Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waziri Akukweti aanguka na ndege
Waziri Akukweti aanguka na ndege
By Habari Tanzania | Published  12/17/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Christopher Nyenyembe na Happiness Katabazi

ZIARA ya kukagua maafa yaliyolikuta Soko la Mwanjelwa lililoungua na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi, imemalizika kwa balaa la ndege kuanguka, kuua mtu na kujeruhi wengine, akiwamo Waziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Kama siku njema huonekana asubuhi, basi na siku mbaya nayo pia huwa hivyo hivyo, kwa sababu jana asubuhi saa 12.40 hivi, ndege ya Tanzanair, iliyokuwa imembeba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Juma Jamaldin Akukweti, ilishindwa kupaa angani na kuanguka.

Akukweti na ujumbe wake, walikuwa ndio wamepanda ndege hiyo baada ya kazi iliyowapeleka Mbeya kumalizika juzi Ijumaa, na walikuwa wakirejea Dar es Salaam, bila shaka wangepata mapumziko ya mwisho wa wiki, kisha Jumatatu kuanza tena kazi.

Lakini haikuwa hivyo, kwani ndege hiyo aina ya Sesin namba 5H TZ iliyokuwa ikirushwa na rubani Martin Sumari, ilishindwa kuruka hadi usawa unaotakiwa kwa ajili ya kujiweka sawa angani, ikaangukia makazi ya watu, eneo la magharibi ya Uwanja wa Ndege wa Mbeya.

Katika ajali hiyo, ambayo ndege ilisambaratika vipande vipande, Ofisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Teddy (Theresia Richard) Nyantori alikufa papo hapo.

Majeruhi wengine katika ndege hiyo, ni pamoja na rubani Sumari, Msaidizi wa Waziri wa Nchi, Nisetas Kanje, Ofisa Habari katika Ofisi ya Waziri Mkuu, George Bendera na Mratibu wa Programu ya Uendelezaji Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo (AMSDP).

Habari ambazo Tanzania Daima ilizipata ni kwamba, wakati Waziri wa Nchi akiondoka, hapakuwa na kiongozi yeyote uwanjani hapo, lakini baadhi walifika baada ya taarifa za kutokea kwa ajali hiyo.

Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema kwamba, ndege hiyo ilianguka mara ilipoanza kuruka na kisha kuwaka moto, ambao hata hivyo ulizimwa na wananchi, wakazi wa eneo ilipoangukia.

Alois Chaula, aliiambia Tanzania Daima kwamba, wakati akipita eneo hilo la Uwanja wa Ndege, aliona magari mawili eneo la kuegesha magari uwanjani hapo na baadaye kidogo akaiona ndege hiyo ikijiandaa kuruka ikitokea mashariki ya uwanja.

“Ilipoanza kuruka, ilionekana wazi haina nguvu, ilimaliza kiwanja kabla haijaruka angani, ilianza kupaa ikiwa eneo la nyasi, haikufika mbali, niliona tairi zake zikikanyaga paa za nyumba na kisha vikafuata vishindo vikubwa vitatu, moto ukalipuka… wananchi waliwahi kuuzima, Zimamoto wamefika wakati tumemaliza kazi ya kuzima moto,” alisema Chaula.

Mkazi wa eneo ilipoangukia ndege hiyo, Bruno Swali, alisema kuwa, walisikia vishindo kwenye mapaa ya nyumba zao na walipotoka, wakakuta moto unawaka ndipo walipoenda kuuzima na kuwakimbiza abiria Hospitali ya Rufaa Mbeya.

“Mimi ndiye niliyewakimbiza majeruhi hawa hospitali, walikuwa wameungua vibaya, dada mmoja huyo nina uhakika amefariki kwani hata wakati tunamtoa kutoka kwenye ndege, alikuwa anaonyesha kuwa tayari amefariki, nilikimbiza hospitali majeruhi wawili, mwingine wanasema ni waziri, sijui,” alisema Swali.

Wananchi walioshiriki kuwaokoa abiria hao walidai kuwa, walipowafuata askari wa Kikosi cha Zimamoto uwanjani hapo, waligoma kukimbiza majeruhi hospitali na hivyo kuamua kutumia teksi, ikiwamo moja yenye namba za usajili T 175 AEL iliyokuwa ikiendeshwa na Danford Kambole.

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mbeya, John Mwakipesile, alipofika hospitali, kati ya majeruhi wote ni Waziri Akukweti pekee aliyeweza angalau kuzungumza. Wakati huo alikuwa akiandaliwa kwa ajili ya kupelekwa chumba cha upasuaji. Akampatia RC majina ya watu alioomba wataarifiwe juu ya yaliyompata.

Ndege hiyo ya Tanzanair ilivunjika vipande vipande, na vilikuwa vimesambaa eneo ilipoangukia, huku injini yake nayo ikiwa peke yake.

Katika ajali hiyo, nyumba tatu zimeharibiwa vibaya mapaa yake pamoja na samani, lakini hadi jana mchana hapakuwa na taarifa za wakazi wa eneo ilipoangukia kudhurika.

Taarifa iliyotolewa jana mchana na MAELEZO jijini Dar es Salaam, ilisema kwamba, Nyantori (41) alizaliwa Agosti 26, 1965 wilayani Moshi Vijijini. Baada ya kuhitimu masomo yake ya elimu ya msingi na sekondari, alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ) alikosoma kati ya mwaka 1988 na 1990 na kujipatia Diploma ya Uandishi wa Habari.

Aliajiriwa MAELEZO kama Ofisa Habari Msaidizi Mei 1990 na ilipofika Desemba mwaka huo huo, Theresia alifunga ndoa na Abraham Nyantori. Juni 28, 1992, yeye na mume wake walihamishiwa Mwanza.

Januari 2002, Teddy na mumewe walipata uhamisho kurejea Dar es Salaam, Teddy akiwa na cheo cha Ofisa Habari Msaidizi Mwandamizi na hadi mauti yanamkuta, alikuwa ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT). Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.