Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Walimu sasa kulipwa mishahara tarehe 23
Walimu sasa kulipwa mishahara tarehe 23
By Habari Tanzania | Published  12/16/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Magreth Kinabo

SERIKALI imekubaliana na benki ya National Microfinance (NMB) kutoa malipo ya mishahara ya watumishi wote wa halmashauri za wilaya ifikapo tarehe 23 ya kila mwisho wa mwezi, badala ya tarehe 25.

Uamuzi huo ambao utawanufaisha hasa walimu wa shule za msingi, utakaoanza kutekelezwa mwezi huu, ulitangazwa jana na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Waziri Meghji alisema, hatua hiyo imetokana na semina elekezi juu ya utaratibu wa ulipaji mishahara ya watumishi hao, iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumanne wiki hii.

Alisema semina hiyo iliwashirikisha wadau wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Menejimenti na Utumishi wa Umma, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na wakurungenzi wote watendaji wa wilaya.

“Hii imetokana na matatizo makubwa ya ucheweleshaji wa ulipaji wa mishahara ya watumishi hao, hasa wengi walio katika kundi hilo ni walimu na wafanyakazi wa sekta ya afya.

“Serikali imeamua kutafuta njia nafuu ya kutatua tatizo hilo, ambapo imekubalina na benki ya NMB kulipa mishahara ya watumishi hao, hata kama fedha haijaingia kwenye benki hiyo toka kwa waajiri tarehe 23 ya kila mwisho wa mwezi.

“Uamuzi wa makubaliano haya umefikiwa baada ya agizo la serikali la kisheria la kutaka kuwa mishahara ya watumishi hao, ilipwe tarehe 25 ya kila mwisho wa mwezi, lakini bado tatizo hilo, lilikuwa halijapatiwa ufumbuzi,” alisema Waziri Meghji.

Alisema tatizo hilo ni kubwa, hasa kwa watumishi ambao ni walimu wa shule za msingi na wafanyakazi wa sekta ya afya waliokuwa hawapati mishahara hiyo kwa wakati.

Aliongezea kuwa, utaratibu huo utawanufaisha kwanza walimu wa shule za msingi, lakini wa shule za sekondari utafuata baadaye, kwa kuwa wao bado wanatumia utaratibu tofauti wa kulipa mishahara na wa shule za msingi.

“Hakuna sababu ya kuchelewesha mishahara hiyo kwa kuwa, fedha zinazotumika kuwalipa zinatoka kwenye bajeti ya serikali,” alisisitiza Meghji.

Alisema serikali imeamua kubadilisha mfumo wa kuchukua payroll kutoka Hazina Makao Makuu kwa kuwa umepitwa na wakati.

Sababu nyingine ni waajiri kuchelewa kuipeleka NMB, huku baadhi yao kutowajibika ipasavyo kwa kuchukua muda mwingi wa kuhakiki malipo ya mishahara.

Alisema serikali imekubaliana na benki ya NMB kuboresha huduma ya malipo ya mishahara hiyo ili kuweza kufanikisha azma ya kuwalipa wafanyakazi hao mapema.

Waziri Meghji alisema, benki ya NMB itafungua vituo vya malipo ya mishahara nje ya makao makuu ya wilaya ili kuwezesha ulipaji huo.

Katika kutekeleza hilo, jukumu la serikali na halmashauri za wilaya, ni kuainisha maeneo ambayo ofisi hizo zitafunguliwa kwa kuzingatia wingi wa watumishi.

Alisema NMB itasaidia kufungua akaunti benki hata kama mtumishi husika hana fedha za kufungua akaunti hiyo, na itaanzisha mfumo ya utoaji taarifa ya mshahara kuingia kwenye akaunti ya mtumishi kupitia ujumbe wa maandishi katika simu ya mkononi (SMS).

Alieleza pia kwamba, huduma hiyo ya SMS itakuwa bure kwa kipindi cha miezi mitatu ya kwanza.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, alisema uamuzi wa serikali wa kuwezesha walimu hao kupata mishahara yao kwa wakati, ni jambo la kujivunia kwa vile halijawahi kutokea.

“Hatua hii ni kitu cha kujivunia, itafanya elimu iwe bora nchini kwani walimu hawatakuwa wakipoteza muda mwingi kushughulikia mishahara yao pasipo uhakika,” alisema Waziri Sitta


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.