidharaulisha chama,” alisema Kikwete ambaye alikuwa akizindua awamu ya tatu ya mradi wa kuimarisha chama hicho.
Alisema ili chama kiitwe chama, ni lazima kuwapo na uongozi, vikao kufanyika kwa muda unaohitajika, na kutimiza wajibu wao, mambo ambayo hayazingatiwi ipasavyo katika chama chake.
Alisema kinachotakiwa sasa ni kukiimarisha chama kwa kukijingea uwezo wa rasilimali ili kuepuka kukishushia heshima.
Mwenyekiti huyo alisema, bila ya CCM madhubuti, nchi itayumba na wanachama wakiwa dhaifu, wataanza kuyumba wao wenyewe na kufuatiwa na serikali kwa kuwa chama legelege huzaa serikali legelege, jambo ambalo kwa sasa halikubaliki kwa kuwa serikali legelege inaweza kung’olewa madarakani na wapinzani.
Katika uzinduzi huo, jumla ya wanachama 5,819 kutoka vyama mbalimbali vya upinzani walikabidhi kadi za vyama vyao kwa Rais Kikwete na kujiunga na CCM