Na Waandishi Wetu, Lindi na Dar
WAKATI siku 14 alizotoa Rais Jakaya Kikwete kwa wanunuzi wa korosho kununua zao hilo kwa wakulima ulimalizika Jumatatu wiki iliyopita, wananchi wilayani Liwale, Lindi wamesema agizo hilo limepuuzwa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamelalamika kuwa bado korosho zao hazijanunuliwa na zimelundikana majumbani mwao.
Wamedai kuwa tangu kufunguliwa kwa msimu wa ununuzi mwezi Novemba, mwaka huu, ni kampuni moja tu iliyojitokeza kununua korosho wilayani Liwale, hali inayowapa mashaka kuwa huenda msimu huu wasiuze kabisa korosho zao.
Hashim Mohamed, mkazi wa Kijiji cha Mbuli-Kichonda, aliitahadharisha serikali kwamba kama jitihada za makusudi hazitafanyika, huenda mwakani wananchi wa Liwale wakakumbwa na baa kubwa la njaa kutokana na kushindwa kuandaa mashamba mapema kwa kupoteza muda mwingi kwenye vituo vya kuuzia korosho.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Umoja wilayani Liwale, Hassani Myao, alisema katika historia ya zao la korosho, haijawahi kutokea wanunuzi wakafanya mgomo baridi kama mwaka huu na kuiomba serikari kuchunguza kwa kina chanzo cha hali hiyo na kuchukua hatua za haraka ili kuwanusuru wakulima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima na Wafugaji wilayani hapa, Mohamed Mpotto, aliiomba serikali kutoa kauli nzito yenye kuheshimiwa, kwani licha ya Rais Kikwete kutoa siku14 kwa wanunuzi wa korosho kuhakikisha wananunua kulingana na leseni zao, hadi sasa hakuna mabadiliko yaliyotokea Liwale.
Alisema wananchi wilayani Liwale wana imani kubwa na Rais Kikwete, hivyo wamemuomba aingilie kati ili kuwanusuru wakulima wa korosho ambao wengi wao wamekatishwa tamaa na hali hiyo na kuhisi pengine serikali imeshindwa kuwasaidia.
Wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya uhuru kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Liwale, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Said Sadick, aliwataka wakulima wa korosho kuwa na subira wakati serikali inafuatilia kwa karibu tatizo la soko la zao hilo.
Aliahidi kuwa tatizo hilo litakwisha muda si mrefu kufutokana na jitihada za serikali katika kutafuta ufumbuzi.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, mkuu huyo wa mkoa alisema serikali inatambua tatizo na kwamba wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alikuwa kwenye mkutano uliowajumuisha wanunuzi wa zao la korosho na kuahidi kutoa taarifa zaidi baada ya kikao hicho.
Akiwa jiji Dar es Salaam jana, Sadick alikiri kuwa katika wilaya ya Liwale mambo hayajaenda sawa, kwani kati ya tani 5,000 walizonazo wakulima, zimenunuliwa tani 700 tu.
Alisema kutokana na hali hiyo amelazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kujaribu kuwashawishi wanunuzi hao kwenda Liwale kununua korosho za wakulima.
Hata hivyo, alisema kimkoa lengo la ununuzi wa zao hilo mkoani mwake halijafikiwa lakini kuna mafanikio makubwa ambapo tani 45,000 za korosho zimeshanunuliwa kati ya tani 78,000 zinazokadiriwa kuwa zimezalishwa na wakulima wa mkoa huo.
Hivi karibuni gazeti dada la Mwananchi, The Citizen lilikariri taarifa kwamba uingiazaji wa wa korosho za magendo kutoka Msumbiji unachangia kwa kiasi kikubwa kushusha soko la zao hilo hapa nchini.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, bei ya korosho Msumbiji ilikuwa ni chini ya Sh300 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya hapa ambayo ni Sh600 kwa daraja la kwanza na Sh480 daraja la pili