MADAKTARI wanaomtibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Maafa), Juma Akukweti, aliyepata ajali ya ndege mjini Mbeya, wamesema anapaswa kupelekwa nchini Afrika Kusini, kwa matibabu maalumu ya majeraha ya moto.
Wamesema Akukweti anahitaji kupatiwa matibabu maalumu ambayo hayawezi kutolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Wakizungumza na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, jana aliyekwenda kumjulia hali, madaktari hao walisema wamefanikiwa kumfanyia upasuaji katika mkono wake wa kushoto ulioungua.
Walisema wameshindwa kumfanyia upasuaji kwenye mguu ulioungua kwa sababu bado kuna majereha ya moto, ambayo yanahitaji tiba maalumu ambayo haipatikani katika Hospitali ya Muhimbili.
Lowassa ambaye alitaka kujua kama tiba hiyo inahitajika kwa majeruhi wengine, walimwambia kuwa hali za majeruhi wawili zinaendelea vizuri na hawahitaji kupelekwa Afrika Kusini.
Walisema majeruhi mwingine, George Bendera, ambaye amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU), hawezi kusafirishwa kwa sababu hali yake si nzuri.
Pamoja na Waziri Akukweti, majeruhi wengine ni msaidizi wake, Nestas Kanje na rubani wa ndege hiyo ya Tanzanair, Martin Sumari.
Naye Mwandishi Wetu, Magreth Kinabo, anaripoti kuwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Philip Marmo, jana aliiwakilisha serikali kwenye mazishi ya Mkuu wa Mradi wa Uendelezaji Masoko kwa Wakulima (MSDP), Nathaniel Katinila.
Marehemu Katinila ni mmoja wa waliokuwa wamejeruhiwa katika ajali ya ndege iliyotokea mjini Mbeya, Jumapili iliyopita.
Akizungumza baada ya mazishi hayo, Marmo alisema serikali imempoteza mtumishi aliyekuwa na bidii ya kazi.
“Kazi alizozifanya marehemu ni matunda ya kujivunia, kwani alikuwa mchapakazi hodari,” alisema Marmo.
Alisema marehemu alipata mafunzo mbalimbali ya uchumi wa kilimo na uongozi ndani na nje ya nchi.
Marehemu Katinila aliajiriwa na serikali mwaka 1984, ameacha mke na watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike.
Ibada ya mazishi yake iliongozwa na Askofu Steven Mollel wa Kanisa la Pentekoste Arusha, ambaye alisema marehemu alitumia muda wake pia kwenye shughuli za kanisa.
Alizikwa jirani na kaburi la Theresia Nyantori, mwandishi wa Idara ya Habari (MAELEZO), ambaye pia alifariki dunia katika ajali ya ndege hiyo, kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.