Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Sita wafungwa jela kwa wizi wa fedha NBC Moshi
Sita wafungwa jela kwa wizi wa fedha NBC Moshi
By Habari Tanzania | Published  12/15/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Daniel Mjema

WASHITAKIWA wanne kati ya 14, wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12, baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kushiriki tukio la wizi wa kutumia silaha katika benki ya NBC tawi la Moshi.

Inawezekana hukumu hiyo iliyosomwa juzi na Hakimu Mkazi kutoka Dar es Salaam, Amir Mruma, ikawa imeweka rekodi baada ya kusomwa kwa saa nane mfululizo kuanzia saa 7.15 mchana hadi saa 2.30 usiku.

Likiwa ni jambo jipya kabisa kuwahi kuonekana mkoani Kilimanjaro, mahakama iliwekewa kipaza sauti ndani ya mahakama na spika nje ili kuwawezesha maelfu ya wasikilizaji waliofurika kusikiliza hukumu hiyo.

Kilichowagusa wengi ni staili ya washitakiwa hao kuendesha misa maalum ndani ya chumba cha mahakama, muda mfupi tu baada ya kuingia, hali iliyowafanya baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki kububujikwa na machozi.

Hali ya ulinzi katika eneo lote la mahakama ilikuwa si ya kawaida ambapo polisi wa vikosi vya FFU, mbwa, farasi na makachero wa jeshi hilo wakiwa na silaha nzito, walionekana wakishika doria katika eneo lote la mahakama.

Waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 kila mmoja ni pamoja na mshitakiwa wa kwanza, Jackson Ole Nametemi, mshitakiwa wa pili na wa tatu ambao ni ndugu, Benjamin Dia na Kelvin Dia. Mwingine aliyeingia katika kundi hilo ni mshitakiwa wanne, Jacob Raphael Kalaghe

Pia mahakama hiyo imewahukumu washitakiwa wengine wawili kifungo cha miaka mitatu jela kwa kupokea mali iliyopatikana kutokana na fedha za wizi huo.

Washitakiwa hao ni wa tisa, Happy Memei aliyepokea gari aina ya Suzuki Escudo T 206 ACU iliyonunuliwa na mshitakiwa wa kwanza na Evelyne Mlaki aliyeshiriki kuficha Sh47,872,000 za mshitakiwa wa kwanza.

Washitakiwa wengine wanane, wakiwamo polisi wanne, wawili wakiwa ni wale waliokuwa katika lindo siku ya tukio wengine wanne kwa waliachiwa huru kukosekana kwa ushahidi dhidi yao.

Polisi walioachiwa huru ni Seif Makono, Mohamed Mnunguye, Jovin Mogera na Stide Kahamba, wakati raia walioachiwa ni Happy Mlaki ambaye ni mke wa mshitakiwa wa kwanza na Asina Abdallah, mke wa Makono.

Wengine walioachiwa ni shangazi wa Kalaghe, Grace Adriano na mganga wa kienyeji, Ramadhan Juma.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mruma, ambaye aliteuliwa wiki iliyopita kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alisema vitendo vya wizi katika benki nchini vilivyoanza hivi karibuni, vinaendelea kushika kasi isiyo ya kawaida.

Hakimu huyo alisema mahakama haiwezi kuvumilia vitendo hivyo na kulielezea tukio la uporaji NBC kuwa ni la kihistoria kwa kuwa kiasi cha Sh5.3 bilioni kilichoporwa ni kikubwa mno kuwahi kuibwa katika historia ya nchi.

“Ili kuzuia kasi ya vitendo hivi, ni lazima mahakama itoe adhabu zinazokatisha tamaa watu wanaopanga kufanya vitendo hivyo,” alisema Mruma na kueleza kuwa adhabu ya wizi wa kutumia silaha iko wazi kuwa ni miaka 30 jela.

Akiainisha ushahidi huo, Hakimu Mruma alisema mahakama imeridhika pasipo shaka kuwa mshitakiwa wa kwanza, Ole Nametemi na wa nne, Kalaghe walikula njama na kushiriki katika wizi huo.

Alifafanua kuwa kitendo cha Ole Nametemi kukamatwa na orodha ya majina ya baadhi ya watuhumiwa, akiwamo Kalaghe na wengine ambao hawajakamatwa, kinathibitisha kuwa walikuwa wakifahamiana na kula njama pamoja.

“Katika orodha ile kuna mtu anatajwa kama Mchungaji ambaye anaonekana alilipwa Sh150,000 na ushahidi unaeleza kuwa kuna Mchungaji alikodisha gari lililotumika katika ujambazi na kulipa malipo ya awali ya Sh160,000,” alisema Hakimu Mruma na kuongeza;

"Kuna mtu anaitwa Leon Mushi ambaye ametajwa sana na mashahidi na katika orodha aliyokamatwa nayo Ole Nametemi kuna jina pia la Mushi naamini ndiye huyo anayetafutwa.”

Mruma aliukataa utetezi wa mshitakiwa huyo kuwa waliotajwa katika orodha hiyo ni wateja wake, akisema kama ilikuwa ni hivyo basi mshitakiwa alipaswa kuleta watu wenye majina hayo kuthibitisha kuwa sio wale wanaotafutwa.

Kulingana na tathmini ya ushahidi, Hakimu Mruma alisema kitendo cha Ole Nametemi kupangisha nyumba ambayo baadaye ilitumiwa na watuhumiwa wa Kenya na Uganda kinaonyesha kiwango kikubwa cha ushiriki wake.

“Mshitakiwa (Nametemi) anajitetea kuwa nyumba hiyo aliikodisha ili kuanzisha ofisi ya kampuni ya utalii, lakini hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kuna taratibu zilianza za kuanzisha kampuni hiyo,” alisema Mruma na kuongeza;

“Kuna ushahidi kuwa Ole Sademak ambaye ni dereva wa Riverside Shuttle, aliwabeba watuhumiwa hao wa kigeni kutoka nyumba hiyo na Nametemi anakiri anamfahamu Patrick Ingoi aliyekuwa ni kiongozi wa genge hilo.”

Hakimu Mruma alisema mshitakiwa huyo alitambuliwa kikamilifu na mashahidi watatu wa upande wa mashitaka kuwa ni miongoni mwa majambazi waliokuwa ndani ya benki hiyo, wakipora fedha kwa mtutu wa bunduki.

“Nimeridhika gwaride la utambulisho liliendeshwa kwa kufuata taratibu na hakuna sababu zozote za msingi zilizotolewa kuonyesha ni kwa nini mashahidi hao wamsingizie mshitakiwa huyo.”

“Pili mshitakiwa alikuwa na kiasi kikubwa cha fedha (Sh47,872,000) na maelezo aliyoyatoa kuhusiana na fedha hizo hayalingani,” alisema Hakimu Mruma.

Mathalani, anasema wakati mshitakiwa alijitetea kuwa yeye ni wakala wa kuuza madini na alikuwa akilipwa kwa kamisheni lakini Thobias Mamy aliyemwita amtetee anasema alikuwa akinunua mzigo kwa fedha taslimu.

Kuhusu Benjamin Dia na Kelvin Dia, Hakimu alisema kuna mashaka makubwa kutokana na matendo yao na jinsi walivyoweza kuwa na fedha nyingi katika kipindi kifupi cha mwezi wa tano pekee muda mfupi baada ya tukio la wizi.

Vivyo hivyo kwa mshitakiwa wa nne, Kalaghe, Mahakama iliukataa utetezi wake kuwa Sh38 milioni alizokamatwa nazo akiwa amezichimbia ardhini ilikuwa ni sehemu ya mkopo wa Sh40m aliopewa na mchungaji Ashery Ashery.

Kuhusu polisi waliokuwa zamu, Hakimu alisema kwa mujibu wa taratibu za benki hiyo, polisi hao hawakuwa na uwezo wa kumhoji au kumpekua mteja yoyote anayeingia ndani na mwanya huo ndio uliotumiwa na majambazi.

Mruma alifafanua kuwa hata mikataba kati ya benki na wateja wakubwa ya kutumia mlango wa nyuma haikuwa inafahamika kwa polisi hao hivyo wasingekuwa na uwezo wa kumhoji mteja wa aina hiyo.

Kulingana na ushahidi huo, tuhuma dhidi ya watuhumiwa wengine wakiwemo polisi wengine wawili walioachiwa, ulijengwa katika mazingira na maelezo yake yalikuwa hafifu kuthibitisha shitaka dhidi yao.

Kuhusu mshitakiwa wa 11, Evelyne Mlaki, Hakimu Mruma alisema kitendo cha mshitakiwa huyo kuhamisha sanduku lililokuwa na fedha za mshitakiwa wa kwanza na kulificha, kilidhihirisha wazi alikuwa akifahamu jambo hilo.

Hakimu Mruma ameamuru mali na fedha walizokamatwa nazo washitakiwa ambao waliachiwa huru hiyo juzi, zirejeshwe kwao iwapo hakutakuwa na rufaa kupinga maamuzi dhidi yao kutoka upande wa Jamhuri.

Kadhalika, Mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa zaidi ya Sh167 milioni, magari matatu na mali nyingine za mamilioni walizokamatwa nazo watuhumiwa ili zifidie fedha za NBC zilizoporwa katika tukio hilo.

Alifafanua kuwa mali kama magari na vitu vingine vitauzwa kwa mnada na dalali atakayeteuliwa na mahakama chini ya uangalizi wa benki ya NBC na polisi na fedha zitakazopatikana zitaifishwe na kurejeshwa NBC.

Hata hivyo baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, mawakili wa utetezi, Loom Ojare na Midian Mwale waliliambia Mwananchi kuwa watakata rufaa haraka iwezekanavyo kupinga hukumu hiyo.

“Tumeshamuarifu Hakimu kwamba tunakata rufaa na ametuahidi atatupatia nakala ya hukumu mapema na ndani ya muda wa rufaa…tunakwenda Mahakama Kuu kupinga hukumu hii,” alisema Mwale.

Kwa upande wake, wakili wa Serikali, Yohana Massara ambaye ni mmoja kati ya mawakili wa serikali aliyeendesha kesi hiyo, alionekana mwenye furaha kutokana na hukumu hiyo iliyowatia hatiani watuhumiwa sita.

Pamoja na hukumu hiyo kuchukua muda mrefu, lakini si wananchi wala mahakimu wa mahakama ya wilaya ya Moshi na wafanyakazi walioondoka mahakamani hadi hakimu alipomaliza kuisoma.

Baada ya hukumu, ndugu wa washitakiwa waliofungwa walionekana kububujikwa na machozi, lakini kwa wale ambao ndugu zao waliachiwa, walikuwa na furaha isiyo na kifani huku wengine wakibubujikwa na machozi.

Katika tukio lisilo la kawaida, mke wa Stide ambaye jina lake halikupatikana, alizimia ghafla kwa muda nje ya mahakama baada ya kusikia mumewe ameachiwa huru. Kwa ujumla hali ilikuwa ni ya mkanganyiko.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.