Na Stephano Simbeye
SAKATA la usambazaji wa mbolea ya ruzuku sasa limeingia katika sura mpya, baada ya serikali kufanya msako na kuwakamata watu 13 waliokuwa wakiuza mbolea hiyo kwa bei ya juu ili kujipatia faida kubwa kinyume na agizo la Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Mbeya, Halima Kihemba, alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Wwanja wa CCM, mjini Vwawa, kufuatia ombi la mkazi mmoja Hamisi Jemadari kwa Serikali kuwa iweke ruzuku katika mbolea yote ili kuepuka kuwafikia watu wachache wenye tamaa ya kujipatia faida kubwa.
Kihemba alisema kufuatia taarifa walizozipata kutoka kwa raia wema, walifanya msako na kuwakamata wafanyabiashara 13 waliokuwa wameficha mbolea ya ruzuku kwa lengo la kuiuza kwa bei kubwa tofauti na iliyopangwa na Serikali.
Alisema wilaya ya Mbozi inahitaji zaidi ya tani 28,000 za mbolea za chumvi chumvi, lakini imepatiwa tani 7,200 ambazo hakitoshelezi mahitaji halisi ya wananchi wa wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa watu hao watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.
Baadhi ya wakulima walieleza kuwa tatizo la kuanza kulanguliwa kwa mbolea ya ruzuku linatokana na baadhi ya mawakala waliopewa vibali vya kuchukulia mbolea hiyo kwa ajili ya kuisambaza kwa wakulima, hushindwa kuifikisha kwa walengwa, badala yake wameificha na kuiuza kwa bei kubwa.
Wakazi wa Kijiji cha Masangula wamemueleza mwandishi wa habari hizi kuwa wakala wao hana duka la kuuza pembejeo katika kijiji hicho na kuuzia Vwawa mjini, ambako wao wakienda huambiwa mbolea imekwisha hivyo kulazimika kununua kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa ya kati ya Sh25,000 na 29,000 badala Sh19,500.
Tathimini ya awali ya ugawaji wa mbolea ya ruzuku mwaka huu inaonyesha kuwa utaratibu wa kuwatumia mawakala wa vijijini kusambaza mbolea hiyo ni chanzo cha matatizo mengi yaliyojitokeza.