ARI, Nguvu na Kasi mpya ya Serikali ya Awamu ya Nne sasa imeelekezwa katika Wizara ya Miundombinu, kutokana na kashfa inayosemekana kuwamo katika wakala ulioundwa wa Umeme na Ufundi (TEMESA).
TEMESA iliundwa chini ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli, mwaka jana, lengo likiwa ni kuipunguzia serikali mzigo. Awali ilikuwa idara ndani ya wizara hiyo, na kutokana na utendaji mbovu, ilishafikiriwa kuvunjwa, lakini ikatetewa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, Ari mpya imefikia uamuzi wa kuvunja wakala huo mwakani, baada ya kufanyika tathmini inayoonyesha kwamba unafanya kazi chini ya kiwango na kufanya biashara kwa hasara, hivyo kutokuwa na maana kwa serikali.
TEMESA ni wakala wa tatu ndani ya wizara hiyo, baada ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambao sasa uko katika tathmini za kuangalia nyumba zilizouzwa, zinazotakiwa kurejeshwa serikalini na wakala mwingine ni TANROADS, unaoshughulikia barabara.
TEMESA ilitakiwa ijiendeshe kwa kujitegemea kupitia miradi mbalimbali na vyanzo vingine vya mapato, lakini yote hayo yameonekana kuwa ni kazi bure, kwa kuwa kinachoonekana katika rekodi ni hasara tupu.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Wizara ya Miundombinu zinasema muda wa uangalizi umemalizika na ripoti ya kamati ya tathmini inaonyesha kuwa TEMESA sasa inatakiwa kuvunjwa kwa mujibu wa sheria, wala haitaongezewa muda kama ambavyo baadhi wangependa.
Chanzo cha habari kiliiambia Tanzania Daima kuwa baada ya kuzinduliwa wakala huo ulikabidhiwa miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa vivuko vyote nchini, magari aina ya Mercedes Benz kwa ajili ya kukodisha, masuala ya umeme katika majengo ya serikali na karakana ya serikali iliyopo eneo la Vingunguti, Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutoandikwa gazetini, mmoja wa maofisa wa ngazi za juu katika wizara hiyo alikiri kuwapo utendaji mbovu katika TEMESA na kwamba kwa mujibu wa sheria inatakiwa kuvunjwa.
“Ni kweli ripoti inaonyesha kuwa hawakufikia lengo lililokusudiwa na kama aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara, John Kijazi alivyosema wakati wa uzinduzi, isipofikia lengo ivunjwe…huo ndio utekelezaji utakaofuata,” alisema.
Kati ya miradi iliyokabidhiwa kwa TEMESA na kuendeshwa kinyume cha utaratibu na kwa masilahi binafsi ni ule wa magari ya kukodi aina ya Mercedes Benz, yenye namba za serikali STJ na STK.
Inaelezwa kwamba, baadhi ya maofisa wameanza kutumia magari hayo kinyume cha taratibu, ikiwa ni pamoja na kuyatumia kwa shughuli zao binafsi, huku wakiegesha magari yao ya kawaida (kama vile Pick Up) na kustarehe na hayo waliyotakiwa wayakodishe.
“Yale magari sasa yameshuka hadhi, kwani wameanza kuyatumia tofauti na ilivyokusudiwa. Sasa yamekuwa ya kutembelea, hawataki tena kutembelea magari yao ya awali ya Pick Up Double Cabin.
“Si kwamba hatujaliona hilo, tumeshaongea mpaka sasa tumeamua kuwaacha wafanye wanavyotaka, kwa kuwa wanaona kuwa wao wana maamuzi ya mwisho na huwa hawataki kushauriwa,” alisema ofisa huyo.
Mmoja wa madereva wanaoyaendesha magari hayo aliiambia Tanzania Daima kuwa sasa hivi magari hayo hayana hadhi kama awali, kwa kuwa yamekuwa yakitembelewa na vigogo wa TEMESA kama watakavyo na mengi sasa ni mabovu.
“Sisi haituumi, kwa kuwa tunafurahia kuendesha magari ya kifahari, lakini ukweli ni kwamba kwa sasa hayaingizi fedha kabisa. Ni kufanya kazi za mabosi na familia zao, yaani yanakuwa kama school bus (kama mabasi yanayopeleka na kurudisha watoto shule).
“Baadhi ya vigogo wanaozurura na magari hayo ni … pamoja na baadhi ya wahasibu, wahandisi, inategemea na ukaribu wao na bosi wao,” alisema mmoja wa wafanyakazi.
Mradi mwingine ni ule wa vivuko, ambapo kumekuwa na ubabaishaji wa hali ya juu kwa kufanya maamuzi bila kufuata ushauri wa kitaalamu, hivyo wananchi kubaki katika matatizo makubwa ya kuvuka maeneo husika.
“Mbali na vivuko vya mv Alina na mv Kigamboni ambavyo ni maarufu kwa Watanzania kwa sababu ya matatizo yake, kuna vivuko vingine ambavyo wameshindwa kuvitafutia ufumbuzi, kama kivuko cha Kilombero na cha huko Mto Rufiji,” alibainisha ofisa mwandamizi wizarani.
Mwingine alisema kwamba, pamoja na kuwapo matatizo ya vivuko mara kwa mara, uongozi wa TEMESA ulipaswa kutembelea na kukagua mara kwa mara, lakini hawaonekani, wanaonekana kuwa na shughuli nyingine na kuwatuma huko maofisa wa chini, hivyo matatizo kuendelea.
Mradi mwingine ni ufundi wa umeme katika majengo ya serikali, ambapo pia kumekuwa na ubabaishaji, ikiwa ni pamoja na mradi wa ufundi wa magari ambapo kwa sasa wamepoteza wateja kutokana na kuwa na kauli mbaya zinazowakera wateja na ucheleweshwaji wa kazi za wateja hao.
“Kwa upande wa kauli mbaya kwa wageni wanaokuja kupata huduma, hilo lipo lakini sijui wanajiamini nini, kwani wakiwa wanawajibu vibaya hufanya hivyo kwa sauti mpaka sisi tunasikia huku nje na mteja akitoka anakuwa amejiinamia, inakuwa kama ni ofisi ya mtu binafsi na si ya serikali,” alisema mmoja wa wafanyakazi.
Mbali na wakala huo kufanya kazi chini ya kiwango, unashutumiwa kwa kutowalipa kabisa, au kuwacheleweshea malipo wafanyabiashara wanaowauzia vipuri vya magari na mitambo mbalimbali kwa kutowalipa fedha kwa wakati, kwa sababu binafsi.
Baadhi ya wafanyabiashara ambao wanadai TEMESA waliiambia Tanzania Daima kuwa wamekuwa wakizungushwa bila sababu za msingi na wakati mwingine hutakiwa ‘kuongea vizuri,’ ili wapate haki zao haraka.
“Utakuta jina limetoka na file (jalada) linaonyesha nimepitishwa na ninastahili kulipwa, lakini wakati ukifika hakuna malipo. Mara unaambiwa limepotea, na wanalipana kiuswahiba, kwa kifupi haki hakuna,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao