Na Mwandishi Wetu DENMARK imesema itapunguza Sh4.1 bilioni sawa na asilimia 20 ya fedha za msaada katika bajeti kuu ya Tanzania mwakani, baada ya serikali kushindwa kutimiza ahadi yake ya kupeleka bungeni muswada wa sheria mpya ya kupambana na rushwa katika mkutano wa Novemba mwaka huu.
Nchi hiyo iliweka sharti la kutoa msaada kutunisha bajeti kuu ya serikali na asilimia 20 ya fedha zilizoahidiwa zilihusishwa na kurekebisha sheria ya kupambana na rushwa kwa sharti kwamba muswada huo upelekwe bungeni Novemba 2006.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Denmark nchini imesema kuwa kuwasilishwa kwa sheria mpya ya kupambana na rushwa bungeni ilikuwa ni mojawapo ya kipimo cha utekelezaji, kilichokubaliwa na serikali ya Tanzania na washirika wa maendeleo wanaoichangia bajeti ya serikali mwanzoni mwa mwaka huu.
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu wa Kwanza wa Ubalozi huo, Jacob Dal Winther, imeeleza kuwa sheria mpya ya kupambana na rushwa inatarajiwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha vita dhidi ya rushwa.
Alisema sheria hiyo inaweka mazingira ya kupata taarifa na inatoa uwezekano wa kuwaadhibu watu wanaothibitika kuwa ni wala rushwa na pia inalinda watu wanaotoa taarifa za vitendo vya rushwa.
"Kutokana na umuhimu wa sheria hii kwa Tanzania, Denmark ilikubaliana na serikali ya Tanzania kuwa asilimia 20 ya fedha za msaada itakazotoa kwa ajili ya bajeti ziunganishwe na kipimo hiki maalum. Hata hivyo sheria hii haikuweza kuwasilishwa bungeni mwezi Novemba kama ilivyokubaliwa," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Denmark imekubali kuipatia Tanzania msaada wa bajeti wa Sh109 bilioni wa kipindi cha miaka 2006-2010. Sambamba na msaada huo, Denmark inatoa kiasi cha Sh22 bilioni kusaidia kuboresha sekta ya umma katika maeneo ya utumishi wa umma, usimamizi wa fedha za umma na maboresho ya sekta ya sheria.