Na Peter Katulanda, Mwanza
MIPANGO "inasukwa" ya kuandaa cheti bandia ili mtuhumiwa anayekabiliwa na tuhuma za mauaji, aachiwe huru kwa madai aliwahi kuugua kichaa na kutibiwa nchi jirani.
Imebainika kuwa mipango hiyo, inaandaliwa nchini Kenya kufuatia njama za kumtorosha, kumnusuru na kesi ya mauaji inayomkabili kugonga mwamba, baada ya polisi kugundua na kuimarisha ulinzi wa mahabusu wanaopelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa habari za kuaminika kutoka ndani ya familia ya mtuhumiwa huyo anayedaiwa kuwa siyo raia wa Tanzania, nduguze wawili hivi sasa "wanahaha" katika mojawapo ya hospitali nchini humo, kughushi cheti cha kumuonyesha mshitakiwa aliwahi kuugua kichaa.
Habari hizo zimedai ndugu zake hao wenye asili ya Kisomali, mwishoni mwa Novemba mwaka huu, walikuwa Mwanza wakifanya mikakati ya kumtorosha mtuhumiwa huyo, lakini hawakufaulu baada ya mpango wao kuvuja.
"Waliambiwa hawataweza kumtoa ndugu yao mikononi mwa vyombo vya dola kirahisi, hata kama ni kwa nguvu, wakashauriwa warudi kuandaa cheti cha hospitali
ambacho daktari atathibitisha kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kuugua kichaa miaka iliyopita kabla ya kuua," kilieleza chanzo cha habari kutoka ndani ya familia hiyo.
Jumapili iliyopita gazeti la MZALENDO liliandika kwamba Mkoa wa Mwanza umegundua njama za kutaka kuwatorosha baadhi ya mahabusu hatari
wanaohusishwa na makosa ya ujambazi na mauaji, wanaoshikiliwa gerezani, ambazo zinadaiwa kufanywa na watu wasiojulikana.
Kufuatia kubainika kwa njama hizo, polisi iliimarisha ulinzi kwa mahabusu katika mahakama na kutoruhusu ndugu zao kuwasogelea.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, mahabusu mmoja mwenye asili ya Kisomali, baada ya kusomewa shitaka na kurudishwa katika benchi mahakamani hapo, alionekana akitoa simu mfukoni na kuwasiliana na ndugu zake kwa kuandikiana ujumbe.
Kitendo hicho kilisababisha manung'uniko miongoni mwa polisi waliokuwa wakiwalinda mahabusu hao, ambao walisikika wakilalama kuwa inakuwaje mahabusu anakuwa huru kuwasiliana kwa simu wakati tayari kuna habari za baadhi yao kutaka kutoroshwa.