NAIBU Waziri wa Habari na Utangazaji nchini Kenya, Koigi Wamwere, ameanzisha chama kipya nchini humo, chenye kifupisho cha CCM, akilenga kubeba ajenda zinazofanana na za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Chama hicho ambacho jina lake kamili ni Chama Cha Mwananchi (CCM) kimefanya mabadiliko kidogo katika kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.
Mbali ya ufupisho wa chama hicho kubeba jina CCM-Kenya, kaulimbiu yake inabeba ajenda ile ile ya ‘mpya’ ikisema Mwanzo Mpya, Watu Wapya na Kenya Mpya.
Katika kuonyesha namna ilivyoamua kubeba ajenda kuu ya Chama Cha Mapinduzi, CCM Kenya iliyoanzishwa Septemba mwaka huu, na baadaye kupatiwa usajili wa kudumu tayari kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao nchini humo, imeamua kutumia itikadi ya Ujamaa na Demokrasia, ikibeba sura ile ile ya Ujamaa (na Kujitegemea) ya CCM ya hapa nchini.
Hata hivyo, uamuzi wa chama hicho, kujiita chama cha kijamaa, unaweza ukakisababishia misukosuko mikubwa ya ushindani kisera, kutokana na ukweli wa kimazingira nchini Kenya, ambao kwa zaidi ya miongo minne iliyopita, umeifanya nchi hiyo kujijenga katika misingi inayokinzana na ujamaa wa CCM.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho nchini Kenya zinaeleza kwamba, tayari kimepata nakala ya Ilani na Katiba ya CCM ili baadhi ya vipengele iweze kuchukua vile vitakavyoonekana kufaa katika ilani na katiba yake.
Akizungumza na Tanzania Daima, kwa njia ya simu jana kutoka jijini Nairobi nchini Kenya, Katibu Mkuu wa chama hicho, Gammy Mwaniki alisema wameamua kuigia CCM ya Tanzania baada ya kufurahishwa na jinsi chama hicho kinavyoongoza nchi.
“Ni kweli chama chetu kina mambo mengi mazuri tuliyoiga kutoka CCM ya Tanzania. Na tunafikiria kuomba ushirikiano wa kindugu na chama hicho,” alisema Mwaniki.
Alikiri kuwa chama chake kinatumia baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye Ilani na Katiba ya CCM ya Tanzania na kuiingiza kwenye Ilani na Katiba ya CCM ya Kenya. “Yote hayo tumefanya kwa nia nzuri tu, ya kutaka kukiimarisha chama chetu kiwe imara na sifa kama CCM ya Tanzania,” alisema Mwaniki.
Mwenyekiti wa chama hicho, Wamwere, kwa sasa ndiye Naibu Waziri wa Habari na Utangazaji wa Serikali ya Rais Mwai Kibaki, ambaye ameamua kuanzisha chama hicho ili kishiriki uchaguzi mkuu ujao baada ya kuona chama tawala cha NARC kimepoteza mwelekeo na hakina uwezo wa kushinda tena uchaguzi ujao.
Wamwere pia ni Mbunge wa Jimbo la Subukia-Nakuru. Aliwahi kuishi nchini, eneo la Ilala Bungoni, Dar es Salaam toka mwaka 1978 hadi 1979.
Katika harakati za siasa za Kenya, Wamwere na mwanasiasa mwingine maarufu nchini humo, Raila Odinga; mtunzi maarufu wa vitabu vya riwaya, Ngugi Wathiong’o na Gichuki Kamau, mwaka 1982 waliwahi kukamatwa na Serikali ya Rais Daniel arap Moi (wakati huo) kwa kosa la kuandaa mpango wa kutaka kuipindua serikali. Walisota gerezani toka mwaka 1982 hadi 1984.
Mwaka 1985, Wamwere alikimbilia uhamishoni nchini Norway na alirejea mwaka 1990 kugombea ubunge kwa tiketi ya KANU. Hiki ni chama cha pili kuanzishwa na Wamwere. Mwaka 1996 alianzisha chama cha KPF kilichoshiriki uchaguzi mwaka 1997.