Na. M. M. Mwanakijiji
Kuna wakati katika Tanzania rushwa haikuwepo na huduma za umma zilikuwa zinapatikana bila mtu kulazimika kulipa kitu kidogo. Hata hivyo, hii leo rushwa imekita na kuota mizizi katika jamii yetu kiasi cha kwamba tumeikubali na kuichukulia kama ukweli wa maisha yetu.
Licha ya juhudi na mikakati mingi ya kupambana na rushwa na ufisadi katika serikali, tatizo la rushwa limeonekana kuwa haliondoki na kuna baadhi ya watu wamefikia mahali pa kuamini kuwa hakuna jinsi ya kushinda tatizo hilo.
Kwa watu hao, Watanzania hawana budi kujifunza kuishi na rushwa katika nchi yao. Licha ya kwamba watu wengi tunaichukia rushwa kinadharia, wengi wetu hata hivyo tunajikuta tukitoa au kupokea rushwa kwa sababu ndiyo ukweli wa mambo ulivyo.
Kero hii ya rushwa ilikuwa imefikia pabaya hadi Mwl. Nyerere akajikuta akitamka kuwa Ikulu inanuka rushwa. Siyo kusudio langu kuelezea historia ya rushwa katika Tanzania au athari zake kwa jamii kwani hayo yanaeleweka kwa wengi na kuna vyombo vingi ambavyo vimejitahidi kuelezea kwa kina.
Hata hivyo, lengo langu hasa ni kuonesha kuwa endapo serikali ya Tanzania itarekebisha na kubadilisha siyo tu kima cha mshahara au madaraja ya ajira na mishahara inayoenda nayo bali pia mfumo zmzima wa ulipaji mishahara ndipo vita dhidi ya rushwa itaanza kuonesha mafanikio.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha watu kutoa na kupokea rushwa. Kati ya zile zinazosababisha watu kupokea rushwa kubwa mbili huwa zinatajwa; tamaa ya utajiri wa haraka na umasikini wa kipato.
Zile zinazosababisha watu watoe rushwa kubwa ni kuondoa kero ya kupata huduma ambayo ni ya bure au ya bei rahisi kwa kupewa kipaumbele na pia kuharakisha kupewa huduma hiyo ambayo pasipo rushwa basi hucheleweshwa.
Kwa muda mrefu, rushwa katika Tanzania imepiganwa haswa kwa kutoa elimu ya haki za raia na hasa kuonesha ubaya wa rushwa na jinsi rushwa inavyo haribu utendaji haki, inadumaza uwajibikaji, na kuharibu utendaji kazi wa vyombo vya umma.
Vipindi kama vya Mikingamo na kampeni za Vita dhidi ya Rushwa vilisaidia sana kuonesha ubaya wa rushwa lakini vilishindwa kabisa kuondoa au kupunguza gonjwa hilo sugu.
Udhaifu mkubwa wa kampenzi za rushwa katika Tanzania uko kwenye kukaribiri tatizo hili haswa upande wa watoa rushwa kwa kuamini kuwa watu wakipatiwa elimu ya kutosha dhidi ya rushwa basi wataacha kutoa rushwa.
Matokeo ya kampeni hizo yanasikitisha, kwani rushwa imeendelea kushamiri na kuota mzizi karibu katika kila eneo la utendaji kazi wa vyombo vya umma.
Baada ya kuangalia mfano wa nchi nyingi zilizoendelea ambapo rushwa ndogondogo imepunguzwa kwa kiasi kikubwa, nimeonelea kutoa mapendekezo yafuatayo ambayo wenzetu wametumia na ya kuwa sisi nasi tukianza kutumia bila ya shaka tutapunguza tatizo la rushwa.
Kiini cha rushwa katika sehemu yoyote duniani ni tamaa ya fedha, umasikini, na haya ya utajiri wa haraka haraka nikitaja sababu chache. Hivyo, ili kupunguza na ikiwezekana kuondokosha kabisa rushwa hatuna budi kurudi kwenye fedha, fedha, na fedha tu.
Katika kupigana na tatizo hilo la rushwa basi, si lazima tutumie mabadiliko ya sheria ya uhalifu peke yake au zaidi kama ilivyo sasa na inavyopendekezwa na watu wengi.
Ukweli wa mambo ni kuwa tunazo sheria nyingi na taratibu nyingi ambazo zimeshindwa kabisa kutupunguzia kama sio kutuondoshea tatizo la rushwa. Sheria hizi nyingi zaidi ya kushindwa, zenyewe ni dhaifu na zisizo na nguvu ndani yake.
Kutegemea sheria peke yake au elimu peke kupigana na tatizo la rushwa, ni kujipa matumaini ambayo kwa kweli hayapo.
Hivyo katika kukabiliana na tatizo hili na hatimaye kupunguza kwa kiasi kikubwa makali yake katika jamii, napendekeza mambo ambayo yana pande mbili.
Moja, ni mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji kazi (structural and operational change) hususan kwenye suala la ulipaji mishahara kukiwa na lengo la kupunguza mianya na sababu za rushwa; pili, ni suala la kisheria ambapo lengo litakuwa ni kuvipa uhuru na meno zaidi vyombo vile vinavyohusika moja kwa moja na vita hii dhidi ya rushwa.
Haitoshi kufanyia mabadiliko au kuleta sheria mpya ya rushwa bila kufanyia mabadiliko sheria ya kazi au ya utawala kazini.
Mabadiliko ya Muundo
Kama mnavyojua Rais Kikwete aliahidi wakati wa siku kuu ya Mei Mosi kuunda tume ya kuboresha maslahi ya watumishi wa serikali. Hatimaye tume hiyo iliundwa ikiongozwa na Deogratias Ntukamazina. Tume hiyo ilipewa majukumu sita ambayo ni:
1. Kuainisha misingi muhimu itakayoongoza suala zima la mishahara kwa Watumishi wa Umma.
2. Kuainisha vigezo vitakavyotumika katika kuweka viwango vya mishahara na uwiano wa viwango hivyo miongoni na kati ya makundi na ngazi mbalimbali za Watumishi.
3. Kupendekeza kanuni zitakazotumika katika kufikia viwango vya mishahara ya Watumishi.
4. Kutoa mapendekezo ya kuainisha mishahara kwa makundi mbalimbali ya Watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, na Taasisi zote zinazotegemea fedha kutoka bajeti ya Serikali.
5. Kupendekeza utaratibu na mfumo unaofaa katika kuhuisha mara kwa mara mishahara na maslahi ya Watumishi wa Umma.
6. Kuangalia uwezekano wa kuunda chombo cha kudumu cha kuhuisha mishahara Serikalini {Wages and Salary Board).
Hivyo, utaona kuwa katika mambo hayo sita hakuna jambo linalohusu namna ya kulipa mishahara. Aidha kwa watu kutoona umuhimu wake au kutokuelewa uhusiano uliopo kati ya ulipaji mishahara na tatizo la rushwa.
Hoja yangu hapa ni kuwa, kuna uhusiano mkubwa kati ya jinsi na namna watu wanalipwa mishahara yao na vitendo vya kujihusisha na rushwa. Tunaweza kuwalipa watu mamilioni ya fedha lakini bado wataendelea kujihusisha na rushwa, kwani tatizo si kiasi tu cha fedha bali jinsi kiasi hicho kinavyowafikia.
Chukulia kwa mfano, kijana amemaliza chuo cha ualimu na amepangiwa kwenda kuanza kufundisha shule ya Mtakuja. Kijana huyo anaenda kijiji cha Mtakuja kama mwalimu kwa mara ya kwanza, hana nyumba, samani, n.k Ili aweze kuishi na kuanza maisha hana budi kuwa na fedha kiasi, posho ya safari n.k haitoshi hivyo anajikuta anakupa labda kwa walimu wenzake au kwa mmoja wa wafanyabiashara wa duka la Mtakuja.
Anawaahidi kuwa pindi akipata mshahara wake wa kwanza atawalipa. Mshahara wake wa kwanza unachukua miezi mitatu kuja, wakati huo Mwalimu wetu ana deni la zaidi ya shilingi laki moja na nusu.
Mshahara na marupurupu yote yanafikia karibu shilingi laki tatu hivi. Mwalimu wetu hana jinsi bali lazima alipe lile deni na hivyo anajikuta amesaliwa na shilingi laki moja na nusu na baada ya kubajeti kwa kadiri anavyoweza anajikuta mfukoni baada ya matumizi ya lazima amebakiwa shilingi hamsini elfu tu. Mshahara wake mwingine ni siku thelathini zijazo.
Mwalimu wetu anapata nafasi ya kusimamia jukumu fulani hapo shule, jukumu ambalo linampa nafasi ya kupokea michango, ada, na malipo mbalimbali.
Hatimaye anagundua kuwa huduma yake hiyo ni muhimu sana kwa jamii hivyo anaanza kudai pesa kidogo ili aweze kufanya jambo fulani kwa haraka kwa mzazi wa mwanafunzi fulani. Mwisho wa wiki anajikuta ana shilingi elfu kumi za ziada!
Hivyo, mwalimu wetu atakuwa ameanza kamchezo karushwa ndogondogo ili kukabili madeni ya hapa na pale na matumizi ya kila siku, na mara akiisha anza kuzoea maisha hayo mazuri ambapo ana fedha ya ziada ya matumizi ya lazima na anasa inakuwa vigumu kwake kutokutaka au kupokea rushwa! Mfano huo unawahusu mapolisi wanaoanza kazi vituoni, madaktari n.k
Ninachosema hapa ni kuwa utaratibu wa kuwalipa watu kila mwisho wa mwezi umepitwa na wakati kwani ndio umekuwa sababu kubwa ya kuchochea vitendo vya rushwa ndogondogo,umedumaza utendaji kazi, na umechangia ukosefu wa nidhamu ya kazi.
Ni mtindo huu unaowalazimisha watu waende kutafuta kibarua cha ziada wakati wa kazi ili kuweza kukidhi mahitaji ya wiki za mwezi zilizosalia.
Haijalishi unamlipa mtu kiasi gani kwani kama mtu huyo anaanza kazi kwa madeni au anajikuta ana madeni na inambidi asubiri siku thelathini kupata pesa toka mwajiri wake basi tamaa na haja kupokea rushwa kidogo inaongezeka.
Inakuwaje basi tukiamua kumlipa polisi wetu mara moja kwa wiki shilingi hamsini elfu badala ya kusubiri mwisho wa mwezi kupewa laki mbili? Utaona kuwa polisi huyo hatataka rushwa ya shilingi mia tano ili mwisho wa wiki awe na shilingi ishirini elfu wakati asipopokea rushwa bado atakuwa na shilingi hamsini elfu!?
Daktari ambaye anasubiri mwisho wa mwezi alipwe shilingi laki tano wakati ana madeni na matumizi ya shilingi laki tatu, atafurahi zaidi kama atajua kuwa kila baada ya wiki mbili analipwa shilingi laki mbili na nusu.
Hivyo basi wakati tume hii inamalizia maoni yake haina budi kuangalia namna ya kulipa mishahara kama eneo muhimu na nyeti ambalo tukiliangalia vizuri linaweza kuwa ndiyo kiini cha kushinda vita dhidi ya rushwa.
Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa madaraja ya chini yaani wale wanaoshughulika na wateja na wananchi kila siku wanalipwa mara moja kwa wiki wakati wale walio katika utawala wanalipwa angalau mara mbili kwa mwezi. Jambo la msingi ni kuondokana kabisa na malipo ya mwisho ya mwezi!!!
Katika hili la kulipa mishahara hatuna budi kuondokana pia na utaratibu wa kulipa watu kwa siku thelathini hata kama hawakutokea kazini au walikuwa kwenye vibarua vyao.
Hatuna budi kuja na utaratibu utakaolazimisha watu kuwa kazini na siyo tu kuwa kazini bali pia kufanya kazi. Mtindo wa mtu kwenda ofisini na kuzuga zuga hadi muda wa kuondoka ufike na mwisho wa mwezi anapokea mshahara wake ni mfumo mbaya ambao umechangia kwa kiasi kikubwa wachache kufanya kazi kweli wakati wengine wanatanua.
Kama mtu anajua kuwa afanye kazi sana au kidogo, awe makini au la, mshahara mwisho wa mwezi utafika tu, kuna msukumo gani wa mtu huyo kufanya jitihada?
Ni kwa sababu hiyo basi napendekeza pia kuwa licha ya kuongeza kima cha chini kifikie angalau shilingi laki tatu, bali pia kuwapa watu uamuzi wa kuifikia hiyo laki tatu kwa muda wa masaa wanayofanya kazi.
Maana yangu ni hii, badala ya kuwalipa watu kwa siku thelathini ambazo wanaweza kuwa wamefanya kazi au la, kwanini tusiwalipe watu kwa masaa ambayo walikuwapo kazini na kama alikuwapo kazini masaa arobaini (nane kila siku au tisa) basi hizo shilingi laki tatu ni zake.
Nikitumia mfano huo wa kima cha chini utaona kuwa kwa wiki mtu ana uwezo wa kulipwa shilingi elfu sabini na tano kama atafanya kazi masaa hayo arobaini ambapo kila saa itakuwa ni sawa na shilingi 1875 kwa saa.
Jinsi gani tunaweza kuanza kulipa madaraja fulani kwa masaa na madaraja mengine kwa mikataba ni jambo ambalo liko nje ya mada hii. Hata hivyo tukifanya mambo hayo basi tutapunguza sana vitendo vya rushwa ndogondogo.
Mabadiliko ya Kisheria
Mabadiliko mengine muhimu ni ya sheria nzima ya kazi na ile ya kuzuia rushwa. Kwa upande wa kazi mabadiliko yanayotakiwa ni uwezo wa mtu kufukuzwa kazi mara moja kwa sababu yoyote au bila ya sababu, na uwezo wa mtu kuacha kazi mwenyewe kwa sababu yoyote au bila sababu yaani ajira kwa hiari.
Tatizo moja tulilonalo sasa hivi ni kulazimisha mikataba ya kazi kiasi cha kwamba inakuwa vigumu kiongozi kumfukuza mtu kazi kwani vyama vya wafanyakazi vitapiga kelele.
Wakati umefika wa kuhakikisha kuwa maeneo fulani ya kazi ajira ni kwa hiari na hata kwenye mikataba mameneja wana uwezo wa kumfukuza mtu kazi kwa sababu ya kinidhamu, tuhuma n.k bila kusubiri vikao vya kazi au mahakama ya kazi.
Kuwapa waajiri uwezo huu na kuhakikisha kuwa haki za kiraia zinalindwa kutachangia kwa kiasi kikubwa watu kuwa waangalifu. Kama meneja amemuona mfanyakazi wa chini akipokea fedha kwa njia ya pembeni, badala ya kumbembeleza awe na uwezo wa kumfukuza papo hapo!
Nidhamu ya kazi itarudi na watu watafikiri mara mbili kupokea rushwa ya shilingi elfu tano wakati mwisho wa wiki anapata shilingi elfu hamsini!
Kwa wale ambao tumeishi nchi zenye mfumo kama huo wa kazi utaona kuwa ukijaribu kumpa mtu rushwa ya dola 20 ili akufanyie jambo fulani atakushangaa kwani mwishoni mwa wiki anapokea dola mia nne au mia tano!
Kwa upande wa taasisi ya rushwa, ni lazima iwezeshwe kwenye maeneo yafuatayo:
a. Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Rushwa (PCB) ateuliwe na Rais lakini lazima athibitishwe na Bunge na hawezi kuondolewa isipokuwa kwa amri ya Mahakama, hata Rais aliyemteua asiwe na uwezo wa kumuondoa.
b. Kikosi cha Kuzuia Rushwa kipewe uwezo wa kufanya uchunguzi wa chinichini kwa njia za kielektroniki na kurekodi mazungumzo ya simu (surveillance and wiretapping). Kikosi hicho kiwe na uwezo wa kufanya mambo hayo kwa kibali cha mahakama (court warrant) na kiwe na uwezo wa kufanya hivyo kwa mtu yeyote katika Jamhuri ya Muungano au raia wa Tanzania mahali popote.
c. Kwa vile kikosi cha PCB kitakuwa na nguvu (b) ni lazima kihakikishiwe uhuru wake kwa kupewa uwezo wa kumchunguza kiongozi yeyote kwa kibali cha mhimili mwingine wa nchi.
Kwa mfano, kama kiongozi anayetaka kuchunguzwa ni jaji, basi Rais atoe kibali hicho kama anayetakiwa kuchunguzwa ni, Waziri, au Mbunge basi mahakama itoe kibali hicho na kama anayetakiwa kuchunguzwa ni Rais basi Spika atoe kwa niaba ya Bunge aidhinishe uchunguzi huo wa siri.
Kiongozi yeyote atakayekataa kumchunguza kiongozi wa mhimili mwingine alazimishwe na sheria kusema kimaandishi kwa nini akubaliani na uamuzi wa kumchunguza mtu huyo.
Basi kama tukijaribu kufanya mambo haya, nina uhakika tutajenga mazingira mazuri ya kupambana na rushwa na hatimaye tutaipunguza kwa kiasi kikubwa kama siyo kuitokomeza kabisa.
Ni wazi kuwa sikuweka mapendekezo yote kwani yapo mambo mengi ambayo yanaweza kufanyika. Kwa maoni yangu hilo la kubadilisha mfumo wa ulipaji mishahara ni msingi mkubwa wa kushinda rushwa ndogondogo.