MWANAMKE mmoja, mkazi wa Kijiji cha Ntuchi Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuiba mtoto mwenye umri wa siku tatu katika Hospitali ya Wilaya ya Nkasi ya Namanyere.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Germanus Mponguliana alisema kuwa, mwanamke huyo alikamatwa Desemba 10, mwaka huu majira ya asubuhi wakati akiwa katika harakati za kutoroka na mtoto huyo.
Mponguliana alisema mwanamke huyo aliiba mtoto huyo wakati mama yake akiwa bado hajazinduka usingizini kutoka na dawa za usingizini alizopewa wakati akifanyiwa upasuaji baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.
" Mtuhumiwa huyo alikamatwa na wauguzi wa hospitali hiyo mara baada ya kuanza kuhangaika ni njia ipi apite na mtoto huyo... ndipo wahudumu hao walipomgundua na kutoa taarifa getini kwa mlinzi kisha mlinzi akamzuia getini," alisema
Kaimu Kamanda huyo alisema mwanamke huyo alipohojiwa na mlinzi alidai kuwa, amembeba mtoto huyo kwa lengo la kwenda kumnunulia nguo dukani, lakini baadaye alikiri kuwa mtoto huyo si wa kwake bali alikuwa na lengo la kutoroka naye.
Mwanamke huyo anatarajia kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka baada ya upelelezi kukamilika.