.Akukweti azugumza na JK
.Dk. Sheni, Kawawa, Mwinyi wawajulia hali majeruhi
Na Esther Katua
MMOJA wa majeruhi wa ajali ya ndege iliyotokea Jumamosi iliyopita jijini Mbeya, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Marehemu alikuwa ni Mratibu wa Mradi wa Masoko wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (AMSDP), Katimula Nathaniel (42).
Kifo hicho kimeongeza idadi ya waliokufa katika ajali hiyo kufikia wawili, baada ya mpiga picha wa Idara ya Habari (MAELEZO), Theresia Nyantori, kufariki dunia papo hapo ajali ilipotokea.
Hali za majeruhi wengine wa ajali hiyo akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Juma Akukweti, zilielezwa kuwa zinaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa madaktari wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) cha hospitali ya Muhimbili, Nathaniel alifariki saa 6 usiku, na alikuwa amelazwa na majeruhi mwingine ambaye ni ofisa katika kitengo cha maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, George Bendera.
Hali ya Bendera bado ni mbaya kulinganisha na majeruhi wengine waliolazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwenye taasisi hiyo, Waziri Akukweti alisema anamshukuru Mungu anajisikia nafuu licha ya kuwa na maumivu makali kutokana na majeraha aliyoyapata.
Ameishukuru serikali kwa kuwapelekea ndege iliyowasafirisha kuwatoa Mbeya hadi Dar es Salaam, kwa matibabu zaidi katika Hosptali ya Taifa Muhimbili.
Mkewe, Aniseta Akukweti, alisema hali ya mumewe inaendelea vizuri ikilinganishwsa na juzi.
Mke wa rubani wa ndege iliyopata ajali mali ya kampuni ya TanzanAir, Martin Sumari, Gladness Sumari, alisema hali ya mumewe imeimarika kiasi.
Gladness alisema kabla ya ajali hiyo aliwasiliana na mumewe aliyemwambia asingeweza kusafiri siku moja kabla ajali kutokana na hali mbaya ya hewa, na kuongeza kuwa asubuhi ya siku iliyofuata alimpigia simu kumwarifu kuwa angesafiri asubuhi kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam.
Alisema muda mchache baadaye aliarifiwa na wanafanyakazi wa TanzanAir kuwa mumewe alikuwa amepata ajali.
Aliongeza kuwa hali aliyokuwa nayo mumewe kwa sasa ni nafuu na kuongeza kuwa hii ni ajali ya pili ya ndege kwa mumewe, baada ya ajali ya kwanza iliyotokea mwaka 1994 wakati akiwa rubani wa JWTZ ambapo ndege ilianguka na kulipuka eneo la mjini Bukoba. Sumari ni mstaafu wa JWTZ na mwajiriwa wa TanzanAir.
Akizungumza kwenye wodi ya MOI, majeruhi mwingine, Katibu wa Waziri, Nestas Kanje, alisema anaendela vizuri na kuwa ana maumivu makali kwenye mbavu na mkono wa kushoto.
Wakati huo huo Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Sheni, kwa nyakati tofauti jana waliwatembelea majeruhi hao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wengine waliowatembelea majeruhi hao ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Mzee Rashidi Kawawa.
Akizungumza na Rais, Waziri Akukweti alisema hakumbuki nini kilitokea zaidi ya kukumbuka kuwa ndege ilipaa.
"Ninachokumbuka ndege ilipaa, baada ya hapo sielewi kilichotokea. Wakati nikiwa hospitali nilikuwa nikiulizia hali za wenzangu zinaendeleaje, hakuna mtu aliyeweza kunieleza ukweli zaidi ya kusema wako salama," alisema.
Rais ambaye alikuwa amefuatana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alitoa pole kwa majeruhi hao.
Rais alisema amesikitishwa na tukio hilo lililosababisha sio tu majeruhi, bali vifo vya watu wawili.
" Nimesikitishwa sana na ajali hii, yote yaliyotokea pamoja na kupotea kwa maisha ya watu wawili ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Natoa pole zangu kwa familia za marehemu na Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, nawatakia kila la kheri mpone haraka", alisema Rais Kikwete.
Alisema awali serikali ilitaka kutumia ndege yake aina ya FOKKER 28, ambayo mwendo wake ni wa kasi kuwawahisha majeruhi hao na mwili wa mwandishi wa habari, Theresia, aliyefariki juzi katika ajali hiyo, lakini ikagundulika milango ya ndege hiyo ni midogo.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali iliamua kukodi ndege ya Kahama Gold Mine ambayo milango yake ni mipana kuweza kuwaingiza majeruhi na mwili wa marehemu, kuwawahisha Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea juzi asubuhi muda mfupi baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Songwe jijini Mbeya.
Majeruhi kwa nyakati tofauti waliwashukuru madaktari, wauguzi wa Hospitali ya Rufani Mbeya na wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na wengine wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kuokoa maisha yao.
Waziri Akukweti na ujumbe wake walikwenda Mbeya kutoa pole na kujionea kuungua kwa soko la Mwanjelwa kulikotokea mapema wiki iliyopita.
Akiwa Muhimbili Makamu wa Rais, Dk. Sheni, pia alimjulia hali Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Issa Mohammed, ambaye amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi katika hospitali hiyo.
Naye Solomon Mwansele anaripoti kutoka Mbeya kwamba,wataalamu kutoka Dar es Salaam, jana walishindawakifanya uchunguzi kujua chanzo chaajali ya ndege hiyo.
Eneo la ajali limezungushiwa utepe wa njano kuzuia watu kupita huku askari mwenye silaha akililinda pamoja na mabaki ya ndege.
Wamiliki wa nyumba zilizoangukiwa na ndege hiyo, walisema wamepata kutokana na nyumba zao kuharibiwa vibaya.
Ashura Mwangupile (35) alisema jana alilalanje na kunyeshewa na mvua akiwa na wanae wannekutokana na nyumba yao kuharibiwa vibaya na kuta zotekuwa na nyufa hali iliyosababisha waogope kulala ndani.
Alisema vyumba vyote vya nyumba yakevimebomoka, mito ya makochi imeungua, televisheni, redio, mita yaumeme na vyombo mbalimbali vya ndani vimevunjika.
"Sisi tulikuwa tumelala natukasikia mngurumo mkubwa wakati ndege inakwangua mabati na pia moshi mzito ulitanda ndani ya vyumbavyote," alisema Ashura.
Aliongeza kuwa, alimka na kufanikiwakuwaokoa watoto vyumbani mwao.
"Sasa kwa leo hatuelewi tutalalawapi kwani kulala ndani tunaogopa kutokana na kuta zote kuwa na nyufa..." alisema Ashura.
Naye mmiliki mwingine wa nyumba ambayo ndege ndiyo ilipoangukia, Willbald Venge (61), alisema hasara aliyoipata kutokana na ajali hiyo ni sh.milioni tatu.
Venge alisema geti kubwa limeungua, mlango mmoja umeharibika, kanopi na grili zilizokuwepo katika kanopi ziling'olewa na ndege hiyo.
"Wakati ndege inaanguka, nilikuwepo ndani na wanangu, na nguvu ya ndege ile ilimalizikia kwenye kanopi ya nyumba yangu na baadaye kuanguka chini na kuanza kuwaka moto," alisema.
Venge alisema wataalamu waliokuwa wanachunguza ajali hiyo walishinda eneo hilo, na waliondoka saa 9 alasiri.
"Nawashukuru sana majirani zangu kwani ndege ilipoanguka wao alichukua maji pamoja na mchanga na kuanza kuuzima moto na bila wao nadhani nyumba yangu nayo ingeteketea kwa moto huo," alisema Venge.