Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wazee Kawe wamwandikia Lowassa
Wazee Kawe wamwandikia Lowassa
By Habari Tanzania | Published  12/19/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda

WANANCHI wa Kata ya Kawe, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wamemwandikia barua Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wakimuomba aingilie kati mgogoro wa kuuzwa kwa eneo la Shule ya Msingi Kawe B.

Katika barua hiyo ambayo Tanzania Daima ina nakala, wazee hao wamemuomba Lowassa akutane nao kabla hali haijawa mbaya, na atoe tamko kuhusu mgogoro huo kabla madhara hayajatokea.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya Desemba 12, mwaka huu, ambayo imesainiwa na mjumbe wa kusuluhisha mgogoro huo, kwa niaba ya wananchi wa Kawe, James Riso, inaeleza kuwa, hali si nzuri baada ya kuuzwa kwa eneo la shule hiyo.

Barua hiyo inaeleza kuwa, wananchi wamefikia uamuzi wa kuiandika, baada ya Naibu Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rita Mlaki, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe na mwenzake wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani, kushindwa kuhudhuria mkutano wa hadhara, walioalikwa ili kwenda kuona hali halisi ya mgogoro huo.

Inaeleza barua hiyo kuwa, wananchi wana hasira, baada ya Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, kuvamia mkutano ulioitishwa na wananchi kujadili mustakabali wa eneo hilo pamoja na kuwaonyesha viongozi hao madhara ya kuuzwa kwa sehemu ya kiwanja cha shule hiyo.

Inaeleza kuwa, Londa akiwa na kikundi cha watu, waliwasili kwenye eneo la mkutano na kutupiana maneno na Mwenyekiti wa kikao hicho, James Riso, na kuamsha hasira miongoni mwa wananchi na kusababisha mkutano huo kuahirishwa.

“Hali halisi ya kiwanja namba 696. Kuna shule mbili za msingi Kawe B na Ukwamani, sekondari mbili moja ya wananchi na nyingine ni ya mtu binafsi… hatujui katika shule mbili za sekondari ipi isiyokuwa na hati.

“Madhara yaliyojitokeza baada ya ugawanywaji wa kiwanja namba 969, ni kuwa msingi wa shule ya wananchi na chumba cha maabara imechukuliwa pamoja na viwanja vya michezo.

“Mafuriko ya maji kuingia madarasani ni jambo la kawaida kutokana na uzio wa matofali, hakuna eneo la kuongezea madarasa ya kidato cha tatu na cha nne na hakuna sehemu ya wanafunzi kukutana kwa pamoja,” anaeleza sehemu ya barua hiyo.

Sehemu nyingine ya barua hiyo inaeleza kuwa, waliohusika na njama za kugawa eneo la shule hiyo bila kuishirikisha Kamati ya Shule, walikwenda kwenye eneo la shule peke yao, na kudai kuwa lina ukubwa wa ekari 17 na hakuna madhara yoyote yanayoweza kutokea kutokana na kuuzwa eneo hilo.

Inazitaja hatua zilizochukuliwa na wananchi kutatua tatizo hilo kuwa ni kumwalika Londa ambaye alisema hakubaliani na ujenzi wa ukuta huo na ni lazima ubomolewe.

Inasema Londa alisimamia uchaguzi wa wajumbe sita wa kuungana na Kamati ya Maendeleo ya Kata kutafuta ufumbuzi wa utata wa kuuzwa kwa eneo hilo.

Hatua nyingine ni wananchi kumuomba Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro kufika shuleni hapo kuzungumza na wazazi, lakini hakuweza kufika, wananchi kufikisha malalamiko yao bungeni kupitia Mbunge wa Viti Maalumu Halima Mdee, CHADEMA ambapo serikali haikutoa jibu la kuridhisha.

Inazitaja hatua nyingine kuwa ni wananchi kuitisha mkutano wa hadhara na kumwalika Naibu Waziri Kombani na Mlaki ili kwenda kujionea hali halisi, hata hivyo mawaziri hao hawakuhudhuria licha ya kupelekewa barua za mwaliko.

Mmoja wa watu waliopeleka barua hiyo, Albert Millinga, alilithibitishia gazeti hili kuwa, barua hiyo ilipokelewa na wasaidizi wa Lowassa na waliahidi kuiwasilisha. Wametakiwa wafike leo, kujua hatua zilizochukuliwa na Lowassa kuhusu mgogoro huo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.