Na Mwandishi Wetu
WADAU wa sekta ya habari nchini waliokutana jijini Dar es Salaam jana kupitia rasimu ya muswada wa sheria ya uhuru wa habari, wameeleza kutokuridhishwa kwao na mapendekezo yaliyoko kwenye rasimu hiyo.
Katika mkutano wa majadiliano ulioitishwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na kuhudhuriwa na wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na wanaharakati wa uhuru wa habari, waliazimia kuwasilisha mapendekezo yao serikalini kuhusiana na rasimu hiyo.
Wadau hao pamoja na kutambua maeneo yanayochangia mwekeleo mzuri wa kukuza uhuru wa habari nchini katika rasimu hiyo, sehemu kubwa ya muswada huo umeelezwa kwamba unapingana kabisa na misingi ya kukuza na kuendeleza uhuru wa habari ambao ni nguzo muhimu katika kukuza demokrasia na utawala bora.
Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Reginald Mengi, alisema ni vizuri maneno ya serikali yakaendana na matendo, na kwamba rasimu ya muswada huo hauonyeshi kuuwiana kwa maneno na matendo ya serikali.
Alisema kwamba kitu kinachoshangaza ni kwamba badala ya muswada huo kuongeza nguvu ya kuleta uhuru wa habari nchini, unalenga kupokonya hata zile taasisi chache za kukuza uhuru huo ambazo zimejengwa na wadau wa uhuru wa habari wenyewe.
Mengi alisema usiri ni mama wa rushwa, na kamwe vita dhidi ya rushwa haiwezi kufanikiwa kama dhamira ya kufanya kazi katika mazingira ya usiri itaendelezwa.
Awali akichambua muswada huo, Dk Sengodo Mvungi, alisema mapendekezo yaliyoko kwenye muswada huo ya kuundwa kwa Bodi ya Viwango vya Habari inalenga kupora madaraka ya Baraza la Habari.
Alisema muswada huo unataka kutwaa madaraka ya MCT kwa kuunda sheria ambayo inanyang’anya mafanikio yaliyofikiwa na wadau wote wa habari nchini mwaka 1993 walipounda MCT baada ya mapambano makubwa dhidi ya mapendekezo ya serikali ya kuunda baraza la kisheria.
Maoni ya Dk Mvungi pia yalifanana na Mohamed Tibanyendera, Afisa kutoka Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa-Tan), kwamba muswada huo unakosa vigezo vingi vya kuweza kuufanya kutoa uhuru wa kupata habari kwa kiwango cha juu kabisa kama msingi mmojwapo muhimu wa kutungwa kwa sheria ya uhuru wa habari.
Kutokana na mapungufu yaliyobainika katika rasimu hiyo, wadau wamekubaliana kwamba juhudi sasa zielekezwe katika kuboresha muswada huo na kuuwasilisha serikalini mapandekezo hayo.
Katika mkutano wa jana pia uliohudhuriwa na Balozi wa Sweden, ambaye alitoa hotuba ya ufunguzi na kueleza kwamba pamoja na mambo mengine uhuru wa habari ni moja ya nguzo za kujenga mfumo wa kidemokrasia katika jamii yoyote duniani.
Alisema Sweden ni nchi ya kwanza duniani kuwa na sheria ya uhuru wa habari, ikiwa imetungwa mwaka 1766, ambayo imefanya taifa hilo kutambua na kuheshimu haki ya kutoa habari.
Alisema Tanzania kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita vyombo vya habari vimeongezeka kwa idadi na uwezo wa kutoa habari na kujadilia mambo, lakini hatua zaidi zinahitajika kuzidi kuviimarisha vyombo hivyo.
Alisema sheria ya uhuru wa habari itasaidia kuongeza utamaduni wa utawala bora katika nchi, kupambana dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Mkutano huo pia ulikuwa na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Uingereza na Umoja wa Ulaya (EU).