Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  ‘Mke wangu kafa shujaa ajali ya ndege Mbeya’
‘Mke wangu kafa shujaa ajali ya ndege Mbeya’
By Habari Tanzania | Published  12/19/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Magreth Kinabo

MUME wa mwandishi wa habari wa Idara ya Habari (MAELEZO), Theresia Nyantori, aliyefariki dunia katika ajali ya ndege iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Mbeya, amesema kuwa mke wake amekufa kishujaa.

Akizungumza baada ya mazishi ya mkewe yaliyofanyika jana katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Abraham Nyantori, ambaye ni Ofisa wa Habari katika idara hiyo hiyo, alisema mara baada ya kupata taarifa ya msiba, hakuamini kuwa mkewe mpenzi amefariki dunia.

“Ninawashukuru wale wote walionifariji kwa kunipa Neno la Bwana. Sasa nimeamini kuwa mke wangu bado niko naye kiroho, lakini kimwili siko naye. Mke wangu amefariki kishujaa, kwani baada ya kumaliza kazi ya kupiga picha alizotumwa na ofisi, alizituma katika vyombo mbalimbali vya habari na zikatumika siku iliyofuata.

“Ninapenda kuahidi mbele ya umma uliopo hapa kuwa, nitalitumikia taifa kwa uaminifu na utii kama mke wangu, baada kumaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma,” alisema.

Nyantori, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), kilichoko Nyegezi, Mwanza, alisema kuwa, atamkumbuka mkewe kwa ushujaa wake na akawataka watu kuondokana na dhana kwamba mashujaa ni wanasiasa pekee.

“Mashujaa si wana siasa tu, hata sisi watu wa chini tunaweza kuwa mashujaa,” alisisitiza Nyantori, aliyeonekana kuwa mnyonge na mwenye majonzi mengi.

Alisema marehemu mkewe alikuwa mchapakazi hodari, ambapo anakumbuka katika semina elekezi iliyofanyika Ngurdoto, aliweza kupiga picha za mawaziri wote na wakurugenzi wote, pasipo msaada na zilitumika, kwa kiwango cha kumshangaza hata Mkurugenzi wake, Kassim Mpenda.

Alisema kuwa, alikuwa anaishi na mke kama mtu na rafiki yake, hata wafanyakazi wenzake na watu wengine wanaowafahamu, ni mashahidi kwa hilo, na ana ushahidi wa ujumbe mfupi wa simu walizokuwa wakitumiana za utani na kikazi mara kwa mara.

Umati wa watu ulifurika nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho, wakiwamo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Mwili wa marehemu uliwasili nyumbani kwake Changanyikeni majira ya saa 7:30, na kupokewa na mamia ya waombolezaji, wakiwamo wafanyakazi wenzake, viongozi wa serikali na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya umma na binafsi.

Ilipofika saa 8: 20 mchana, Rais Jakaya Kikwete akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Daniel Nsanzugwanko na viongozi wengine, aliwasili.

Kikwete alipowasili katika eneo la msiba, alikwenda moja kwa moja ndani kutoa pole kwa wafiwa kabla ya kuwaongoza waombolezaji kuanza kuaga mwili wa marehemu.

Baadhi ya wanahabari, marafiki na wafanyakazi wenzake marehemu, walilazimika kupatiwa msaada wa kubebwa kutokana na kuishiwa nguvu kila walipokuwa wakipita mbele ya mwili wa marehemu kutoa heshima za mwisho.

Naye Katibu wa Chama cha Wapiga picha wa Tanzania, Suleiman Mpochi, alisema kifo hicho ni pigo kwa chama hicho, kwa vile marehemu alikuwa hana uchoyo na alipenda kutoa msaada wa kimaadili na kikazi.

“Baada ya kututumia picha alizopiga akiwa Mbeya, marehemu alituandikia ujumbe wa maneno kutoka katika simu yake, akitueleza kuwa nawatakieni kazi njema,” alisema Mpochi na kuwaacha waombolezaji kububujikwa machozi.

Viongozi wengine waliofika nyumbani kwa marehemu ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli na mke wa Waziri Mkuu, Regina Lowassa.

Ibada ya kumuaga marehemu iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri kutoka Junior Seminari ya Kisarawe, Crisstosila Karata, ambaye ni ndugu wa marehemu, ambaye pia alimwelezea Theresia kuwa alikuwa mchapakazi mahiri.

Baadhi ya wafanyakazi wenzake walimwelezea marehemu kuwa alikuwa mtu aliyekuwa akijituma, asiyechagua kazi na aliyekuwa tayari kufanya kazi katika mazingira yoyote bila ubishi.

Wakirejea uhusiano wake na mumewe, walisema watu hao wawili walikuwa wakiishi kama mapacha, kwani Theresia alikuwa hawezi kwenda kula pasipo kumtaarifu mumewe, ambaye wamekuwa wakifanya kazi katika ofisi moja.

Marehemu Theresia hadi mauti yanamfika, alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili akisomea Shahada ya Sanaa (B.A) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, na alikuwa akitarajia kuhitimu mwakani.

Theresia alifariki dunia katika ajali ya ndege ndogo iliyotokea Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita, ambayo pamoja naye ilisababisha kifo cha ofisa mwingine wa serikali, Nathanieli Katimila, ambaye alikuwa Mratibu Mkuu wa Mpango wa Uendelezaji wa Masoko ya Kilimo.

Katika ajali hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Juma Akukweti, alijeruhiwa na hivi sasa yeye na majeruhi wengine watatu wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wakiuguza majeraha ya ajali hiyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.