HALI ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Maafa), Juma Akukweti, na majeruhi wengine watatu, waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam kutokana na ajali ya ndege iliyotokea mkoani Mbeya, mwishoni mwa wiki, zinaendelea vizuri.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Ofisa Uhusiano wa Kitengo cha Mifupa (MOI), Jumaa Almasi, alisema kuwa wagonjwa wote hali zao zinaendelea vizuri.
Aliwataja wengine kuwa ni rubani wa ndege hiyo, Martin Sumari, msaidizi wa Waziri Nisetas Kanje na Ofisa Habari Kitengo cha Maafa, George Bendera, ambao wanaendelea kupata matibabu hospitalini hapo.
Viongozi mbalimbali wa kitaifa walifika kutoa pole kwa majeruhi na kuwajulia hali zao.
Waliofika hospitalini hapo, ni pamoja na Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai; Naibu Waziri wa Miundombinu, Maua Daftari na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Isidore Shirima; Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, George Waitara na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini.
Viongozi wengine ambao wameshatembelea majeruhi ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein.
Ajali hiyo ilitokea Jumamosi asubuhi wakati ndege hiyo aina ya Sesin namba 5H TZ iliposhindwa kuruka na kuanguka katika makazi ya watu eneo la magharibi ya uwanja wa ndege wa Mbeya na kuungua moto.
Katika ajali hiyo, mwandishi wa habari wa Idara ya Habari (MAELEZO), Theresia Nyantori, alifariki baada ya ndege hiyo kuanguka wakati Mratibu Mkuu wa Mpango wa Uendeshaji wa Masoko ya Mazao ya Kilimo, Nathaniel Katimila alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili